Serikali yamuokoa Mama wa Kivule kwa matibabu ya moyo ya shilingi milioni 29 JKCI
.jpeg)
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Zaina Mlingo akimpima shinikizo la damu Mama Anna Mwansasu mkazi wa Kisamvule jijini Dar es Salaam ambaye amefanyiwa upasuaji mdogo wa kupandikiziwa kifaa cha CRT (Cardiac Resynchronization Therapy) ambacho kinausaidia moyo kupiga mapigo yake kwa mpangilio sahihi. Gharama ya matibabu hayo ni zaidi ya shilingi milioni 29 ambapo serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imelipia.
*****************************************************************************************************************************************************************************************************
Mkazi wa Kivule jijini Dar es Salaam Mama Anna Mwansasu, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumsaidia kugharamia matibabu ya kubadilishiwa kifaa cha CRT (Cardiac Resynchronization Therapy) ambacho kinausaidia moyo kupiga mapigo yake kwa mpangilio sahihi.
Mama Anna
alifanyiwa upasuaji mdogo wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na
kupandikizwa kifaa hicho ambapo gharama ya matibabu ni zaidi ya shilingi milioni
29 na kwa sasa anaendelea vizuri kiafya baada ya kupata matibabu hayo.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana akiwa wodini, Mama Anna alisema hali yake inaendelea
kuimarika baada ya kufanyiwa upasuaji wa kubadilishiwa kifaa hicho muhimu.
“Naishukuru sana
JKCI kwa huduma nzuri niliyoipata. Baada ya kufanyiwa upasuaji sina tatizo
lolote na nasubiri kumaliza dawa nilizoandikiwa ili niruhusiwe kurudi nyumbani”,
alisema Mama Anna.
Alieleza kuwa
alifika hospitalini hapo tarehe 6 Machi, akalazwa tarehe 7 na kufanyiwa
upasuaji tarehe 8. Awali madaktari walitarajia kubadilisha CRT peke yake lakini
baada ya uchunguzi wa kina ilibainika kuwa ilibidi kubadilisha CRT pamoja na
vifaa vyake vyote.
Mama Anna aliongeza
kuwa hakuwa na uwezo wa kugharamia matibabu hayo ya gharama kubwa lakini baada
ya taarifa yake kurushwa kupitia Azam
Media, Serikali iliamua kugharamia matibabu yote.
“Nilikuwa sina
uwezo wa kupata fedha za kubadilishiwa kifaa hiki lakini baada ya taarifa
kusikika kwenye vyombo vya habari, Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ilinisaidia kugharamia matibabu yote”, alisema Mama Anna.
Aidha Mama Anna
alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa
JKCI, Dkt. Peter Kisenge pamoja na timu nzima ya wataalamu wa taasisi
hiyo kwa huduma bora aliyopata.
“Kifaa hiki
kimenisaidia sana. Ninaamini nitaweza kufanya shughuli ndogo ndogo za maisha
yangu. Kwa kweli JKCI imenipa maisha mapya”, aliongeza.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema walimpokea
mgonjwa huyo baada ya kujitokeza kuomba msaada wa matibabu kutokana na tatizo
la moyo kushindwa kufanya kazi vizuri ambapo awali alishafanyiwa upasuaji wa
kuwekewa kifaa hicho miaka iliyopita.
Dkt. Kisenge
alifafanua kuwa matatizo ya umeme wa moyo na moyo kushindwa kufanya kazi vizuri
husababishwa na umri mkubwa, presha ya juu, kisukari, kuziba ghafla kwa mishipa
ya damu, pamoja na baadhi ya watu kuzaliwa na tatizo hilo.
Aliwashauri
wananchi kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa ya moyo kwa kufanya mazoezi
angalau mara mbili hadi tatu kwa wiki, kuepuka uvutaji wa sigara na matumizi ya
pombe kupita kiasi pamoja na kuzingatia ulaji wa lishe bora.
Dkt. Kisenge pia
aliwahimiza wagonjwa wote waliofanyiwa matibabu ya kuwekewa vifaa vya kuusaidia
moyo kufanya kazi vizuri (CRT, Pacemaker) kufika hospitalini hapo mara kwa mara
kwa ajili ya uchunguzi ili kufuatilia
maendeleo ya vifaa hivyo.
“Tunawashauri
wagonjwa hawa wafike hospitalini kwa uchunguzi angalau kila baada ya miezi sita
ili kufuatilia maendeleo ya kifaa na kuhakikisha kinafanya kazi vizuri”, alisema
Dkt. Kisenge.
Aidha Dkt. Kisenge aliishukuru
Serikali kwa kuanzisha mpango wa Bima
ya Afya kwa Wote huku akisema utasaidia wananchi wengi hasa wenye kipato
cha chini kupata matibabu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ya moyo ambayo mara
nyingi huwa na gharama kubwa.
Naye Daktari bingwa
wa Moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba wa JKCI, Yona Gandye aliyemuhudumia mgonjwa
huyo alisema Mama Anna aligundulika kuwa na tatizo la moyo kushindwa kufanya
kazi vizuri (heart failure)
takribani miaka saba iliyopita.
Alisema tatizo hilo
lilitokana na moyo kutanuka, hali iliyosababisha dalili za uchovu wa mara kwa
mara, kupumua kwa shida pamoja na kikohozi.
Baada ya kufanyiwa
uchunguzi zaidi, ilibainika kuwa kifaa cha awali cha CRT (Cardiac Resynchronization Therapy) alichokuwa amewekewa
kilikuwa kimepoteza nguvu hivyo kulihitajika kubadilishwa ili kuepusha kurejea
kwa tatizo hilo.
Dkt. Gandye alisema
kwa sasa mgonjwa huyo anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji wa
kubadilishiwa kifaa kipya cha CRT na anaendelea kupata uangalizi wa madaktari
wa JKCI hadi hali yake itakapotengamaa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Kifaa hiki cha CRT (Cardiac Resynchronization Therapy) kinatumia pacemaker maalum yenye nyaya nyingi (leads) zinazowekwa kwenye sehemu tofauti za moyo ili kurekebisha rhythm yake, kufanya moyo usukume damu vizuri, kupunguza dalili za uchovu, kizunguzungu na kupumua kwa shida na kumwezesha mgonjwa kufanya shughuli za kila siku kwa urahisi na kupata maisha bora zaidi.
Comments
Post a Comment