Afya Kwanza: JKCI yawafikia Waumini wa KKKT Mbezi Beach kwa huduma za kibingwa
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Morisi Budotela akizungumza na muumini wa Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach Magrateh Misericordias mara baada ya kufanya vipimo vya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku moja iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kanisa hilo lililopo jijini Dar es Salaam.
Mtalaamu
wa vipimo vya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Yatimuni Mushi akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mwananchi
aliyefika katika kambi maalumu ya siku moja ya uchunguzi na matibabu ya moyo
iliyokuwa ikifanywa na Taasisi hiyo katika Kanisa la
Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach jijini Dar es
Salaam.
Afisa
Uuguzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Happiness Muragwa akimpima
shinikizo la damu mkazi wa Bunju B wakati wa kambi maalumu ya siku moja ya
uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Mbezi Beach jijini Dar es
Salaam.
Afisa
Masoko wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Agness Mndasha akimpatia
zawadi Mzee wa Kanisa na Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii wa Kanisa la
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Beach
Wintyapa Lionel wakati wa kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya
moyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kanisa hilo lililopo jijini Dar es
Salaam.
Picha na Khamis Mussa
********************************************************************************************
Jumla
ya Waumini 93 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa
Mbezi Beach wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo
katika jitihada za kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza
vifo vya ghafla vinavyosababishwa na kutofanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
Uchunguzi
huo ulifanyika kupitia kambi maalumu ya siku moja iliyoendeshwa na wataalamu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Mbezi Beach jijini
Dar es Salaam.
Kambi
hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki ni sehemu ya mkakati wa JKCI wa kuimarisha
kinga na kutoa elimu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza hususan magonjwa ya moyo,
shinikizo la juu la damu na kisukari.
Akizungumza
wakati wa kuhitimisha zoezi hilo Afisa Masoko wa JKCI, Agness Mndasha alisema
mwitikio wa waumini hao ulikuwa wa kuridhisha na unaonesha namna jamii
inavyoendelea kutambua umuhimu wa kuchunguza afya zao mapema.
Alieleza
kuwa jitihada hizo zinaungwa mkono na maboresho makubwa ya sekta ya afya
yanayofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
jambo linaloiwezesha JKCI kupanua wigo wa huduma za kibingwa na kuokoa maisha
ya Watanzania wengi zaidi.
“Ni
muhimu wananchi wakajenga utamaduni wa kujitokeza kupima afya zao pindi fursa za uchunguzi zinapotolewa. Kinga
ni bora kuliko tiba na magonjwa ya moyo pamoja na shinikizo la damu yameendelea
kuathiri jamii kwa kiwango kikubwa”, alisema Agness.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Huduma za Jamii na Mzee wa Kanisa wa Usharika huo
Winytyapa Malawa, aliishukuru JKCI kwa kusogeza huduma hizo kanisani hapo huku
akisema zimewapa fursa ya kupata uchunguzi bila gharama na elimu ya kujiepusha
na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo itakayowasaidia kubadili mtindo wa
maisha.
“Kutokana
na majukumu mengi ya kazi niliyokuwa nayo, mara nyingi nakosa muda wa kwenda
hospitali kupima afya yangu. Leo nimepata nafasi ya kujua hali yangu ya afya
bila ya kulipia gharama zozote zipo jambo lililonipa faraja kubwa”, alisema Malawa.
Naye
Katibu wa KKKT Usharika wa Mbezi Beach, Mhandisi Lilian Marry alisema elimu ya
lishe bora na uchunguzi wa mapema uliotolewa umeongeza uelewa miongoni mwa
waumini ambao wameahidi kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuchukua tahadhari
dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
“Hatua
hii ni muhimu kwetu kwani mbali na kuombea afya ya miili yetu leo tumejifunza
kulinda miili yetu kwa kuzingatia lishe bora na kuepuka kutumia vitu ambavyo
vinasababisha magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu”, alisema Lilian.
Bendriba
Lyanga muumini wa Kanisa hilo aliipongeza JKCI kwa kuwafikia wananchi moja kwa
moja huku akisema amekutana na madaktari bingwa wa moyo na kufanyiwa vipimo na
kupata ushauri kitu kilichomfungua macho na kumpa matumaini mapya.
Kambi
hiyo imeendelea kudhihirisha dhamira ya JKCI ya kuhakikisha huduma za kibingwa
za moyo zinawafikia wananchi popote walipo huku ikisisitiza umuhimu wa kinga,
elimu na uchunguzi wa mapema katika kulinda afya ya jamii.




Comments
Post a Comment