JKCI yahimiza familia kulinda watoto dhidi ya mazingira hatari


Afisa Ustawi wa Makao ya Watoto Kurasini, Andrew Haule akiwakaribisha wanawake wa Chama cha Wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walipotembelea makao hayo jana jijini Dar es Salaam na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali wenye thamani ya shilingi milioni 3.55 ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theresia Marombe, akikabidhi zawadi kwa watoto wanaolelewa katika Makao ya Watoto Kurasini jijini Dar es Salaam wakati wanawake wa taasisi hiyo walipotembelea makao hayo na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 3.55 katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
*********************************************************************************************************************************************************************************************
Familia zimetakiwa kuishi kwa amani, upendo na mshikamano ili kuwalinda watoto dhidi ya changamoto za malezi zinazoweza kuwafanya baadhi yao kukimbilia kuishi katika mazingira hatarishi ikiwemo mitaani.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sr. Theresia
Marombe wakati wanawake wa taasisi hiyo walipotembelea Makao ya Watoto Kurasini jijini Dar es
Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Sr. Theresia ambaye pia ni Afisa Muuguzi katika taasisi hiyo alisema
migogoro ya kifamilia na hali ngumu za maisha ni miongoni mwa sababu
zinazowafanya baadhi ya watoto kukosa malezi bora na hatimaye kuishi katika
mazingira hatarishi.
Alisema ni muhimu kwa wazazi na walezi hususan wanawake ambao ni nguzo
ya familia kuhakikisha wanatunza na kuimarisha misingi ya familia ili kupunguza
tatizo la watoto wanaoishi mitaani.
“Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani, wanawake wa JKCI tumetoa
msaada wa vifaa mbalimbali katika makao haya ikiwemo jiko la kuoka mikate lenye thamani ya shilingi milioni 2.2 lenye
uwezo wa kuoka mikate 60 kwa wakati mmoja, mchele
na sukari vitu vyote hivi thamani yake ni shilingi milioni 3.55 lengo likiwa ni kusaidia kuboresha huduma kwa watoto wanaoishi katika
makao haya”, alisema Sr. Theresia.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Makao ya Watoto Kurasini, Farida Kabezya aliishukuru JKCI kwa
msaada huo na kuiomba jamii kujenga utamaduni wa kuwatembelea na kuwasaidia
watoto wanaoishi katika makao hayo.
Alisema makao hayo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu
wa uzio pamoja na baadhi ya vifaa tiba kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
“Tunaishukuru sana JKCI kwa kutukumbuka na kutuletea msaada huu muhimu.
Tunawaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kwani watoto wengi waliopo hapa
wanasoma na wanahitaji kutiwa moyo ili kufikia ndoto zao”, alisema Farida.
Nao wanachama wa Chama cha Wanawake wa JKCI walisema wamefarijika
kushiriki kuadhimisha Siku ya Wanawake kwa kuwasaidia watoto hao na kuwaletea
tabasamu.
“Tunafanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa wakiwemo watoto, hivyo
tunafahamu mahitaji yao ya msingi. Tumeona ni vyema katika siku hii muhimu
kuwatembelea na kuwafariji watoto hawa”, alisema Afisa Muuguzi wa JKCI, Magerth
Mbaruku.
“Watoto hawa wana ndoto kubwa za kuwa
viongozi, madaktari, walimu na wataalamu mbalimbali wa kesho wa taifa letu. Ni
wajibu wa jamii kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu
kama huduma za afya, elimu bora na lishe, ili kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto
zao na kuwa tegemeo la baadaye la nchi”, alisema Mkurugenzi
wa Fedha na Mipango wa JKCI, CPA. Agnes Kuhenga.
Makao ya Watoto Kurasini yana jumla ya watoto 94, wakiwemo wavulana 60 na wasichana 34. Makao hayo yanaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Sura ya 13 Marejeo ya mwaka 2019, pamoja na kanuni zake ikiwemo Kanuni ya Makao ya Watoto ya Mwaka 2012 na kanuni za ulinzi na usalama wa mtoto.



Comments
Post a Comment