Madaktari wa watoto wapewa mafunzo ya kufanya kipimo cha ECHO
************************************************************************************************************************************************************************************************************
Madaktari 22 wanaotoa huduma kwa watoto kutoka Tanzania na nje ya nchi wanashiriki mafunzo maalumu ya awali ya namna ya kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) kwa watoto.
Mafunzo hayo ya siku tano yanafanyika kwa mara ya sita tangu
yalipoanzishwa mwaka 2018 yakiratibiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kushirikiana na Shirika la Madaktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka
Ujerumani (GTP) na chama cha madaktari wa watoto Tanzania (PAT).
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Stela Mongela alisema mafunzo
hayo yamewalenga madaktari wanaotoa huduma kwa watoto ili waweze kubaini
magonjwa ya moyo kwa watoto mapema na watoto waweze kupatiwa matibabu
wanayostahili kwa wakati.
“Kati ya madaktari 22 wa watoto wanaoshiriki katika mafunzo
ya mwaka huu watano wametoka nchini Uholanzi na Ujerumani na wengine 17
wametoka katika mikoa ya Mtwara, Morogoro, Dodoma na Dar es Salaam”, alisema
Dkt. Stella.
Dkt. Stella alisema wanatarajia baada ya mafunzo hayo kumalizika
wataalamu wa afya walioshiriki watakuwa wamepata maarifa yakuweza kufanya
kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) kwa
watoto na kuchukuwa maamuzi stahiki pale watakapokutana na watoto wenye shida
za moyo.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo Daktari bingwa wa magonjwa ya
watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Nsajigwa Misidai alisema mafunzo
hayo yatawasaidia kuwa wafanisi zaidi katika kugundua magonjwa ya moyo kwa
watoto mapema.
Dkt. Nsajigwa ambaye ni daktari katika wodi ya watoto
wachanga (Neonatal) alisema kwasababu yeye anafanya kazi katika wodi ya watoto
wenye umri wa kuanzia siku moja hadi siku 28 ataweza kuwafuatilia kwa karibu na
pale atakapoona dalili za magonjwa ya moyo kwa mtoto atachukua hatua za haraka
kuhakikisha mtoto anapata matibabu kwa wakati.
“Nimefurahi sana kushiriki katika mafunzo haya ambayo
yanaenda kunirahisishia majukumu yangu ya kazi kwani nitakuwa na uwezo wa kuwagundua
watoto wenye shida za moyo mapema na kuwapa matibabu stahiki mapema”, alisema
Dkt. Nsajingwa
Tangu mafunzo hayo yalipoanza kutolewa mwaka 2018 madaktari
wanaotoa huduma kwa watoto 100 kutoka Tanzania na nchi za nje wameweza
kushiriki mafunzo hayo.
Comments
Post a Comment