JKCI yakutana na wazabuni wake
Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delilah Kimambo akielezea namna ambavyo Idara yake inafanya kazi na waagizaji na wasambazaji wa dawa za binadamu na vifaa tiba wakati wa kikao cha kuimarisha uhusiano na kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili wazabuni wa huduma na bidhaa wa Taasisi hiyo kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Daniel Bunare akijibu hoja zilizotolewa na wazabuni wa huduma na bidhaa wa Taasisi hiyo wakati wa kikao cha kuimarisha uhusiano na kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili washitiri hao kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amewaomba wazabuni wa huduma na bidhaa wa Taasisi hiyo kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na kwa wakati.
Dkt. Kisenge ametoa
ombi hilo leo wakati wa kikao chake na wazabuni wa huduma na bidhaa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa
Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Dk. Kisenge alisema ili kuhakikisha dira ya Taasisi hiyo ambayo
ni kuwa Taasisi yenye ubora wa kimataifa katika utoaji wa matibabu ya moyo,
mafunzo na utafiti inafanikiwa ushirikiano wa pamoja unahitajika baina ya JKCI na
wadau wake.
“Tukifanya kazi kwa pamoja tutatimiza dira ya JKCI, jukumu
letu sisi ni kuhakikisha tunawalipa kwa wakati na jukumu lenu ni kuhakikisha
mnaleta vifaa tiba na kutoa huduma iliyo bora na kwa wakati lakini kama kila
mtu atashindwa kutimiza wajibu wake hatutaweza kufikia dira ya Taasisi”,.
“Zabuni za manunuzi ya vifaa na huduma katika Taasisi yetu zinatangazwa kupitia mfumo
wa ununuzi wa umma kwa njia ya mtandao - NeST kwa uwazi na kwa wakati, ni
jukumu lenu kujisajili huko na kuhakikisha mmeomba na ikitokea mmeshindwa jinsi
ya kuomba ombeni msaada kutoka ofisi ya manunuzi na ugavi ili wawaelekeze”, alisema Dkt. Kisenge.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo
aliwasihi washitiri hao badala ya kuagiza dawa za binadamu pamoja na vifaa tiba nje ya nchi wajenge viwanda hapa nchini
ili kurahisisha kupatikana kwa vifaa hivyo kirahisi zaidi.
Aidha Dkt. Kisenge alisema taasisi hiyo inahudumia wagonjwa
wengi kutoka nje ya nchi hii ni kutokana
na huduma bora inazozitoa na hivyo
kutimiza maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Tanzania kuwa nchi ya utalii
wa matibabu.
Nao wazabuni wa huduma na bidhaa wa Taasisi hiyo walishukuru kwa kuitwa kwao kushiriki katika
mkutano huo na kusema kuwa umewasaidia kubadilishana mawazo, kuzidi kujenga na kuimarisha uhusiano kati yao na JKCI na kuonesha
jinsi ambavyo JKCI imejipanga kuboresha
huduma za matibabu.
Sandip Datta kutoka Computech Ltd. ambao ni wasambazaji wa
vifaa tiba alishukuru kwa ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wafanyakazi wa JKCI
na kusema kuwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete hawapati changamoto kubwa
ukilinganisha na Taasisi nyingine ambazo wanafanya nao kazi ni rahisi kwao watoa
huduma na wazabuni kupata huduma.
“Sisi wasambazaji wa vifaa tiba huwa tunakutana na changamoto
kutoka kwa watengenezaji wa vifaa tiba ambao wako nje ya nchi kuna wakati wanatupatia
vifaa vichache hatupati vyote kutokana
na oda tunayowapa na kutufanya tulete vifaa pungufu tofauti na oda tuliyopewa, lakini
tunajitahidi vifaa hivyo vinapokuwa tayari tunavileta kwa wakati ili wagonjwa
wasikose huduma”,alisema Sandip.
“Kupanda kwa dola kuliwasababishia vifaa vingi kupanda bei na kutokufika kwa wakati na wazabuni wengine walikaa kimya kwani walishindwa kuleta bidhaa husika kama Taasisi muangalie kwa baadaye kama hali hiyo itatokea mtafanyaje ili kukabiliana na changamoto hii”, alisema Ibrahim Kuhoga kutoka kampuni ya usambazaji wa dawa za binadamu ya AstraZeneca Ltd .
Lengo la kikao hicho kilichohudhuriwa na wazabuni wa huduma na bidhaa wa taasisi hiyo kilikuwa ni kuimarisha uhusiano na kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili washitiri hao ili zitatuliwe kwa wakati.
Comments
Post a Comment