Wasemavyo wakazi wa Geita huduma za matibabu ya moyo


Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anayetoa huduma katika kliniki maalum ya VIP Grace Mbanga akimpima sukari kwenye damu mkazi wa Geita aliyetembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho ya sita ya kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.

**************************************************************************************************************

Wananchi wa Mkoa wa Geita wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kufikisha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi hao bila gharama.

Shukrani hizo zimetolewa na wananchi mbalimbali waliotembelea banda la JKCI lililopo katika maonesho ya sita ya kitaifa ya Teknolojia ya madini yanayoendelea katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Donard Francis alisema Taasisi ya JKCI imeonyesha kuwajali watanzania ambao hawakuwa na matarajio ya kuchunguza mioyo yao kutokana na mazingira waliyopo hivyo kuwaomba kuendelea kushiriki katika matukio mbalimbali yatakayowapa nafasi wananchi kujua afya ya mioyo yao.

“Leo kwa mara ya kwanza nimepima moyo wangu, nimepima sukari kwenye damu na shinikizo la damu, kwakweli sikujua kama kuna umuhimu wa kuchunguza magonjwa haya hapo awali lakini kupitia Taasisi hii nimepata elimu ambayo nitawaelimisha na wenzangu umuhimu wa kuchunguza afya zao”, alisema Donard

Kwa upande wake Sada Hassan mkazi wa Geita aliyepatiwa huduma katika banda la JKCI alisema kuwa yeye ni mjamzito anayetarajia kujifungua wakati wowote wiki hii lakini tangu alipobeba ujauzito huo hakuwahi kupima shinikizo la damu hadi wiki hii ya mwisho alipoenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita na kupimwa shinikizo la damu ambapo majibu yake hayakuwa mazuri.

“Nimetoka kijiji cha Nyang’wale ambapo nimekuwa nikienda kliniki lakini sikuwahi kupimwa shinikizo la damu, leo nimefika katika banda la JKCI nimepimwa shinikizo la damu na kuanzishiwa dawa ili niweze kutoka katika hatari ya kupata madhara wakati wa kujifungua maana shinikizo langu la damu lipo juu”, alisema Sada

Sada alisema amefurahia huduma alizopata katika banda la JKCI kwani hata mtoto wake aliyopo tumboni ameweza kufanyiwa uchunguzi wa moyo wake na kuonyesha kuwa yupo salama.

“Wanawake wenzangu ambao wana ujauzito wafike katika banda la JKCI kuchunguza kama afya zao zipo sawa kuondokana na athari zinazoweza kujitokeza kipindi cha ujauzito na wakati wa kujifungua kama wataalamu wa afya wanavyoelimisha”, alisema Sada

Akitoa wito kwa Taasisi nyingine zinazotoa huduma za afya Victor Maduhu ameziomba Taasisi za afya kuwafuata wananchi walipo kama ambavyo JKCI imefanya ili wananchi wapate huduma za afya kiurahisi kwani watu wengi wanahitaji huduma za kibingwa lakini kutokana na hali zao kiuchumi wanakosa fursa ya kupata huduma hizo.

Victor alisema Serikali imewekeza vizuri katika sekta ya afya ambapo sasa hivi hakuna haja ya mtu kufuata huduma za kibingwa nje ya nchi kwani huduma zote za kibingwa zinapatikana hapa Tanzania.

“Naipongeza sana Serikali yangu kuwekeza katika huduma za afya, ila nawaomba wataalamu wa afya kutoka Taasisi za kibingwa kuiga mfano wa JKCI kutufikia kwani sisi wananchi wenye uchumi wa chini tunawahitaji sana ili tupate huduma kwa karibu na kirahisi bila ya kuhangaika”, alisema Victor

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa magari