Magonjwa ya kinywa, meno na njia ya hewa tishio matatizo ya valvu za moyo
Madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya
damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Open
Heart International (OHI) lililopo nchini Australia wakimfanyia mgonjwa
upasuaji wa kupandikiza valvu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku sita iliyomalizika
leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya wagonjwa 25
watoto 16 na watu wazima tisa walifanyiwa upasuaji katika kambi hiyo.
*********************************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Magonjwa ya kinywa, meno na njia ya hewa kama hayatatibika kikamilifu yanaweza kusababisha matatizo ya watu kupata magonjwa ya valvu za moyo (Rheumatic Heart Diseases).
Hayo yamesemwa leo na
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Angela Muhozya wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya
upasuaji wa moyo iliyomalizika leo katika Taasisi hiyo.
Kambi hiyo ya siku sita ya upasuaji wa moyo kwa watoto na
watu wazima imefanywa na wataalamu wa moyo
wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Open Heart International
(OHI) la nchini Australia.
Dkt. Angela alisema magonjwa ya valvu za moyo yamekuwa tatizo
kubwa hapa nchini kutokana na idadi ya wagonjwa hao kuongezeka kutokana magonjwa
ya mafua na kifua kutotibiwa vizuri.
“Mgonjwa mwenye matatizo ya valvu za moyo hupata tatizo hilo
akiwa na umri mdogo na baadaye kuanza kuonyesha dalili za kupata madhara kwenye
moyo hivyo kupelekea valvu kuvujisha damu au valvu kufunga na kutokupitisha
damu vizuri”, alisema Dkt. Angela
Dkt. Angela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na
wagonjwa mahututi alisema matibabu ya matatizo ya valvu hufanyika kwa kubadilisha
na kuweka valvu za bandia ili kuiruhusu damu kuzunguka kwenye moyo kama
inavyotakiwa.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo ambapo wagonjwa 25 watoto wakiwa 16 na watu wazima tisa
walifanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo Dkt. Angela alisema wataalamu wa JKCI pia
walipata mafunzo ya jinsi ya kufanya
upasuaji wa moyo kwa watu wazima wenye matatizo ya valvu za moyo.
“Upande wa matibabu ya watoto, katika kambi hii tumetoa
huduma kwa watoto wenye matatizo ya matundu kwenye moyo, kurekebisha mishipa ya
damu pamoja na kuwafanyia upasuaji wa mara ya pili watoto ambao tayari
walishafanyiwa upasuaji”, alisema Dkt. Angela.
Naye daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu
kutoka Shirika la Open Heart International (OHI) la nchini Australia Dkt. Hugh
Wolfenden alisema wanashirikiana na JKCI kuongeza ujuzi kwa wataalamu wanaotoa
huduma za upasuaji wa moyo pamoja na kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma za
upasuaji wa moyo.
Akizungumzia kuhusu matatizo ya valvu za moyo Dkt. Wolfenden
alisema nchini Austaria wangonjwa wenye matatizo ya valvu za moyo wamepungua
kutokana na elimu inayowekezwa katika jamii tangu utoto kuhusu afya ya kinywa
na meno.
“Nchini Australia elimu kuhusu afya ya kinywa na meno
inatolewa mara kwa mara ili kuhakikisha jamii inakuwa na mazoea ya kupiga
mswaki kila baada ya kula chakula, umuhimu wa kukaa maeneo masafi na yasiyo na
msongamano ili kuzuia magonjwa ya mfumo wa hewa yanayoweza kupelekea kupata
magonjwa ya valvu za moyo”,.
“Nimeshafanya kazi kwa kipindi cha miaka 32 sasa, idadi ya wagonjwa wenye matatizo ya valvu za moyo Australia ni wachache kwa sasa kwani jamii inajikinga zaidi kuepuka kupata magonjwa yanayosababishwa na afya ya kinywa” na meno, alisema Dkt. Wolfenden.
Comments
Post a Comment