JKCI yapewa tuzo ya umahiri wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza
Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Genofeva Matemu akimweleza Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof.Paschal Ruggajo huduma zinazotolewa kwenye banda la Taasisi hiyo wakati wa mkutano wa kimataifa wa kisayansi wa magonjwa yasiyoambukiza unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere.
Picha na Khamisi Mussa
***************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepokea tuzo ya umahiri kutokana na jitihada zake na kuelimisha jamii jinsi ya kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kutoa huduma ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo.
Tuzo hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo wakati wa mkutano wa kimataifa
wa kisayansi wa magonjwa yasiyoambukiza unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa
wa mikutano wa Julius Nyerere.
Akizungumza wakati alipotembelea banda la Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Ruggajo aliipongeza JKCI kwa kutoa huduma za
kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo na hivyo kupunguza asilimia 80 ya
wagonjwa wa moyo waliokuwa wakipelekwa na Serikali nje ya nchi kwaajili ya matibabu.
“Ninawapongeza sana kwa kuratibu zoezi la utalii tiba nchini
kwani mmekuwa mkipokea wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi ambao wanafika katika
Taasisi yenu kwaajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo”, alisema Prof.
Ruggajo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt.Peter Kisenge
alisema moja ya kipaumbele ambacho Taasisi hiyo imejiwekea ni kudhibiti
magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa elimu ya magonjwa ya moyo pamoja na lishe
bora kwa wananchi na kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa ya
moyo kwa kuwafuata wananchi mahali walipo.
Dkt. Kisenge alisema
hadi sasa wameshatoa huduma hiyo ya tiba mkoba katika mikoa zaidi ya 10 na
kuwafikia wananchi zaidi ya 7000 na hivi karibuni watakwenda kutoa huduma ya
uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo katika mikoa ya Arusha, Tabora, Kigoma
na wilaya za Siha na Kigamboni.
“Huduma hii inajulikana kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan Outreach Services ambapo hadi sasa tumeshatoa huduma hii katika mikoa ya
Tanzania Bara na Visiwani na huduma tunazozitoa ni pamoja na elimu ya lishe na
matumizi sahihi ya dawa za moyo, uchunguzi na upimaji wa magonjwa ya moyo,
shinikizo la damu na kisukari”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema magonjwa yasiyoambukiza yanachangia vifo vingi duniani kote karibu watu milioni 17 wanapoteza maisha yao kutokana
na magonjwa hayo.
Katika mkutano huo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatoa elimu ya jinsi ya kuyatambua magonjwa ya moyo pamoja na kueleza huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa.
Comments
Post a Comment