Daktari bingwa wa upasuaji mgumu wa moyo kwa watoto duniani aipongeza Serikali


 Wataalamu wa upasuaji  wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na mwenzao kutoka Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland Prof.  Tomasz Mroczek wakifanya upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu ya moyo ambayo haijakaa katika mpangilio wake wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto iliyofanyika JKCI. Prof. Mroczek ni mmoja wa madaktari bingwa wachache duniani wanaofanya upasuaji mgumu wa moyo kwa watoto alifika JKCI ili kuona namna ambavyo madaktari wa taasisi hiyo wanavyofanya upasuaji na kuangalia jinsi watakavyoweza kushirikiana katika kufanya upasuaji mgumu zaidi.

***********************************************************************************************************************************************************************************************************

Mmoja wa madaktari bingwa wachache duniani wanaofanya upasuaji mgumu wa moyo kwa watoto Prof. Tomasz Mroczek kutoka Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland ameipongeza Serikali kwa kusomesha wataalamu wa moyo na kununua vifaa tiba vinavyotumia teknolojia ya kisasa.

 Prof. Mroczek alizitoa pongezi hizo hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa  kambi maalumu ya siku tano ya matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto waliyoifanya katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Prof. Mroczek alisema hii ni mara yake ya  kwanza kufika hapa nchini  na walikuja kuona namna ambavyo madaktari wa JKCI wanavyofanya upasuaji wa moyo na kuangalia jinsi watakavyoweza kushirikiana katika kufanya upasuaji mgumu zaidi.

“Kitu nilichokitegemea kukikuta siyo nilichokikuta hapa, nimekuta madaktari wanafanya upasuaji mgumu wa kurekebisha mishipa ya damu ya moyo ambayo haijakaa katika mpangilio wake kwa kutumia muda mfupi tofauti na nchi zingine nilizokwenda pia kuna wataalamu wazuri na vifaa tiba viko vya kutosha na vya kisasa vinavyoenda na teknolojia ya matibabu ya moyo inayotumika katika nchi zilizoendelea”,.

“Nimekutana na watalamu wazuri ambao tumefanya nao upasuaji wa moyo kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ninaamini ushirikiano huu utakuwa endelevu ili sote kwa pamoja tuweze kuwahudumia watanzania wenye matatizo ya moyo”, alisema Prof. Mroczek.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliwashukuru wataalamu hao kutoka nchini Poland ambao walifanya upasuaji mkubwa  kwa watoto na mdogo kwa watu wazima  na kusema kuwa ujio wao  unaenda kufungua milango ya mafunzo kwa madaktari hapa nchi.

 Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo alisema  kwa muda wa siku tano ambao madaktari hao walikuwepo katika Taasisi hiyo wameweza kufanya upasuaji mgumu wa moyo na kutoa mafunzo na ujuzi kwa wataalamu wa JKCI.

 “Tulisaini makubaliano na wenzetu wa Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland ya kushirikiana katika mafunzo, tafiti na kufanya matibabu. Ushirikiano huu umeanza kufanya kazi na utakwenda kufungua milango ya kufanya tafiti mbalimbali zitakazoleta manufaa kwa nchi ikiwepo uingizaji wa fedha za kigeni”, alisema Dkt. Kisenge.

 "Walipofika wametuonyesha vitu ambavyo kwetu sisi ilikuwa ni vigunu kufanya kwani wamekuja kutuonyesha namna ya kutumia mitambo iliyopo ikiwepo kurekebisha mishipa ya damu kwenye moyo”, alisema Dkt. Kisenge.

 Prof. Bartconie Guzlk kutoka Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland ambaye kwa kushirikiana na wataalamu wa kuzibua mishipa ya damu wa JKCI walifanya upasuaji  mgumu (Complex Percutaneous Coronary Intervention – PCI)  wa kuzibua mshipa wa moyo iliyokuwa imeziba kwa asilimia 99 na hivyo kushindwa kupitisha damu vizuri  kwa wagonjwa 14 alisema madaktari wa Tanzania wapo tayari kujifunza kwaajili ya kusaidia watu wenye  matatizo ya moyo kwani wanafanya kazi  kwa bidii na umakini mkubwa.

 "Tutaendelea kushirikiana na JKCI katika kufanyakazi ya kuwatibu watu wenye matatizo ya moyo na kufanya tafiti zitakazosaidia katika matibabu, hii ni mara yangu ya kwanza kuja Tanzania nimefurahi na nimeipenda hii nchi ninaahidi tutaendelea kushirikiana zaidi”, alisema Prof. Guzlk.

 Uzibuaji wa mishipa hiyo ulifanyika kwa njia ya upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo (Minimum Invasive Surgery) bila kufungua kifua kwa kutoboa mshipa kwenye paja (Percutaneous Coronary Angioplasty) kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalum kwa ajili ya uchunguzi na tiba za magonjwa ya moyo.

 Awali Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI Dkt. Angela Muhozya amesema uwepo wa madaktari hao ambao ni  Daktari bingwa wa moyo na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto umetoa fursa kwa wao kujifunza mambo makubwa zaidi katika upasuaji wa moyo.

 "Tangu tumeingia nao mkataba ni mwaka sasa na tulipopata nafasi ya kuwatembelea wenzetu katika chuo chao  tuliona ni namna gani wanafanya upsauaji wa mishipa ya damu pamoja na moyo tukatumia fursa hiyo kuomba waje nchini ili na sisi tuweze kufaidika,"alisema Dkt. Angela.

 Naye  daktari bingwa wa upasuaji moyo kwa watoto wa JKCI Godwin Sharau alisema uwepo wa madaktari bingwa kutoka Poland umesaidia kwa wao kujifunza zaidi kwani madaktari hao ndani ya siku tatu wamefanikiwa kuwafanyia upasuaji mkubwa watoto watano ambao ulikuwa mgumu kwa wao kufanya.

"Tumekutana na madaktari ambao tunaamini tunaweza kufika kwenye viwango vya juu kutokana na utendaji wetu na pia kwetu ni fursa kwani Prof. Mroczek anatumiwa na watu wengi duniani katika kusaidia watoto”, alisema Dkt. Sharau.


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari