Wakuu wa Vitengo wa JKCI wapewa mafunzo ya kufanya kazi kimkakati na kufikia malengo waliyojiwekea
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wakuu wa vitengo kutoka JKCI wakati wa
kufunga mafunzo ya siku mbili yaliyotolewa kwa viongozi hao na Taasisi ya
Uongozi katika ukumbi wa Hoteli ya Giraffe iliyopo jijini Dar es Salaam
Na: JKCI
*******************************************************************************************************
Wakuu wa Vitengo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wametakiwa kutumia ujuzi walioupata kupitia mafunzo ya uongozi kufikia dira na
malengo ya Taasisi hiyo kuiwezesha Taasisi kuwa kituo cha umahiri cha utalii
tiba katika kutoa matibabu ya moyo Barani Afrika.
Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akifunga mafunzo ya siku
mbili kwa viongozi hao yaliyotolewa na Taasisi ya Uongozi na kufanyika katika
Hoteli ya Giraffe iliyopo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Kisenge alisema mafunzo hayo yaendelee kuandaliwa mara
kwa mara lengo likiwa kuwakumbusha viongozi kuchukua majukumu yao, kuwa na
mahusiano mazuri na wafanyakazi wanaowaongoza ili kwapamoja waweze kufikia
malengo ya Taasisi.
“Ninaimani kubwa mkitoka hapa mtaenda kuyafanyia kazi yale
yote mliyofundishwa kwa siku mbili ambayo yakifuatwa kama mlivyojifunza
mabadiliko makubwa yataenda kutokea katika vitengo vyenu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema mafunzo hayo yametoa fursa kwa wakuu
wa vitengo wa JKCI kujifunza namna bora
ya kuongoza, umuhimu wa mawasiliano pamoja na usimamizi wa rasilimali za umma.
“Kama viongozi mnatakiwa kuwa na ujuzi ambazo utasaidia
kuwaongoza watu walio chini yanu ili kwa pamoja muweze kufikia malengo ambayo
yatawasadia wakati wa kuandaa mpango mkakati katika vitengo vyenu.
Aidha Dkt. Kisenge aliwashukuru wawezeshaji kutoka Taasisi ya
Uongozi kwakuwa karibu na JKCI kwani wanapowahitaji kwaajili ya kutoa mafunzo
kwa wafanyakazi wa JKCI wamekuwa mstari wa mbele kutoa huduma na kuleta mabadiliko
katika utendaji wa kazi.
Kwa upande wake mwezeshaji kutoka Taasisi ya Uongozi Fortune
Ekklesiah alisema mafunzo kwa viongozi husaidia kuwaonyesha umuhimu wa kufanya
kazi kwa pamoja na watu wanaowaongoza ili kuleta tija katika utendaji wa kazi.
Fortune alisema viongozi wanatakiwa kuwa na uwezo wa
kutambua, kutafuta ufumbuzi, kushirikisha na kufanyia kazi yale yote
yanayohusiana na idara/vitengo vyao bila ya kuingilia idara/vitengo vingine.
“Katika mafunzo haya tumefanya baadhi ya mafunzo kwa vitendo
lengo likiwa kuona ushirikiano unavyojengwa katika kutafuta ushindi lakini pia
kuangalia kiongozi anachukua majukumu gani kuhakikisha kundi lake linafikia
malengo yaliyokusudiwa”, alisema Fortune
Akielezea mafunzo hayo Mkuu wa kitengo cha Rasilimali watu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Abdulrahman Muya alisema mafunzo hayo kwa
viongozi yamefanyika kutekeleza mpango mkakati wa utekelezaji wa majukumu kwa mwaka
wa fedha 2023/2024.
Muya alisema mada zilizotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja
na Uongozi, kujitambua, akili hisia, mawasiliano ya kimkakati, kutunza mali za
umma katika sehemu za kazi, namna ya kutambua viashiria vya hatari eneo la kazi,
na namna ya kutengeneza mikakati ya kukabiliana na viashiria vya hatari endapo
vitatokea.
“Tunaamini viongozi hawa wanaenda kuwa mabalozi wa kufanya
mabadiliko katika maeneo yao ya kazi na kuwa timilifu katika uongozi ili waweze
kusaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi”, alisema Muya
Naye mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mkuu wa wauguzi
Hospitali ya JKCI Dar Group Magreth Mbaruku aliushukuru uongozi wa Taasisi hiyo
kwakutoa nafasi kwa wakuu wa vitengo kupata mafunzo hayo yaliyoweza
kuwakumbusha wajibu wao kama viongozi.
“kupitia mafunzo haya nimejua mimi kama kiongozi natakiwa
kujitambua na baadaye kuwatambua watu ninaowaongoza kwasababu kila mtu ametoka
katika mazingira tofauti hivyo kama hatutatambuana vizuri tunaweza kukwamisha
kazi kutokufanyika kutokana na matendo ya mtu au watu tunaowaongoza”, alisema
Magreth
Magreth alisema mafunzo hayo yataenda kumsaidia katika
majukumu yake ya kila siku kufikia malengo ya kitengo anachokiongoza kwa
kushirikiana na wenzake na kujenga mahusinao mazuri.
Comments
Post a Comment