Upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo Kisiwani Pemba
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba watafanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Kisiwa cha Pemba.
Upimaji huo utafanyika kwa watoto na watu wazima kuanzia tarehe 19/06/2023 hadi tarehe 23/06/2023 saa mbili kamili asubuhi mpaka saa 10 kamili jioni katika Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee.
Kutakuwa na wataalamu wa lishe ambao watatoa elimu ya lishe bora ambayo itawapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na yanaweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.
Watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapohapo au kupewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam.
Tunawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupima afya zenu kujua kama mna matatizo ya moyo ili kuanza matibabu mapema kwa atakayegundulika kuwa mgonjwa.
“Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu”.
Comments
Post a Comment