Idadi ya wagonjwa wa moyo na shinikizo la damu yaongezeka nchini
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu akikagua maeneo mbalimbali ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group alipofika katika Hospitali hiyo leo kwaajili ya maadhimisho ya siku ya moyp duniani.
Baadhi ya wananchi waliofika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam wakipata huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani.

Baadhi ya wananchi wakisoma vipeperushi vya shinikizo la juu la damu wakati wa maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyofanyika leo katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu akiwa katika
picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI), wanachama wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Moyo Nchini (TCS) na wawakilishi
wa makampuni ya uingizaji na usambazaji wa dawa za binadamu wakati wa
maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyofanyika leo JKCI Dar Group Hospitali.
**************************************************************************************************************************************************************************************
Takwimu za wizara ya Afya kupitia MTUHA (DHIS -2) zinaonesha kumekuwa na ongezeko la asilimia 9.4 kwa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu pekee kutoka wagonjwa milioni 2.5 mwaka 2017 hadi wagonjwa 3.4 mwaka 2022.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu wakati akizungumza
na wananchi waliohudhuria maadhimisho ya
siku ya moyo duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Mhe. Waziri Ummy alisema taarifa za ufuatiliaji wa magonjwa
yasiyoambukiza kutoka mwaka 1980 hadi mwaka 2020 inaonesha ongezeko la magonjwa
ya shinikizo la juu la damu na kisukari katika jamii kutoka asilimia 1 hadi 9
kwa wagonjwa wa kisukari na kutoka asilimia 5 hadi 26 kwa wagonjwa wa shinikizo
la juu la damu.
“Magonjwa haya mawili ndiyo chanzo kikuu cha magonjwa ya
moyo, figo pamoja na ugonjwa wa kiharusi hivyo ongezeko hili ni tishio kwa
ustawi wa afya ya jamii yetu na ndiyo sababu inatuweka hapa leo kujadili
mikakati ya kukabiliana nayo”,.
“Matatizo haya ya moyo na ugonjwa wa kiharusi yanaweza
kuzuilika kwa mtu mmoja mmoja na jamii yetu kuweza kuchukuwa hatua. Kwa mujibu
wa maelezo ya wataalam sababu zinazopelekea kuongezeka kwa magonjwa
yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya kiharusi ni pamoja na kutozingatia ulaji
unaofaa ambapo kwa nchi yetu inaonesha asilimia 3 tu ya watu wazima wanatumia
kiasi cha wastani wa kutosha cha matunda na mbogamboga”, alisema Mhe. Ummy
Mwalimu.
Akizungumzia kuhusu suala la kufanya mazoezi waziri Ummy
alisema idadi ya watu wazima wanaofanya mazoezi ni kubwa ukilinganisha na
watoto na vijjana ambapo takwimu zinaonesha kwa takribani asilimia 20 ya vijana
wote wenye umri wa chini ya miaka 17 wanaendekeza tabiabwete na kutoshughulisha
miili yao ipasavyo.
“Ninawasihi ndugu zangu mtenge muda wa kufanya mazoezi japo dakika
150 kwa wiki na mazoezi haya siyo lazima yawe ya kukimbia yanaweza kuwa hata ya
kutembea, kupima afya japo mara moja kwa mwaka, kupunguza vilevi na kuacha
kabisa matumizi ya tumbaku , kupunguza matumizi yaliyokithiri ya chumvi, sukari
na mafuta ya kupikia yenye lehemu na
kuzingatia ushauri wa muhimu unaotolewa na madaktari kwa kufanya hivi tutaweza kukabiliana na ongezeko la magonjwa haya yasiyoambukiza
ikiwemo tatizo la moyo pamoja na ugonjwa wa kiharusi”, alisema Mhe. Ummy.
Aidha Mhe. Waziri Ummy aliitaka Taasisis ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) pamoja na Hospitali za Kanda Maalum kufanya ulezi wa kuwajengea uwezo
hospitali zilizo chini ya ngazi zao kwenye mikoa na kanda walizopo kwa kushuka
chini na kufanya kambi za matibabu za pamoja, huduma mkoba na kuwaalika
wataalam kutoka hospitali hizo kuja kujishikiza kwao na kujifunza stadi
mbalimbali kutoka kwa muda mfupimfupi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu
wa wilaya ya Temeke Mhe. Mobhare Matinyi aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kufanya maadhimisho ya siku ya moyo duniani katika wilaya
yake na kuwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika zoezi la upimaji na
matibabu ya moyo.
“Ninawapongeza wananchi mliojitokeza siku ya leo kwaajili ya
kupima afya zenu, ninawaomba wananchi wengi zaidi mjitokeze siku ya kesho
ambapo zoezi la upimaji litakuwa linaendelea pia tutakuwa na matembezi ya
kupambana na magonjwa yasiyoambuikiza yatakayoanzia uwanja wa Taifa na kuishia
hapa JKCI Hospitali ya Dar Group”, alisema Mhe.Matinyi .
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alimshukuru waziri wa Afya kwa
kukubali kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo na kusema kuwa wataalamu
wamejipanga kufanya upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es
Salaam na mikoa ya jirani.
Dkt. Angela alisema katika kupambana na magonjwa
yasiyoambukiza Taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi ya jinsi ya
kuepukana na magonjwa ya moyo hii ikiwa ni pamoja na kutoa huduma ya tiba mkoba
ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan outreach Services kwa
kuwafuata wananchi mahali walipo na kufanya upimaji pamoja na kutoa ushauri.
“Tunakwenda katika mikoa mbalimbali hapa nchini kutoa huduma
za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi, katika maeneo hayo kumekuwa na uitikio mkubwa
na wengi wa watu tunaowapima tunawakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu,
kutanuka kwa misuli ya moyo, umeme wa moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya
moyo na kwa watoto tunawakuta na matundu
pamoja na mishipa yao ya damu kutokukaa katika mpangilio wake”, alisema Dkt.
Angela.
Naye Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Moyo Nchini (TCS) Robert
Mvungi alisema historia ya maadhimisho ya siku ya moyo duniani ilianza
kuadhimishwa mwaka 2000 na Shirikisho la Moyo Duniani kwakuona kuna umuhimu wa
kuwa na siku hyo hii ni kutokana na
matatizo ya moyo kuzidi kuongezeka.
“Duniani kote siku hii inaadhimishwa kwa kutoa uelewa kwa
wananchi kuhusu magonjwa ya moyo ili wajue jinsi ya kujikinga nayo pia
tunafanya upimaji wa magonjwa haya kwa wananchi na upimaji huu unafanyika bila
malipo yoyote yale ili kila mwananchi aweze kufikiwa na huduma hii”, alisema
Dkt. Mvungi.
Katika maadhimisho hayo ya siku ya moyo duniani Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa
Moyo Nchini (TCS) na makampuni mbalimbali ya uingizaji na usambazaji wa dawa za
binadamu wanatoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo pamoja na kutoa dawa kwa
wananchi wanaokutwa na matatizo. Huduma
hii ya siku mbili inatolewa bila malipo yoyote yale JKCI Dar Group Hospitali.
Comments
Post a Comment