Dkt. Kisenge: Tumuenzi Prof. William Mahalu kwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba akitoa neno la shukrani kwa wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma nzuri walizompatia aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo marehemu Prof. William Mahalu wakati wa uhai wake leo wakati familia ya Prof. Mahalu ilivyofika JKCI kwaajili ya kushukuru.
Mdogo wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Costa Mahalu akiwashukuru wafanyakazi wa
Taasisi hiyo kwa kumhudumia aliyekuwa kaka yake marehemu Prof. William Mahalu
wakati familia ya Prof. Mahalu ilipofika JKCI leo kwaajili ya kushukuru.
Prof. Costa Mahalu akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge zawadi ya kuthamini mchango uliotolewa na Taasisi hiyo wakati wa kumuuguza hadi kumpumzisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo marehemu Prof. William Mahalu leo wakati familia hiyo ilivyofika JKCI kwaajili ya kushukuru.
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) wakisikiliza wakati famila ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini
ya Taasisi hiyo marehemu Prof. William Mahalu ilivyofika JKCI leo kwaajili ya
kushukuru.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na wanafamilia ya Mahalu leo baada ya familia hiyo kufika JKCI kwaajili ya kutoa neno la shukrani kwa huduma alizopatiwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo marehemu Prof. William Mahalu wakati wa uhai wake.
Madaktari wa moyo wametakiwa kumuenzi aliyekuwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
marehemu Prof. William Mahalu kwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa wenye matatizo
ya moyo.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa
hafla fupi iliyofanywa na familia ya marehemu Mahalu kutoa neno la shukrani kwa
wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwa kumuuguza hadi kumpumzisha Marehemu Prof.
William Mahalu.
“Marehemu Prof. Mahalu ni mlezi wetu, asilimia kubwa ya
wataalamu wa magonjwa ya moyo hapa wamefundishwa naye, Tunamshukuru Mungu kwa
mambo makubwa ambayo ameyafanya katika sekta hii ya afya hasa upande wa
upasuaji wa moyo, tunaahidi kuyaenzi yote ili tusije tukapoteza jina lake”,
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema kabla ya kuanza safari yake ya matibabu
nchini India marehemu Prof. William Mahalu alikaa naye na kumuomba kuziendeleza
huduma za matibabu ya moyo kwa kuwafikia wananchi mahali walipo.
“Sasa hivi JKCI tumekuwa tukifanya huduma ya tiba mkoba kwa
kuwafuata wananchi mahali walipo na kuwapa huduma za uchunguzi na matibabu ya
moyo hii yote ni jitihada za marehemu Prof. Mahalu kutusihi tuwafikishie
wananchi huduma karibu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema ukiizungumzia historia ya Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete uwezi kuacha kumzungumzia Prof. Mahalu kwani yeye ni
miongoni mwa waanzilishi wa upasuaji wa moyo hapa nchini.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Jaji Joseph Sinde
Warioba aliwashukuru wataalamu wa afya wa JKCI kwa kumhudumia kwa kiwango cha
juu marehemu Prof. William Mahalu na kuhakikisha kuwa afya yake inaimarika.
“Huduma mlizompa hapa zilikuwa za hali ya juu, wakati wote
wahudumu walikuwa naye karibu, mlijitahidi sana kuokoa maisha yake lakini Mungu
akampenda zaidi”, alisema Mhe. Jaji Warioba.
Jaji Warioba alisema marehemu Prof. William Mahalu kimwili
hayupo lakini kiroho babo yupo kwani ameweza kuifanya kazi yake kwa kutoa
mchango mkubwa hapa nchini hivyo kuacha msingi katika huduma za kibingwa za
upasuaji wa moyo.
Naye mdogo wa marehemu Prof. Costa Mahalu aliwataka
wafanyakazi wa JKCI na wataalamu wa afya wengine wanaomfahamu marehemu Prof.
William Mahalu kuyasherehekea maisha yake kwa kuvienzi na kuviendeleza vile
alivyokuwa akivifanya wakati wa uhai wake.
Prof. Costa alisema wafanyakazi wa JKCI wamekuwa sehemu ya
familia ya Prof. Mahalu kwa upendo, ushirikiano na umoja waliokuwa nao tangu
kuumwa hadi kumpumzisha marehemu Prof. William Mahalu.
“Tunamshukuru Mungu mapenzi yake ameyatimizwa, marehemu Prof.
William Mahalu ametuachia upendo na familia ya JKCI tunamshukuru Mungu kwa
hilo”, alisema Prof. Costa
Comments
Post a Comment