JKCI na Hospitali ya Medanta ya India kushirikiana matibabu ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpa tuzo ya kutambua mchango wake kutokana na huduma aliyoitoa ya kubadilishana ujuzi kwa wataalamu wa taasisi hiyo daktari bingwa wa moyo kutoka Hospitali ya Medanta iliyopo nchini India Preveen Chandra leo wakati wa kumuaga baada ya kutembelea JKCI na kufanya upasuaji wa tundu dogo na wataalamu wa JKCI.
Daktari bingwa wa moyo kutoka Hospitali ya Medanta iliyopo nchini India Preveen Chandra akizungumza na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) baada ya kushirikiana nao kufanya upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa watano wanaotibiwa na Taasisi hiyo.
Na: JKCI
********************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na
Hospitali ya Medanta iliyopo nchini India kubadilishana ujuzi katika fani
mbalimbali za kutoa huduma za matibabu ya moyo.
Ushirikiano huo umeanza kwa mara ya kwanza jana baada ya
daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Medanta kufika JKCI na
kuanza kutoa huduma za upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa wanaotibiwa katika
Taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema ujio wa daktari huyo umedhamiria kuwajengea
uwezo wataalamu wa JKCI na kushirikiana kwa pamoja kubadilishana ujuzi kwa
kuwafanyia upasuaji wa tundu dogo wagonjwa.
“Dkt. Chandra amefika jana na kushirikiana nasi kutoa huduma
za upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa wawili na leo ataendelea nasi kuwafanyia
upasuaji wa tundu dogo wagonjwa wengine watatu”, alisema Dkt. Waane
Dkt. Waane alisema Medanta ni moja ya Hospitali kubwa
zinazotoa matibabu ya moyo kwa utaalamu mkubwa na sasa imeanza kushirikiana na
JKCI katika kutoa huduma mbalimbali bingwa bobezi za moyo katika upasuaji wa
moyo pamoja na kupokea wataalamu wa JKCI wanaopenda kuongeza ujuzi katika fani
mbalimbali za matibabu ya moyo.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka
Hospitali ya Medanta iliyopo nchini India Preveen Chandra alisema amekuwa akifanya
upasuaji wa tundu dogo kwa utaalamu wa juu hivyo akaona ni wakati sasa kukutana
na wataalamu wenzake kuona namna wanavyofanya upasuaji huo na kubadilishana
ujuzi.
“Wagonjwa tunaowatibu India wanatoka nchi mbalimbali duniani
ikiwemo Afrika, wagonjwa hawa tumekuwa tukiwatibu kwa kutumia utaalamu mpya
kila tunapopata ujuzi mpya kama vile upasuaji wa Tavi wa kubadilisha valvu ya
mshipa mkubwa wa damu bila ya kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve
Implantation procedure – TAVI)”, alisema Dkt. Chandra
Dkt. Chandra alisema baada ya kufanya upasuaji na wataalamu
wa JKCI ameona ni Taasisi inayokuwa kwa kasi kutokana na uwekezaji wa vifaa
tiba vya kisasa vinavyotumika kutoa huduma za upasuaji wa moyo.
“Naamini baada ya miaka 10 ijayo taasisi hii itakuwa inafanya
aina zote za upasuaji wa moyo zinazofanyika duniani, ushirikiano wetu na
taasisi hii utaendelea kuhakikisha kila hatua inayopigwa duniani katika kutoa
huduma hizi na hapa hatua hiyo inafanyika”, alisema Dkt. Chandra
Comments
Post a Comment