Ushirikiano na Jamii waongeza nguvu ya matibabu ya Moyo JKCI
Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akiwa katika picha ya pamoja na wadau kutoka Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Moyo Mission ya nchini Ujerumani pamoja na wafanyakazi wa JKCI wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ushirikiano wa kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani akizungumza na wadau wa afya hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ushirikiano wa utoaji huduma za matibabu ya moyo kwa watoto baina ya JKCI na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Moyo Mission ya nchini Ujerumani.
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Bernard Paul maarufu kama Ben Paul akizungumza kuhusu ushirikiano wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Moyo Mission ya nchini Ujerumani na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wa kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika hivi karibuni katika viwanja vya JKCI jijini Dar es Salaam.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela akizungumzia ushirikiano kati ya JKCI na Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Moyo Mission wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ushirikiano wa utoaji huduma za matibabu ya moyo kwa watoto iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
*************************************************************************************************************************************************************************************
Jamii na wadau mbalimbali wametakiwa kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuleta marafiki na washirika watakaosaidia taasisi hiyo kufikia malengo yake ya kutoa huduma bingwa na bobezi za matibabu ya moyo kwa watoto.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani wakati wa uzinduzi
wa kampeni ya ushirikiano kati ya JKCI na taasisi isiyo ya kiserikali ya Moyo Mission uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
Dkt. Naizihijwa ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
kwa watoto alisema ushirikiano huo unaoenda sambamba na ujio wa wataalamu wa
afya ya moyo kutoka Ujerumani unalenga kuongeza uwezo wa taasisi
hiyo katika kutoa huduma za kibingwa na kibobezi za moyo hususan katika
upasuaji wa moyo kwa watoto.
"Lengo kubwa la ushirikiano huu ni kubadilishana uzoefu na
kusaidia kufanya upasuaji kwa watoto wengi kwa muda mfupi. Tunatarajia
kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto kati ya 10 hadi 15 ndani ya siku tano", alisema Dkt.
Naizihijwa.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa
Upasuaji wa Moyo na Mishipa ya Damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex
Joseph aliipongeza
taasisi ya Moyo Mission kwa kuchagua kushirikiana na JKCI katika juhudi za
kuwasaidia watoto wenye matatizo ya moyo.
"Kupitia ushirikiano huu na madaktari kutoka Ujerumani,
tutahakikisha tunatoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa kutumia rasilimali
zilizopo ili watoto wapate matibabu bora", alisema
Dkt. Joseph.
Naye
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa
Moyo kutoka Ujerumani, Daniel Briemann aliishukuru JKCI kwa
kukubali kushirikiana nao katika kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.
"Tunafurahi kuwa
sehemu ya juhudi za kuwahudumia watoto wa Tanzania wenye matatizo mbalimbali ya
moyo. Lengo letu ni kuwafikia wagonjwa wengi zaidi na kuokoa maisha yao", alisema
Dkt. Briemann.
Kwa
upande wake msanii wa muziki wa kizazi kipya Bernard Paul maarufu kama Ben Pol ambaye pia ni rafiki wa
karibu wa JKCI na Moyo Mission aliwataka wadau mbalimbali kujitokeza kuunga
mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za matibabu ya moyo kwa
watoto.
"Kazi kubwa inayofanywa na Moyo Mission ni kutafuta wadau watakaoshirikiana na JKCI katika kutoa matibabu ya moyo na kuokoa maisha ya watoto wengi", alisema Ben Pol.





Comments
Post a Comment