Bulembo aipongeza JKCI kupeleka vipimo waliko wananchi
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo akiwasili katika viwanja vya Hospitali ya wilaya hiyo kwaajili ya kuangalia huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinatolewa na wataalamu ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali hiyo. Kulia kwa Mkuu wa Wilaya ni Mkurugenzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group Dkt. Tulizo Shemu.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Hospitali ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dar Group Dkt. Tulizo Shemu kuhusu kambi maalumu ya upimaji na matiababu ya moyo inayofanywa na wataamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Wilaya Kigamboni.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Halima Bulembo ameipongeza
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwafuata wananchi wa Wilaya hiyo na
kuwapatia huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Pongezi hizo amezitoa jana alipotembelea kambi maalumu ya uchunguzi
na matibabu ya moyo inayofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni.
Kambi hiyo ya siku tano inafanywa na wataalamu wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya wilaya
Kigamboni.
Mhe. Halima alisema wataalamu wa JKCI wamekuwa wakijitoa
kuhakikisha huduma za matibabu ya moyo zinawafikia wananchi mahali walipo kama
ambavyo wamefanya kuwafikia wananchi wa Kigamboni.
“Tunawapongeza sana kwa kujitoa kwenu, tunaamini huduma mnazozitoa
sio kazi rahisi lakini mmendelea kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma za
kibingwa”, alisema Mhe. Halima.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alisema JKCI
imekuwa ikizunguka maeneo mbalimbali nchini kuangalia ukubwa wa matatizo ya magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo yanayogharimu maisha ya watu wengi na
kupunguza nguvu kazi ya watanzania.
Dkt. Shemu alisema kupitia huduma ya tiba mkoba ijulikanayo
kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services JKCI inazingatia
utoaji wa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali
walipo kutoa huduma za kibobezi za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
pamoja na elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa hayo.
“Tumekuwa tukishirikiana na makampuni mbalimbali
yanayosambaza dawa za binadamu katika kambi tunazofanya ili tunapopata wagonjwa
katika maeneo tunayotembelea tuweze kuwapatia dawa bila gharama”, alisema Dkt.
Shemu.
Dkt. Shemu alisema hadi sasa katika kambi hiyo wameshatoa huduma kwa wananchi zaidi ya 150 ambapo baadhi yao wamekutwa na magonjwa yasiyoambukiza na wengine wameshapewa rufaa kufika JKCI kwaajili ya uchunguzi zaidi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Comments
Post a Comment