Wafanyakazi 121 wa TANAPA wapimwa Afya ya Moyo Arusha

Afisa Masoko wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Mndasha  akimueleza mfanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) huduma zinazotolewa na taasisi hiyo wakati wa zoezi la upimaji afya ya moyo kwa wafanyakazi wa TANAPA ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Aim Sports mkoani Arusha.

Daktari wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Advotus Kimomogoro akimsikiliza mkazi wa Arusha aliyefika katika viwanja vya Aim Sports kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji wa afya ya moyo iliyokuwa inatolewa kwa wafanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.


Matroni wa Hospitali ya  Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Florah Kasembe akimkabidhi zawadi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Mathew Mombo wakati wa zoezi la upimaji afya ya moyo kwa wafanyakazi wa TANAPA ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Aim Sports mkoani Arusha.


Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nadia Zuberi akimpima shinikizo la damu Mkaguzi wa  Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Arusha Janeth Joseph wakati wa zoezi la upimaji afya ya moyo kwa wafanyakazi wa TANAPA ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Aim Sports mkoani Arusha.

 Afisa Muuguzi Msaidizi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Upendo Mwanda akimpima uzito mfanyakazi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wakati wa zoezi la upimaji afya ya moyo kwa wafanyakazi wa TANAPA ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Aim Sports mkoani Arusha.

*********************************************************************************************************************************************************************************************************************

Jumla ya wafanyakazi 121 wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika hivi karibuni mkoani Arusha.

Huduma hizo zilitolewa na wataalamu kutoka Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo Matroni wa ALMC, Afisa Muuguzi Mwandamizi Sr. Florah Kasembe alisema kati ya waliopimwa wanawake walikuwa 75 na wanaume 46. Aliongeza kuwa watu 17 walibainika kuwa na changamoto za afya ya moyo zinazohitaji uchunguzi zaidi na hivyo kupewa rufaa kwa ajili ya matibabu ya kina katika hospitali hiyo.

Alifafanua kuwa baadhi ya waliopatiwa rufaa walikutwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kiwango kikubwa cha sukari mwilini pamoja na hitilafu za mfumo wa umeme wa moyo. Kutokana na hali hiyo aliwahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kugundua mapema changamoto za kiafya.

Aidha, Sr. Florah alisema taasisi hiyo inaendesha kampeni maalum ya uhamasishaji ijulikanayo kama “Ijue Namba Yako”, inayolenga kuwahamasisha wananchi kufahamu viashiria muhimu vya afya ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha sukari, mafuta mwilini, uzito na urefu.

“Kufahamu namba zako za afya ni hatua muhimu ya kujikinga na magonjwa ya moyo. Endapo utagundua changamoto yoyote mapema itakuwa rahisi kupata matibabu stahiki kwa wakati”,  alisema Sr. Florah.

Aliongeza kuwa katika kuboresha upatikanaji wa huduma, JKCI imepanua wigo wake kwa kufungua matawi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kariakoo, Kawe, Oysterbay, Hospitali ya Dar Group, Chato pamoja na ALMC na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupima afya zao mara kwa mara.

Sr. Florah alibainisha kuwa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inatoa huduma mbalimbali za afya kwa kiwango cha ubora wa juu, zikiwemo matibabu ya moyo, afya ya kinywa na meno, pamoja na huduma za dharura, kliniki ya uzazi na magonjwa ya wanawake, kliniki ya watoto, matibabu ya magonjwa ya kuambukiza, pamoja na huduma za macho, pua, masikio na koo na hivyo kukidhi mahitaji mbalimbali ya wagonjwa.

Aliongeza kuwa ALMC pia inatoa huduma za matibabu ya ngozi, saikolojia, mfumo wa mkojo, magonjwa ya tumbo na ini, figo na magonjwa ya ndani, pamoja na huduma za upasuaji mkubwa na mdogo na matibabu ya mifupa, huduma za kliniki ya baba, mama na mtoto (RCH), upimaji wa VVU na ushauri nasaha (VCT), fiziotherapia (mazoezi tiba) na wodi maalumu za VIP, hatua inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa makundi yote ya jamii.

 “Tuligundua kuwa wananchi wengi kutoka mikoa ya Arusha, Manyara  na Kilimanjaro, Mwanza na Shinyanga walilazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kupata huduma za moyo jambo ambalo lilikuwa changamoto kwa wengi,” alieleza.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa TANAPA, Mathew Mombo alieleza kuridhishwa na huduma alizopata baada ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo.

“Nimepata fursa ya kupima vipimo mbalimbali ikiwemo presha, sukari na kipimo maalum cha moyo. Madaktari wamenithibitishia kuwa afya yangu iko vizuri. Nimevutiwa na weledi mkubwa wa wataalamu hawa”,  alisema Mombo.

Aliongeza kuwa huduma hizo zinaakisi kiwango cha juu cha utaalamu na maandalizi, hali inayowawezesha wananchi kupata uchunguzi sahihi na ushauri wa kitaalamu.

Naye Mkaguzi kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Arusha, Janeth Joseph alisema uchunguzi alioupata umemsaidia kutambua umuhimu wa kufanya mazoezi na kuzingatia afya yake.

“Nilidhani niko sawa kiafya, lakini vipimo vimenionesha umuhimu wa kuboresha mtindo wangu wa maisha. Nawashukuru JKCI kwa huduma bora waliyoitoa katika maadhimisho haya”, alisema.

Kwa upande wake mfanyakazi wa TANAPA Stella Emmanuel alisema ameridhishwa na huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo aliyoipata na kueleza kuwa imeongeza uelewa wake kuhusu afya ya moyo.

“Katika maadhimisho haya ya Siku ya Wanawake Duniani nimepata huduma muhimu sana ya uchunguzi wa afya ya moyo. Nimefurahi na kunufaika kwa kiasi kikubwa” , alisema.

Ushiriki wa ALMC katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wafanyakazi wa serikali na taasisi mbalimbali unaendelea kuwa daraja muhimu la kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na hivyo kuchangia kuboresha afya ya jamii kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi