Kamati ya Bunge yapongeza uwekezaji wa Mhe. Rais Dkt. Samia JKCI, yasema waongeza nguvu ya matibabu ya Moyo nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akielezea huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI walipofanya ziara katika Taasisi hiyo leo kuona huduma zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Dkt. Johannes Lukumay akimjulia hali mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Naizihijwa Majani akiwaelezea wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI huduma zinazotolewa kwa watoto aliolazwa katika wodi ya wagonjwa watoto wanaohitaji uangalizi maalumu (PICU)wakati kamati hiyo ilipotembelea JKCI leo kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwaonesha moja ya chumba cha kulaza wagonjwa mashuhuri (VIP Ward) wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI walipofanya ziara katika Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona kuona huduma zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Dkt. Johannes Lukumay akizungumza na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mara baada ya kamati hiyo kumaliza ziara yake katika Taasisi hiyo leo jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi akielezea mafanikio ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI walipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Neema Mwandabila akichangia mada wakati wajumbe wa kamati hiyo walipofanya ziara katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kuona huduma zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Dkt. Johannes Lukumay akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi na wajumbe wa kamati hiyo mara baada ya kumaliza  ziara yao  katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo jijini Dar es Salaam.

Na JKCI
************************************************************************************************************

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imetambua uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya ikiwemo Taasisi ya Moyo ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kusema kuwa umeleta matokeo chanya katika kuboresha matibabu ya kibingwa ya moyo nchini.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Johannes Lembulung Lukumay wakati akitoa majumuisho ya ziara ya kamati hiyo walipotembelea  JKCI kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na uwekezaji uliofanywa na serikali katika taasisi hiyo.

Kamati hiyo pia  imeipongeza JKCI kwa juhudi zake za kuboresha huduma za moyo kwa watu wazima na watoto pamoja na kufungua matawi ya matibabu ya moyo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwafikia wananchi karibu zaidi.

“Uwekezaji uliofanywa hapa JKCI na Mhe. Rais Dkt. Samia ni mkubwa na wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 13, ukijumuisha jengo jipya la watoto na vifaa tiba vya kisasa ikiwemo maabara na mitambo kama Cathlab. Huu ni uwekezaji unaoonyesha dhahiri  na umuhimu wa Serikali katika kuimarisha sekta ya afya”, alisema Mhe. Dkt. Lukumay.

Mwenyekiti huyo wa kamati aliongeza kuwa JKCI ni miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri nchini na barani Afrika katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo akitaja pia juhudi za uongozi wa taasisi hiyo katika kupanua huduma zake ikiwemo kufungua vituo vya matibabu ya moyo katika hospitali mbalimbali nchini kama vile Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi alisema uwekezaji uliopo JKCI unasaidia kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo na umeonesha  dhamira ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata matibabu ya moyo ya kisasa na bora.

Aliongeza kuwa mwaka jana jumla ya watoto 350 wamefanyiwa upasuaji wa moyo bila gharama yoyote  upasuaji ambao umegharamiwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali huduma hizo zimeokoa maisha ya watoto wengi na kuonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau katika kuboresha huduma za afya.

Mhe. Dkt. Samizi aliwapongeza watendaji wa JKCI kwa juhudi zao za kuboresha huduma za moyo kwa watoto na watu wazima huku akiwahimiza watanzania hasa wale wenye changamoto za kiafya kwa watoto kuwapeleka  mapema katika taasisi hiyo ili waweze kupata matibabu mapema ikiwa ni njia ya kuhakikisha maisha yao yanaokolewa.

“Ninawapongeza JKCI kwa kutumia teknolojia za kisasa katika tiba, ikiwemo maabara na mitambo ya upasuaji, iliyoongeza muda wa kutoa matokeo na kuhakikisha matokeo hayo ni ya uhakika. Tunaona wazi kuwa JKCI imekuwa kitovu cha matibabu ya moyo nchini kwa kutoa huduma kwa wananchi bila kulazimika kwenda kutibiwa nje ya nchi”,  alisema Dkt. Samizi.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI,  Dkt. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo imeendelea kupanua huduma zake za matibabu ya moyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi ndani na nje ya Tanzania.

Dkt. Kisenge alisema JKCI kwa sasa inatoa huduma mbalimbali za kibingwa na bobezi za matibabu ya moyo ikiwemo upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima, upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo, matibabu ya mishipa ya damu ya moyo, matibabu ya umeme wa moyo, kupandikiza vifaa visaidizi vya moyo pamoja na huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia vifaa vya kisasa vya picha za moyo.

“Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za matibabu ya moyo hapa hapa nchini bila kulazimika kwenda nje ya nchi. Tumekuwa tukipanua huduma zetu kwa kufungua matawi katika maeneo mbalimbali pamoja na kuimarisha miundombinu na teknolojia ya kisasa ili kuongeza ubora wa huduma”,  alisema Dkt. Kisenge.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo pia inaendelea kuwekeza katika mafunzo ya wataalamu wa ndani ili kuongeza idadi ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa ya moyo nchini hatua ambayo itasaidia kuongeza uwezo wa kutoa huduma hizo kwa wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya JKCI Dkt. Hassan Mahmoud Mshinda alisema mafanikio yaliyofikiwa na taasisi hiyo yametokana na weledi na kujituma kwa wafanyakazi wake katika utoaji wa huduma.

Dkt. Mshinda Aliongeza kuwa bodi imepokea ushauri uliotolewa na wadau mbalimbali na itaendelea kuufanyia kazi ili kuboresha zaidi huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na taasisi hiyo.

Kamati hiyo ya Bunge imeiagiza wizara husika kuipatia JKCI eneo zaidi litakalowezesha taasisi hiyo kupanua miundombinu na kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za matibabu ya moyo ili wananchi wengi zaidi wapate huduma za  matibabu ya moyo ya kisasa na bora bila kulazimika kwenda nje ya nchi.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi