Kambi Maalum ya Upimaji na Matibabu ya Moyo Yawafikia watu 302 Arusha
Mkurugenzi wa Arusha
Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwa sasa inasimamiwa na Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akipokea cheti cha shukrani kutoka kwa
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watu wazima na Mshauri wa Upasuaji wa moyo
kupitia tundu dogo kutoka National Heart
Institute (NHI) nchini Misri Prof. Ghada Kazamel baada ya kumalizika kwa kambi
maalumu ya siku mbili ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa watoto na watu
wazima iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali ya ALMC na wataalamu wa JKCI, ALMC, Heart to Heart
Association for Sustainable Development na
Egyptian African Heart Association (EAHA).
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Goup Eva Wakuganda akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) mtoto wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanywa na wataalamu wa JKCI, ALMC na Heart to Heart Association for Sustainable Development na Egyptian African Heart Association (EAHA) katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) jijini Arusha.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watu wazima na Mshauri wa upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo kutoka shirika la National Heart Institute (NHI) la nchini Misri Prof. Ghada Kazamel akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) mkazi wa Arusha wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyokuwa ikifanyika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).
Watu 302 wamefanyiwa uchunguzi wa
magonjwa ya moyo katika kambi maalumu ya siku mbili iliyofanywa na wataalamu wa Hospitali ya Arusha Lutheran
Medical Centre ambayo kwa sasa inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) kwa kushirikiana na Heart to Heart Association for Sustainable
Development na Egyptian African Heart Association (EAHA) za nchini Misri.
Akizungumza wakati wa kambi hiyo Daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Dkt. Eva Wakuganda alisema kati ya wagonjwa hao watoto 18
waligundulika kuwa na magonjwa mbalimbali ya moyo, huku watu wazima 235 wakiwemo
wanawake 112 na wanaume 121 miongoni mwao wamegundulika kuwa na shinikizo la
juu la damu, moyo kutanuka, hitilafu za umeme wa moyo na kuziba kwa mishipa ya
damu ya moyo.
Dkt. Eva alisema kuwa lengo la kambi
hiyo ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kubaini mapema
wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.
“Tumewapa wagonjwa rufaa kwa
matibabu zaidi baadhi wanahitaji matibabu ya haraka kwa njia ya tundu dogo
ikiwemo kuwekewa betri ya moyo, wengine wanahitaji kufanyiwa matibabu ya kufungua
mishipa ya damu ya moyo na wengine upasuaji wa moyo”. alisema Dkt. Eva.
Dkt. Eva alieleza kuwa idadi kubwa
ya watoto waliofanyiwa uchunguzi walikuwa ni wagonjwa wapya waliogundulika kwa
mara ya kwanza wakiwemo wenye matundu kwenye moyo na magonjwa ya moyo
yanayojitokeza baada ya kuzaliwa.
“Baadhi ya watoto tayari walikuwa na
matatizo na wakaona fursa hii waje kupimwa tena na madaktari na kuendelea na
mpango wa matibabu lakini pia tulikuwa na kesi nyingi mpya ikiwemo matundu ya
moyo na magonjwa ya moyo yanayopatikana baada ya kuzaliwa”, alieleza Dkt. Eva.
Kwa upande wa Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Moyo kwa watu wazima na
Mshauri wa upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo kutoka National Heart Institute (NHI) ya
nchini Misri Prof. Ghada Kazamel alisema wingi wa wagonjwa unaonesha hitaji la
kuimarisha zaidi huduma za afya ya moyo mkaoni Arusha.
“Nilishangazwa nilipofika Arusha
kuona idadi kubwa ya wagonjwa, katika kambi hii tumewahudumia takribani
wagonjwa 302, wengi wao wanahitaji kuwekewa betri za moyo na kufanyiwa matibabu
ya uingiliaji wa mishipa ya moyo”. alisema Prof. Ghada.
Alibainisha kuwa kuna umuhimu wa
Hospitali hiyo ya Ausha Lutheran Medical Centre kuwa na mtambo wa Cathlab ili
kuwahudumia wananchi wa mkoa huo.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya
Moyo kwa Watoto kutoka Cairo University Children Hospital, Prof. Amal El-Sisi
alisema wamewahudumia watoto kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 18 wenye matatizo
mbalimbali ya moyo ikiwemo ya kuzaliwa nayo.
“Tumewaona watoto wengi kuanzia
wenye umri wa mwezi mmoja hadi miaka 18 baadhi yao wana matatizo ya moyo ya
kuzaliwa nayo, na baadhi watahitaji kufanyiwa matibabu kwa njia ya catheter au
upasuaji na matibabu hayo yanaokoa maisha”. alisema Prof. Amal El-Sisi.
Kwa upande wao wananchi wa mkoa wa
Arusha waliofika kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi hiyo maalumu
ya siku mbili wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo na kubainisha kuwa imewasaidia
kupata uchunguzi wa mapema.
“Kwa kweli kambi hii imenisaidia sana
kwa sababu imenipunguzia gharama za nauli kwenda Dar es Salaam na kurudi pamoja
na gharama za malazi na maisha ya kule”. alisema Amon Emmanuel Lesilwa mkazi wa
Arusha.
“Baada ya kipimo wamegundua tatizo
lingine ambalo sikuwa nalijua sasa nitachukua uamuzi wa matibabu zaidi kwa kweli
amenisaidia sana”, alisma Christina Kagemuro Rugakingira Mkazi wa Arusha.
Kambi hiyo ni sehemu ya mkakati wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wa kusogeza huduma za kibingwa karibu na
wananchi kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuongeza upatikanaji wa huduma
za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo nchini hasa karibu na wananchi.





Comments
Post a Comment