Watu 689 wapimwa moyo Geita
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete akimpima jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiograph – ECHO) mwananchi wa Geita aliyefika katika banda la JKCI
wakati wa maonyesho ya sita ya kitaifa ya teknolojia ya madini yaliyomalizika
leo Mkoani Geita. Jumla ya watu 689 wamepatiwa huduma katika banda hilo.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
anayetoa huduma katika kliniki maalumu Grace Mbanga akimpima shinikizo la damu
mwananchi wa Geita aliyetembelea banda la JKCI wakati wa maonyesho ya sita ya
kitaifa ya teknolojia ya madini yaliyomalizika leo Mkoani Geita. Jumla ya watu
689 wamepatiwa huduma katika banda hilo.
Afisa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Elimiliki
Kileo akimpima urefu, uzito na uwiano wa urefu na uzito mkazi wa Geita aliyetembelea
banda la JKCI wakati wa maonyesho ya sita ya kitaifa ya teknolojia ya madini
yaliyomalizika leo Mkoani Geita. Jumla ya watu 689 wamepatiwa huduma katika
banda hilo.
Wananchi wa Mkoa wa Geita wakiwa katika foleni ya kupata
huduma katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa
maonyesho ya sita ya kitaifa ya teknolojia ya madini yaliyomalizika leo mkoani
Geita. Jumla ya watu 689 wamepatiwa huduma katika banda hilo.
Na JKCI
*****************************************************************************************************************
Watu 689 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa
ya moyo wakati wa maonyesho ya sita ya kitaifa ya Teknolojia ya madini
yaliyokuwa yakifanyika katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita na kumalizika leo.
Maonyesho hayo yalianza Septemba 20 hadi septemba 30, 2023 na
kutoa fursa kwa wananchi wa Geita na mikoa ya jirani kupima magonjwa ya moyo,
shinikizo la damu na sukari kwenye damu katika kliniki maalum iliyokuwa
ikifanywa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza na waaandishi wa habari leo wakati wa kuhitimisha
maonyesho hayo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete alisema katika maonyesho hayo watu 548
wamefanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph –
ECHO).
“Kati ya watu 689 waliopatiwa huduma katika banda la JKCI
watu wazima walikuwa 669 wanaume wakiwa 200 na wanawake 469 huku watoto wakiwa
20”, alisema Dkt. Salehe.
Dkt. Salehe alisema wananchi 213 wamekutwa na magonjwa
mbalimbali ya moyo ukiongoza ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, sukari kwenye
damu, moyo kutanuka, mishipa ya damu kuziba, magonjwa ya valvu (RHD) na
magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kwa watoto ambayo ni matundu na mishipa ya
damu kutokuwa sawa.
“Tumetoa rufaa kwa watu 28 watoto wakiwa watano na watu
wazima 23 kufika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya kupatiwa matibabu
zaidi huku wengine wakitakiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo kutokana na matatizo
waliyonayo”, alisema Dkt. Salehe
Dkt. Salehe alisema kuwa kati ya watu 173 waliokutwa na
tatizo la shinikizo la juu la damu zaidi ya nusu walikuwa na tatizo hilo bila
ya wao kujijua hivyo kuanzishiwa kliniki ya kufuatilia tatizo hilo kupunguza
athari ambazo wanaweza kuzipata kama hawatatibu tatizo la shinikizo la juu la
damu.
Aidha Dkt. Salehe amewahasa wananchi kufanya uchunguzi wa
afya zao mara kwa mara, kufanya mazoezi, kula matunda na mboga za majani kwa
wingi, pamoja na kupata usingizi wa kutosha ili kuweza kuwa na afya bora.
Kwa upande wake mwananchi aliyepatiwa matibabu katika kliniki
hiyo maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo Ester John aliushukuru uongozi wa
JKCI kwa kuwezesha huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi wa Geita kwani wengi
wao wasingeweza kupata huduma hiyo.
“Nawashukuru sana kwa huduma yenu nzuri mnayoitoa katika
banda hili, ninawaomba muendelee kuwa na moyo huu wa kujitoa kwetu sisi wana
Geita na hasa sisi walemavu, leo nimekutwa na shinikizo la juu la damu na
daktari kanipa ushauri mzuri naahidi kuufanyia kazi”, alisema Ester
Ester ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kuwekeza katika sekta ya afya na kuwapa fursa wananchi kuchunguza afya zao
bila gharama kama ambavyo ilikuwa katika banda la JKCI.
“Nilikuwa natamani sana kupima moyo wangu, nilikuwa naisikia
tu Taasisi hii ya Moyo Jakaya Kikwete leo nimefika na kujionea mimi mwenyewe
wataalamu wa afya wanatoa huduma nzuri”, alisema Ester
Naye mwenyeji wa Kagera Hendry Bamgaya alisema ametembelea
maonyesho hayo akiwa na lengo la kufuata huduma za matibabu ya moyo zilizokuwa
zikitolewa kwenye banda la JKCI baada ya kusikia uwepo wa wataalamu wa afya
kutoka JKCI kwenye maonyesho hayo.
“Nimepokelewa vizuri katika banda la JKCI, nimepimwa moyo
wangu na kukutwa na tatizo la moyo kutanuka. Nashukuru daktari kaniandikia dawa
za kutumia na kunipa ushauri wa nini cha kufanya”, alisema Hendry
Comments
Post a Comment