Upimaji na matibabu ya moyo katika maadhimisho ya siku ya moyo Duniani

 

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Christine Yonathan akimpima shinikizo la damu (BP) mpiga picha wa kituo cha Televisheni cha ITV Idrissa Magomeni wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili inayofanyika katika Hospitali hiyo mwanzoni mwa mwezi huu. 

*****************************************************************************************************************************************************************************************************************

TAARIFA KWA UMMA

UPIMAJI NA MATIBABU YA MAGONJWA YA MOYO KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA MOYO DUNIANI

Katika kuadhimisha siku ya Moyo Duniani tarehe 29/09/2023 yenye kauli mbiu “Tumia Moyo, Kulinda Moyo Wako” wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Bingwa wa Moyo Tanzania (TCS) watatoa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo  kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Upimaji huu utafanyika katika viwanja vya Hospitali ya JKCI Dar Group iliyopo TAZARA wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam kwa siku mbili za tarehe 29/09/2023 na tarehe 30/09/2023 kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa 10 kamili  jioni.

Aidha katika upimaji huu kutakuwa na wataalamu wa lishe ambao watatoa elimu ya lishe bora ambayo itawapa wananchi uelewa na  kufuata mtindo bora wa maisha na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo ambayo yanaweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.

Tunawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupima afya zenu kujua kama mna matatizo ya moyo ili kuanza matibabu mapema kwa atakayegundulika kuwa mgonjwa. Huduma hii itatolewa kwa watoto na watu wazima bila malipo yeyote yale.

Maadhimisho haya yataenda sambamba na matembezi ya umbali wa kilomita nne (4KM) ya kuhamasisha jamii kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo. Matembezi haya yatakayoanzia Uwanja wa Taifa na kuishia JKCI Dar Group yatakayofanyika tarehe 30/09/2023 kuanzia saa 12.30 asubuhi. Tunawaomba wananchi muungane nasi katika matembezi haya ili tufanye mazoezi ya pamoja yatakayotusaidia  kujikinga na magonjwa ya moyo.

Kwa taarifa zaidi wasiliana kwa simu namba 0754578190 Dkt. Tulizo Shemu, 0684345921 Flaviana Masegesa, 0783922571 Irene Charles na 0674179036 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group.

 “Tumia Moyo, Kulinda Moyo Wako”.

 


Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024