Viongozi washukuru kwa kupata huduma ya matibabu ya moyo katika kikao kazi cha Msajili wa Hazina


Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka akimkabidhi Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Izina cheti cha shukrani ya kudhamini kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa taasisi za umma kwa kutoa huduma za upimaji, ushauri na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa washiriki wa mkutano huo uliomalizika hivi karibuni jijini Arusha.

Afisa Muuguzi wa Hospitali ya AICC Loveness Swai akimpima shinikizo la damu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Maji Mbeya Neema Mwangwala wakati wa zoezi la upimaji afya ya moyo lililofanyika kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma walioshiriki kikao kazi cha siku tatu kilichomalizika hivi karibuni jijini Arusha.

Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hamisi Msangi akimchukuwa vipimo vya damu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Tabora Anthony Mayunga kwaajili ya kumpima magonjwa mbalimbali wakati wa zoezi la upimaji afya ya moyo lililofanyika kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa taasisi za umma walioshiriki kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Arusha.

Daktari wa Hospitali ya AICC Innocent Kessy akimuonesha Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Ofisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA) Baraka Katemba jinsi moyo unavyofanya kazi wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za upimaji, ushauri na matibabu ya magonjwa ya moyo iliyokuwa inatolewa kwa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa taasisi za umma walioshiriki kikao kazi cha siku tatu kilichaandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Arusha.


Mtoa Huduma kwa Wateja wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Grace Allan akimuonesha vipeperushi vinavyoelezea huduma zinazotolewa na taasisi hiyo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ardhi Mhe. Balozi Salome Sijaona wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za upimaji, ushauri na matibabu ya magonjwa ya moyo iliyokuwa inatolewa kwa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa taasisi za umma walioshiriki kikao kazi cha siku tatu kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Arusha.


Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Izina akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa Taasisi hiyo na wenzao wa hospitali ya AICC Arusha mara baada ya kumaliza kutoa huduma za ushauri, upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wenyeviti na watendaji wakuu wa taasisi za umma walioshiriki kikao kazi kilichoandaliwa na ofisi ya Msajili wa Hazina kilichomalizika hivi karibuni jijini Arusha.

********************************************************************************************************************************************************************************************************************

Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma nchini wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za ushauri, upimaji na matibabu ya moyo kwenye kikao kazi kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Huduma hiyo ya uchunguzi iliyofanyika hivi karibuni ilitolewa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya AICC ambapo huduma zilizotolewa ni kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu, vipimo vya maabara, kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa moyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi viongozi hao walisema wengi wao hawana muda wa kupima afya zao hii ni kutokana na majukumu ya kazi waliyokuwa nayo lakini kutolewa kwa huduma hiyo katika kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kumewasaidia kupata muda wa kupima afya zao.

“Kutokana na majukumu ya kazi kuwa mengi sisi viongozi huwa tunakosa muda wa kupima afya zetu na wengi wetu tunatumia dawa pale tunapojisikia vibaya, lakini katika kikao kazi hiki  tumeletewa huduma hii muhimu ya kupima afya zetu, nimeona nami nije kupima afya yangu ili nijue nikoje”.

“Ninaishauri JKCI iwe na programu ya kupima afya za moyo za wafanyakazi maofisini hata kama kuna gharama za upimaji wazijulishe taasisi husika ili zigharamie, kwa kufanya hivyo wafanyakazi wengi watafikiwa na huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo”, alisema Stanley Mwonzya Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Tumbaku Tanzania.

“Tulipofika hapa tulitangaziwa kuna huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo mwenye nafasi anaweza kwenda kupima, nilifurahi kupata nafasi hii kwani kupata huduma ya upimaji wa moyo siyo jambo rahisi. Nimeonana na wataalamu na kupima vipimo vya moyo na figo namshukuru Mungu majibu yako vizuri, shida niliyonayo ni uzito mkubwa nimepewa ushauri wa kuzingatia lishe bora na kufanya mazoezi nitaenda kutekeleza ushauri niliopewa na daktari”, alishukuru Edna Mwaigomole Mwenyekiti wa Bodi ya Mamkala ya Maji Mbeya.

Allen Marwa  ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Kahama alishukuru kwa huduma aliyoipata ya ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo amepewa elimu nzuri ya lishe ambayo imemsaidia kujua  aina gani ya vyakula ale ikiwemo mbogamboga na matunda pamoja na kufanya mazoezi.

 “Ninawashauri wenzangu mahali popote pale watakapokuwa wanapopata nafasi ya kupima afya zao wapime na kama watakutwa na matatizo watapata matibabu mapema zaidi kuliko kusubiri tatizo limekuwa kubwa”, alisema Marwa.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dickson Minja alisema kwa kushirikiana na hospitali ya AICC wametoa huduma za kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa viongozi na wenye shida wamewapa rufaa ya kwenda JKCI kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi.

 “Mwitikio umekuwa ni mkubwa viongozi wengi wamekuja kupima afya zao na baadhi tumewapa rufaa kwaajili ya uchunguzi zaidi, ninatoa wito kwa  washiriki  wa mikutano mbalimbali pale kutakapokuwa na nafasi ya kupima  afya wajitokeze kwa wingi na kupima afya”, alisema Dkt. Minja.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya AICC Arusha Dkt. Ezekiel Moirana alisema katika mikutano mbalimbali itakayofanyika jijini Arusha wataendelea kushirikiana na JKCI kutoa huduma za uchunguzi, ushauri na matibabu ya magonjwa ya moyo kwani katika ukumbi wa AICC wanapokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi wanaohitaji huduma hiyo.

“Zoezi hili litakuwa endelevu kwani licha ya washiriki wa mkutano kupata huduma ya upimaji wa moyo ambayo tunaitoa bila malipo yoyote yale lakini pia wataalamu wetu wanajengewa uwezo na wenzao wa JKCI wa jinsi ya kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo kwani upimaji huu tunaufanya kwa pamoja”, alisema Dkt. Moirana.


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024