JKCI yaandaa mpango mkakati wa kwanza wa Utalii Tiba
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akipokea mpango mkakati wa kwanza wa utalii tiba
ulioandaliwa na kamati ya utalii tiba ya Taasisi hiyo kwaajili ya kuwaongoza
kufikia malengo yaliyopangwa na Taasisi hiyo katika kutoa huduma za matibabu ya
moyo kimataifa.
Na JKCI
********************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeandaa mpango mkakati
wake wa kwanza wa utalii tiba, hatua inayolenga kuiweka Tanzania kwenye ramani
ya utoaji wa huduma za afya bora kimataifa na kuvutia wagonjwa kutoka ndani na
nje ya nchi.
Mpango huo uliwasilishwa rasmi na Kamati ya Utalii Tiba ya
taasisi hiyo na kukabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge
ambaye alisema mpango huo utakuwa dira ya utekelezaji wa malengo ya taasisi
katika kukuza huduma za moyo kwa ubora wa juu unaokubalika kimataifa.
“Kupitia mpango huu tunataka kuhakikisha wagonjwa wa ndani na
nje ya nchi wanapata huduma za kitaalamu na zenye viwango vya kimataifa. Ni
mkakati utakaosaidia sio tu kuimarisha afya ya wananchi bali pia kuchangia pato
la taifa kupitia utalii tiba,” alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa mpango huo umejikita katika maeneo kadhaa
ikiwemo kuimarisha miundombinu ya kisasa ya tiba, kuongeza rasilimali watu wenye
ujuzi wa kitaalamu, kuimarisha tafiti za kitabibu, kuboresha mazingira rafiki
ya hospitali pamoja na kuongeza ushirikiano wa kimataifa na taasisi kubwa za
afya.
Kwa mujibu wa Dkt. Kisenge, Tanzania ina nafasi kubwa ya
kunufaika na utalii tiba kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za moyo
barani Afrika na gharama nafuu zinazotolewa na JKCI ukilinganisha na nchi
nyingine.
“Tunataka mtu anayehitaji matibabu ya moyo Afrika Mashariki
na Kati asifikirie kusafiri mbali bali afikirie kuja Tanzania, hususan JKCI,
ambako atapata huduma bora na kwa gharama nafuu zaidi,” aliongeza.
Kwa upande wao wajumbe wa Kamati ya Utalii Tiba walisema
maandalizi ya mpango huu yametokana na utafiti wa kina na mashauriano na wadau
wa sekta ya afya na utalii, ili kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na
fursa hii.
Mpango huu unatarajiwa pia kuchochea ajira, kuongeza mapato
ya kigeni na kukuza sekta ya utalii kwa ujumla, kwani wagonjwa kutoka nje ya
nchi na familia zao watakapofika nchini kupata huduma za tiba, pia watachangia
katika sekta nyingine kama hoteli, usafiri na biashara.
JKCI kwa sasa ni kituo kikuu cha rufaa cha kitaifa cha
matibabu ya magonjwa ya moyo, chenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji mkubwa
wa moyo, upandikizaji vifaa vya moyo na matibabu mengine ya kitaalamu ambayo
awali wananchi walilazimika kuyatafuta nje ya nchi.
Kwa kukamilika kwa mpango huu wa kwanza wa utalii tiba,
taasisi hiyo inatarajia kuongeza zaidi idadi ya wagonjwa wa kimataifa wanaofika
nchini kwa ajili ya huduma, sambamba na kuendelea kutoa huduma bora kwa
Watanzania.
Comments
Post a Comment