Watoto 300 wafanyiwa upasuaji wa moyo kambi ya matibabu ya JKCI na Saudi Arabia

Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe. Yahaya Ahmed Okeshi akizungumza na Rukia Ramadhani ambaye ni mama wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka  Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu cha nchini Saud Arabia wakati wa kufunga kambi hiyo leo jijini Dar es Salaam. Jumla ya watoto 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi hiyo.

Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe.Yahaya Ahmed Okeshi akimpatia zawadi mama wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo Ester Benezed wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kw akushirikiana na wenzao wa Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu cha nchini Saudi Arabia. Jumla ya watoto 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi hiyo. 

Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe. Yahaya Ahmed Okeshi akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.  Peter Kisenge alipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya  kufunga kambi maalumu ya upasuaji wa moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia. Jumla ya watoto 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi hiyo.

Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe. Yahaya Ahmed Okeshi akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa afya wa JKCI na wenzao kutoka Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia alipotembelea JKCI leo kwaajili ya kufunga kambi maalumu ya matibabu ya siku 10 iliyokuwa ikifanywa na wataalamu hao. Jumla ya watoto 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo.

Baadhi ya wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia wakisikiliza wakati wa kufunga kambi maalumu ya upasuaji wa moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu hao. Jumla ya watoto 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo. 

Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe. Yahaya Ahmed Okeshi akimpatia zawadi kwa kazi nzuri aliyofanya Daktari bingwa wa upasuji wa moyo kwa watoto kutoka Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia Hani Mufti wakati balozi huyo alipotembelea kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto iliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo  jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Abdalah Kilima akimpatia zawadi kwa kazi nzuri aliyofanya Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia Omar Almohizy wakati wa kufunga kambi maalumu ya upasuji wa moyo kwa watoto leo jijini Dar es Salaam.

Picha na Stella Gama - JKCI

***************************************************************************************************************

Na Gilbert Mmbaga -JKCI

Watoto 300 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji na wataalamu wa Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia.

Upasuaji huo umefanyika kwa awamu tisa tangu mwaka 2019 ambapo awamu hii watoto 30 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kati ya watoto 50 waliofanyiwa uchunguzi katika kambi maalumu ya siku 10 iliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Akizungumza wakati wa kufunga kambi hiyo leo jijini Dar es Salaam Balozi wa Saudi Arabaia nchini Tanzania Mhe. Yahya Bin Ahmed Okeish alisema huduma za upasuaji wa moyo zinazofanyika kwa watoto zimedhamiria kuwarejeshea uhai watoto ambao wanasumbuliwa na magonjwa hayo.

Mhe. Yahya aliwapongeza wataalamu ambao wamekuwa wakichukua muda wao kutoka nchini Saudi Arabia kuja Tanzania kwaajili ya kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto na kuwataka kuendelea na moyo huo wakujitoa.

“Niwapongeze wataalamu wa Afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na wale wa kituo cha misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman cha nchini Saudi Arabia kwa kujitolea kurudisha tabasamu kwa watoto hawa”, alisema Mhe. Yahya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Wizara ya Mambo ya nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Abdalah Kilima alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaishukuru Serikali ya Saudi Arabia kupitia Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman kwa kuwaruhusu wataalamu wake kutoa huduma kwa watoto wa Tanzania.

Balozi Kilima alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Saudi Arabia kuhakikisha huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto zinaendelea kutolewa hasa katika familia ambazo haziwezi kumudu gharama za matibabu.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo Dkt. Tatizo Waane aliseme Kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman kimeweza kuchangia vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.5 tangu waanze kushirikiana na JKCI ambapo awamu hii wamechangia shilingi milioni 700.

Dkt. Waane alisema kambi ya matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu kutoka kituo cha Misaada ya Kibinadamu cha Mfalme Salman imekuwa ikitoa huduma kwa watoto wengi kwa kipindi cha muda mfupi hivyo kupunguza idadi ya watoto wanaosubiria upasuaji wa moyo.

Kwa niaba ya wazazi wa watoto waliofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo Ester Benazedi alitoa shukrani kwa wataalamu waliotoa huduma ya upasuaji kwa watoto 30 akiwemo mtoto wake aliyekuwa na tundu kwenye moyo pamoja na mishipa yake ya damu kuwa myembamba.

Ester alisema mtoto wake aliteseka kwa muda mrefu ila baada ya kufanyiwa upasuaji anaendelea vizuri na sasa anaweza kucheza na wenzake.

“Nawashukuru sana wataalamu hawa wa JKCI na wenzao kutoka Saudi Arabia kwa kufanikisha matibabu ya mtoto wangu ambaye sasa anaendelea vizuri Mungu awabariki”, alisema Ester.

 

 


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari