Rushwa na Ukiukwaji wa maadili vyapigwa vita JKCI


Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Grace Matunda akitoa elimu ya maadili kwa viongozi na wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) hii leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI jijini Dar es Salaam. Elimu hiyo imelenga kuwajenga viongozi na wafanyakazi wa taasisi hiyo kuendelea kuwa na maadili mazuri katika maeneo yao ya kazi.

 Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum ya Dar es Salaam Hamadi Bakari akitoa elimu ya maadili ya Utumishi wa Umma kwa viongozi na wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

 Baadhi ya Viongozi na Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mafunzo ya maadili kwa viongozi wa utumishi wa yaliyokuwa yanatolewa na Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum ya Dar es Salaam Hamadi Bakari leo katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

************************************************************************************************************************************************************************************************************************

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi kwa kufuata kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma, ikiwemo matumizi ya lugha yenye staha, kuepuka rushwa na unyanyasaji pamoja na kuvaa mavazi yanayozingatia mwongozo wa kiutumishi.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani wakati wa mafunzo ya siku moja ya uadilifu kwa viongozi wa umma yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Dkt. Naizihijwa ambaye pia ni daktarin bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha watumishi umuhimu wa kuzingatia maadili mema ya kazi, kuwa mfano wa kuigwa na kutoa huduma kwa weledi bila upendeleo.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo wafanyakazi wa ngazi mbalimbali wa kusimama imara katika nafasi zao kwa kufuata miiko ya kiutumishi na kuwa na mwenendo mwema wa utumishi wa umma.

“Ninaamini mafunzo haya yataleta mabadiliko chanya katika utendaji wetu wa kazi za kila siku, kwani yameimarisha uelewa wa watumishi kuhusu wajibu wao na namna bora ya kuwahudumia wananchi wakiwemo wagonjwa”, alisema Dkt. Naizihijwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa JKCI, Ghati Chacha alisema ni takwa la Serikali kwa watumishi wote kuzingatia maadili ya kiutumishi ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa bora na zenye kuzingatia maslahi ya wananchi.

Alisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuzingatia misingi ya utu, haki, uwajibikaji na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwani maadili hayo ndiyo msingi wa kujenga taasisi imara na yenye kuheshimika mbele ya jamii.

 “Katika mafunzo haya tumekumbushwa kuwa viongozi tunatakiwa kuzingatia utu na haki, uadilifu na wawajibikaji ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wa ndani na nje” alisema Ghati.

Naye Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hamadi Bakari alisema mafunzo hayo yatawasaidia wafanyakazi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na hivyo kuepuka ukiukwaji wa maadili unaoweza kuathili utendaji kazi wa taasisi na serikali kwa ujumla.

Aidha, alibainisha umuhimu wa matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA kama vile kompyuta na vifaa vya kuhifadhia taarifa (flash) ili kulinda nyaraka za serikali na kuepusha madhara yanayoweza kusababisha matatizo ya kimaadili au kinidhamu.

“Wafanyakazi wakifuata taratibu za kazi na kanuni za utumishi wa umma wana uwezo mkubwa wa kutojiingiza kwenye matatizo ya ukiukwaji wa maadili katika taasisi kwa maslahi mapana ya serikali”, alisema Bakari.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Afisa Muuguzi wa JKCI, Jilala John alisema mafunzo hayo yatamsaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa kwa kuzingatia maadili, kuepuka vitendo vya rushwa na kutumia lugha ya faraja pamoja na kutunza siri za wagonjwa.

“Tunaishukuru serikali kupitia JKCI kwa kutupatia mafunzo haya ambayo ni muhimu kwetu katika kutoa huduma kwa wagonjwa, kwani tumesisitizwa kutumia lugha za faraja na kutunza siri za wagonjwa wetu”, alisema Jilala.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha misingi ya uadilifu, uwajibikaji na utawala bora katika taasisi za umma kwa lengo la kuongeza imani ya wananchi kwa watumishi wao.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi