JKCI yawahamasisha Wananchi kujitokeza kupima Afya Kariakoo

Wananchi wakisubiri kupata huduma ya matibabu ya magonjwa mbalimbali wakati wa kambi maalum ya upimaji wa afya inayofanyika bila malipo katika Tawi la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo Soko Kuu la Kariakoo ghorofa la tano jiji Dar es Salaam.
Daktari wa Afya ya Kinywa na Meno wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group, Joachim Mvungi akitoa elimu ya jinsi ya kupiga mswaki kwa wananchi waliofika katika kambi maalum ya upimaji wa afya bila malipo inayofanyika katika Kliniki ya JKCI Soko Kuu la Kariakoo ghorofa la tano jiji Dar es Salaam.
.jpeg)
Daktari bingwa wa Macho wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group, Festus Mhagama akimfanyia uchunguzi wa macho Edward Mwakilasa mkazi wa Gongolamboto wakati wa kambi maalum ya upimaji wa afya inayofanyika katika Kliniki ya JKCI Soko Kuu la Kariakoo ghorofa la tano jiji Dar es Salaam.
*************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) imewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya
zao katika kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali inayofanyika
katika tawi lake lililopo Soko Kuu la Kariakoo, ghorofa ya tano jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza na
waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa
JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema lengo la kambi hiyo ni kusogeza huduma za
uchunguzi na matibabu ya kibingwa karibu na wananchi hususan wafanyabiashara wa Kariakoo na wakazi
wa maeneo ya jirani.
Dkt. Kisenge ambaye
pia ni daktari bingwa wa moyo alisema kambi hiyo inalenga kuwafikia wananchi
wengi zaidi na kuwahamasisha kupima afya zao mara kwa mara hasa vijana ambao
kwa sasa wako katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo kutokana na mtindo
usiofaa wa maisha ikiwemo matumizi ya pombe, sigara na lishe duni”, alisema
Dkt. Kisenge.
“Ninawaomba
wananchi mbadili mtindo wa maisha kwa kuacha uvutaji wa sigara, kupunguza
matumizi ya pombe kupita kiasi, kula lishe bora na kufanya mazoezi mara kwa
mara ili kuepuka magonjwa hatari kama kiharusi na kisukari”, alisema Dkt.
Kisenge.
Alisisitiza umuhimu
wa wananchi kufahamu namba zao za afya ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha
sukari, uzito, urefu na kiwango cha mafuta mwilini ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza
yanayoongezeka kwa kasi.
“Tunaposema ‘Jua Namba Zako’ tunamaanisha kila
mmoja ajue uzito wake, urefu, sukari, mafuta mwilini na mapigo ya moyo. Ufahamu
huu ni kinga muhimu dhidi ya magonjwa yanayosababisha vifo vya ghafla”,
alisisitiza Dkt. Kisenge.
Baadhi ya wananchi
waliojitokeza kupima afya zao walieleza kuridhishwa na huduma hiyo na kuitaja
kuwa msaada mkubwa kwa jamii.
Hamisi Rashidi
mkazi wa Mbagala Zakheem, alisema alipogundua uzito wake hauendani na urefu
wake alipatiwa ushauri wa kufanya mazoezi ili kuboresha afya yake.
“Naishukuru JKCI
kwa huduma hii. Waendelee kutoa elimu ili wananchi wapate taarifa sahihi kutoka
kwa wataalamu badala ya kuamini uvumi kutoka kwa watu ambao siyo wataalamu wa
Afya”, alisema Rashidi.
“Kambi hii
imenisaidia kuelewa zaidi dalili za
magonjwa ya moyo na umuhimu wa kupima afya mara kwa mara. Huduma hii ni muhimu
sana kwa sababu iko karibu na maeneo yetu ya kazi, imenirahisishia kupima na kupata ushauri wa kitaalamu kwa
wakati”, alisema Amina Lugiso mfanyabiashara
wa Kariakoo
“Huduma hii imewasaidia wananchi wengi ambao mara nyingi
hushindwa kupima afya kutokana na gharama.Tunashukuru kwa huduma hii ya bure.
Inawasaidia wengi wetu ambao hatukuwa na uwezo wa kugharamia vipimo”, alisema Mohamed Issa mkazi wa Ilala.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupima afya ya moyo pamoja na watoto
wangu ambao nimekuja nao, huduma ni nzuri na ya kuridhisha. Nawahamasisha
wananchi wengine wajitokeze kupima afya zao”, alisema Zelda Joas mkazi wa Temeke.
JKCI imeendelea na jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia kampeni mbalimbali za upimaji wa afya zikiwa na lengo la kuwahamasisha watu kufahamu namba zao za afya kama njia ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, hususan magonjwa ya moyo.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Comments
Post a Comment