JKCI: Kigamboni njooni kupima moyo
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samwel George na mwenzake wa Hospitali ya wilaya Kigamboni Ally Kumbuka wakimsikiliza mwananchi aliyefika katika hospitali ya Kigamboni kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo. Wataalamu wa JKCI na wenzao wa Kigamboni wanafanya kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo jakaya Kikwete (JKCI) Saad Kamtoi akichukuwa taarifa za mwananchi aliyefika katika Hospitali ya wilaya Kigamboni kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo.Wataalamu wa JKCI na wenzao wa Kigamboni wanafanya kambi maalumu ya matibabu ya moyo ya siku tano kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Mwakilishi wa kampuni ya uingizaji na usambazaji wa dawa za binadamu ya Micro Labs Ltd Festus Asenga akimpatia dawa za kupunguza mafuta mwilini mwananchi aliyefika katika Hospitali ya wilaya Kigamboni kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo. Kampuni ya uingizaji na usambazaji wa dawa za binadamu ya Micro Labs Ltd inatoa dawa bila malipo kwa wananchi wanaokutwa na matatizo ya moyo katika kambi hiyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Kigamboni.
Wakazi wa wilaya ya Kigamboni na maeneo ya jirani
wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika Hospitali ya Wilaya hiyo iliyopo
Gezaulole kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Matibabu hayo yanatolewa katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo
ya siku tano inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya wilaya Kigamboni.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa
Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda wakati akizungumza na
waandishi wa habari walioshiriki zoezi hilo la upimaji.
Anna alisema katika kambi hiyo wananchi wanapimwa vipimo
mbalimbali vya moyo vikiwemo vya kuangalia uwiano baina ya urefu na uzito, uwingi
wa sukari kwenye damu, shinikizo la damu, kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography - ECHO) na mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG).
“Ninawaomba wananchi mje kupima afya zenu katika Hospitali
hii ya Kigamboni tutakuwepo hapa hadi siku ya Ijumaa. Wataalamu wetu wanafanya
upimaji wa magonjwa ya moyo, wanatoa huduma ya matibabu pamoja na ushauri wa
matumizi sahihi ya dawa za moyo na jinsi ya kuepukana na magonjwa hayo”,.
“Watu ambao tunawakuta
na matatizo ya moyo yanayohitaji uchunguzi wa kitaalamu na matibabu zaidi tunawapa
rufaa ya kuja JKCI kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi pamoja na kuwapa matibabu ya kibingwa”,
alisema Anna.
Anna alisema huduma hiyo ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi
mahali walipo inajulikana kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach
Services ambapo wananchi wanapata huduma za kibingwa za uchunguzi, ushauri na
matibabu ya moyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Kitabibu Manispaa ya
Kigamboni Dkt. Chemere Sirira aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kuwatuma wataalamu wake katika hospitali hiyo ambao wanashirikiana kwa
pamoja kutoa huduma kwa wananchi.
“Huduma za kumuona daktarin na vipimo vya moyo vikiwemo za ECHO
na ECG zinatolewa bila malipo yoyote yale, wananchi wanalipia huduma ya vipimo
vya maabara pia kuna dawa ambazo zinatolewa bila malipo na kuna dawa ambazo wananchi
wanazilipia kwa gharama naafuu”,.
“Pamoja na wananchi kupata huduma ya matibabu ya kibingwa ya
moyo wataalamu wetu wa afya wa Hospitali
hii wanajengewa uwezo wa kufanya vipimo na kutibu wagonjwa wa moyo hii
itatusaidia baada ya kambi hii nasi tutaweza kutoa huduma hii kwa wagonjwa
wetu”, alisema Dkt. Sirira.
Nao wananchi waliopata matibabu katika kambi hiyo ya matibabu
ya moyo waliishukuru Serikali kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia
kupata matibabu kwa haraka na kirahisi zaidi.
“Wananchi wengi wa vijijini tunachangamoto ya kupata huduma
za matibabu za kibingwa, tunashukuru huduma hii imetufuata hapa Kigamboni,
nimetibiwa, nimepata dawa pamoja na ushauri. Ninawaomba wananchi wenzangu mje
kupima moyo kwani wataamu wapo hapa na wanatoa huduma za matibabu”, alisema Rajabu
Salumu mkazi wa Tungi Kigamboni.
“Nilisikia taarifa ya kuwepo kwa kambi hii ya upimaji wa moyo kwenye vyombo vya
habari nami nikaamua kuja na mwanangu kupima, nimepata huduma nzuri na kwa
haraka ninaiomba Serikali ituletee huduma nyingine za kibingwa zikiwemo za
macho pia wananchi wenzangu mtumie nafasi hii mje kupima moyo”, alisema Mwajuma
Ponza mkazi wa Chanika wilayani Ilala.
Comments
Post a Comment