Bima ya afya kwa wote itawapunguzia wananchi kulipia gharama kubwa za matibabu ya moyo
Na Anna Nkinda - JKCI
Kuanza kutumika kwa bima ya afya kwa wote kutasaidia kupunguza gharama za matibabu ya kibingwa yakiwemo ya moyo na hivyo kuwaondolea wananchi mzigo mkubwa wa kulipia gharama hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama wakati akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipofanya ziara ya kuangalia utoaji wa huduma na mwelekeo wa taasisi hiyo tangu alipoteuliwa kuwa waziri wa afya mwezi Agosti mwaka huu.
Waziri Mhagama alisema gharama za matibabu ya kibingwa ni kubwa na Serikali imekuwa na jukumu kubwa la kulipia gharama za matibabu kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kulipia lakini kuanza kutumia kwa bima ya afya kwa wote kutawasaidia wananchi kupata huduma mahali popote walipo hata kama hawatakuwa na fedha mfukoni kipindi ambacho wataugua.
“Ninawaomba bima ya afya kwa wote ikianza kutumika mjiunge kwani itawasaidia kupata matibabu mahali popote pale mlipo na itasaidia kufuatilia matibabu ya mgonjwa kutoka hospitali yoyote nchini kwani mfumo wa matibabu utakaotumika utakuwa ni mmoja”.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kusaidia mfuko unaohudumia watanzania kuweza kufikiwa na matibabu haya ya kibobezi kwa kutoa zaidi ya shilingi bilioni 6 ili ziweze kusaidia katika utoaji wa huduma hizo na kuanzisha mfumo wa bima ya afya kwa wote”, alisema Mhe. Jenista.
Aidha Waziri Mhagama aliwapongeza wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwa kazi nzuri wanazozifanya na ubunifu walionao katika kutoa tiba hapa nchini na kuona ni muhimu kuwe na mfumo wa kuzizawadia hospitali zinafanya ubunifu wa namna yoyote kila mwaka ili kuweza kuhamasisha maendeleo katika sekta ya afya nchini.
Mhe. Waziri huyo wa Afya alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni taasisi pekee inayoongoza na yenye sifa na heshima ya kutoa matibabu ya kibobezi ya moyo hasa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati hivyo basi aliwaomba wataalamu wa Taasisi hiyo kuendelea kutoa huduma hizo kwa kujitoa kwani wagonjwa wanawategemea wao katika kuokoa maisha yao.
“Ninawasihi uongozi wa JKCI mjitahidi kukuza shughuli na huduma zinazofanywa hapa ikiwemo
kutoa huduma mpya za kibingwa mara kwa mara kwa kufanya hivyo mtapata wagonjwa wengi
kutoka nje ya nchi na kuendelea kuimarisha utalii wa tiba kwani wagonjwa wengi
watakuja kutibiwa hapa”, alisisitiza Mhe. Mhagama.
Kwa upande wa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo walishukuru kwa huduma ya matibabu ya moyo wanayoipata na kusema kuwa kwa kiwango kikubwa imesaidia kuokoa maisha yao na ya watoto wao wenye matatizo ya moyo.
Happy Nkinda kutoka mkoani Geita alimwambia waziri huyo wa Afya kuwa mtoto wake alikuwa akisumbuliwa na tatizo la tundu dogo kwenye moyo kwa muda mrefu na kumpeleka hospitali mbalimbali bila mafaniko mpaka pale alipopewa rufaa ya kwenda JKCI.
“Namshukuru sana Mungu, mara baada ya mtoto wangu kupatiwa matibabu kwa sasa anaendelea vizuri, pia nawashukuru waatalamu wa JKCI kwa huduma zao nzuri na ushirikiano wao kipindi chote cha matibabu”, alisema Happy.
“
Mtoto wangu aligunduliwa kuwa na shida ya moyo katika moja ya hospitali iliyopo
mkoani Mara na kupewa rufaa kuja JKCI ambapo aligundulika kuwa na tundu kwenye
moyo, namshukuru Mungu na wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa
kumfanyia upasuaji na sasa anaendelea vizuri”, alisema Edna.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alimshukuru Mhe. Waziri wa Afya Jenista Mhagama kwa kutembembelea Taasisi hiyo na kuona uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo pamoja na kuwekeza katika rasilimali watu.
“Taasisi
yetu ni moja ya taasisi bora za afya
katika nchi za Afrika Mashariki na Kati hivyo mheshimiwa Waziri amekuja kuona
huduma tunazozitoa, na wagonjwa wengi aliowauliza maswali walimjibu kuwa wameridhika
na huduma tunazozitoa na hii inaonesha
ni jinsi gani wataalamu wa JKCI wanavyotoa huduma bora kwa wagonjwa wanaowahudumia”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema wao kama taasisi wataendelea kuimarisha teknolojia ya matibabu ili waweze kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa maeneo ambayo ni vigumu kwa wananchi kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu alisema kutokana na uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba na rasiimali watu uliofanyika katika taasisi hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kuleta wagonjwa kutoka nchi mbalimbali kuja kupata matibabu hapa nchini.
Comments
Post a Comment