Magonjwa ya kinywa yatajwa kuongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo
Daktari wa kinywa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Hospitali ya Dar Group Aitham Mohamed akichunguza kinywa cha mwananchi
aliyejitokeza kufanya uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu ya siku mbili
ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanywa na
Hospitali hiyo katika viwanja vya Mbagala Zakhem vilivyopo Temeke jijini Dar es
Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Helman Nicholaus akipima mapigo ya moyo ya mwananchi
aliyejitokeza kufanya uchunguzi wa afya wakati wa kambi maalumu ya siku mbili
ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services inayofanywa na
Hospitali hiyo katika viwanja vya Mbagala Zakhem vilivyopo Temeke jijini Dar es
Salaam.
Na JKCI
*************************************************************************************************
Magonjwa
ya kinywa kwa watoto yakiwemo ya kuoza kwa meno na mafindofindo
(Tonsillitis) yanaweza kusababisha
magonjwa ya valvu za moyo endapo hayatatibiwa kwa wakati.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Daktari wa Kinywa
na Meno kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group
Aitham Mohamed, wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach
Services inayoendelea katika Viwanja vya Mbagala Zakhem jijini Dar es
Salaam.
Dkt.
Aitham alisema kuna uhusiano mkubwa kati ya matatizo ya meno, kinywa na moyo,
kwani kuharibika kwa meno husababisha kuwepo kwa bakteria ambao wanaweza
kusambaa hadi kushambulia valvu za moyo na hivyo kusababisha magonjwa ya moyo.
“Tumekuwa
tukiishauri jamii kulinda afya ya kinywa kwa kusafisha meno angalau mara mbili
kwa siku. Hatua hii husaidia kuzuia kuharibika kwa meno na magonjwa ya kinywa
yanayoweza kuhatarisha afya ya moyo”,
alisema Dkt. Aitham.
Aliongeza
kuwa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua hupimwa afya ya
kinywa kabla ya upasuaji, ili kuepusha maambukizi yanayoweza kusababishwa na
bakteria baada ya upasuaji.
Kwa
upande wake Daktari wa Upasuaji wa JKCI
- Hospitali ya Dar Group Joyce Mkodo alisema katika kambi hiyo wataalamu
wa upasuaji wameshiriki kutoa huduma kwa watu wenye changamoto za vidonda sugu.
“Tunafanya
kambi hii kama sehemu ya kusherehekea mafanikio ya JKCI katika kipindi cha miaka
10 tangu ianze kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo. Wananchi
wanapopata fursa kama hii wajitokeze kwa wingi, kwani wengi hawachunguzi afya
zao hadi wanapopatwa na matatizo”,
alisema Dkt. Joyce.
Dkt.
Joyce aliongeza kuwa wagonjwa watakaobainika kuwa na matatizo ya kiafya
watapatiwa rufaa kwenda Hospitali ya JKCI Dar Group iliyopo TAZARA kwa
uchunguzi zaidi na matibabu.
Naye Ibrahim Ndube mkazi wa Mbagala alisema amefurahia huduma
hizo akibainisha kuwa ni faraja kubwa kuona taasisi kubwa kama JKCI inawafikia
wananchi wa kipato cha chini.
“Huduma
nilizopata hapa ni nzuri sana. Nimeonana na madaktari wa kinywa, mgongo na
moyo. Nawapongeza kwa huduma bora na elimu nzuri kuhusu afya. Mtaji wa maisha
ni afya, hivyo vijana wenzangu msisite kupima afya zenu”, alisema Ndube.
Kambi
hiyo maalumu ya siku mbili inatoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa
ya moyo, sukari, shinikizo la damu, henia, vidonda vya muda mrefu, uti wa
mgongo, maungio ya mifupa, pamoja na matibabu ya kinywa na meno.
Comments
Post a Comment