Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa
habari katika kambi maalumu ya upasuaji wa moyo inayofanywa na wataalamu wa
JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Open Heart International la
nchini Australia.
***********************************************************************************************************************************************************************************************
Madaktari nchini
wameombwa kuwapeleka wagonjwa wenye matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili
ya matibabu na siyo nje ya nchi kwani Serikali imewekeza vya kutosha katika vifaa
tiba na rasilimali watu.
Ombi hilo limetolewa leo jijini
Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kambi maalumu ya
upasuaji wa moyo inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao
kutoka Shirika la Open Heart International la nchini Australia.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni
daktari bingwa wa moyo alisema kutokana na uwekezaji mkubwa ambao Serikali
umeufanya katika Taasisi hiyo hivi sasa wagonjwa wengi ambao ni watanzania na
wasio watanzania wanatibiwa JKCI.
“Ni muhimu wagonjwa wenye
matatizo ya moyo wakatibiwa hapa nchini hakuna haja ya kuwapeleka nje ya nchi
kwani huduma zinazotolewa huko ndizo zinazopatikana katika Taasisi yetu”,
alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema katika
kipindi cha miezi mitatu iliyopita kuanzia Julai hadi Oktoba taasisi hiyo
imepokea wagonjwa 60 kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Demokrasia ya Kongo,Malawi,Visiwa
vya Comoro, Burundi na Zimbabwe.
"Tulishangazwa
kupokea wagonjwa kutoka Ujerumani na Ufaransa ambao wamekuja kutalii hapa
nchini lakini baada ya kupata matatizo walikuja kutibiwa katika hospitali yetu, miaka ya nyuma walikuwa wanakwenda
Kenya na mataifa mengine lakini sasa
wanakuja kwetu hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika,"alisema
Dkt.Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema katika
kambi hiyo ambayo itamalizika kesho wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji huku wataalamu
wa Taasisi hao wakipewa mafunzo ya kubadilishana ujuzi katika upasuaji wa moyo.
Akizungumzia kuhusu magonjwa ya
moyo Dkt. Kisenge alisema sababu kubwa
ya ugonjwa huo ni shinikizo la juu la damu ambalo chanzo chake ni ulaji
wa chumvi isiyopikwa, kutofanya mazoezi,matumizi ya sigara, pombe, unene
kupitiliza na msongo wa mawazo na namna ya kukabili ugonjwa huo ni kuepuka
vihatarishi vyake.
Aidha Dkt. Kisenge aliwasisitiza
wananchi kujiunga na bima ya afya kwani gharama ya matibabu ya moyo ni kubwa
lakini kama mtu akijunga na bima hiyo
itamsaidia kulipia gharama za matibabu pindi atakapoumwa.
“Gharama ya upasuaji wa moyo
zinafika hadi milioni 15 au zaidi lakini kama mgonjwa atakuwa na bima ya afya
itamsaidia kulipia gharama za matibabu hayo”, alisisitiza Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi
wa Shirika la Open Heart International la nchini Australia Dkt. Darren Wolfers alisema
wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya JKCI tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015.
Dkt. Wolfers alisema jambo kubwa
linalowavutia kufika mara kwa mara JKCI kutoa mafunzo na kufanya kambi za
upasuaji wa moyo ni upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wenye
ujuzi mkubwa vinavyowawezesha kufanyika
kwa upasuaji.
Comments
Post a Comment