Tanzania yapeleka madaktari bingwa Anjouan – Ushirikiano wa Afya waongeza tumaini kwa wananchi
Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete akitoa neno la shukrani kwa Gavana wa kisiwa cha Anjouan katika Muungano wa Visiwa vya Comoro Dkt. Zaidou Youssouf wakati madaktari bingwa kutoka Tanzania walipomtembelea ofisini kwake kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wananchi katika hospitali tatu kubwa zilizopo kisiwani humo.
**********************************************************************************************************************************************************************************************
Serikali ya Tanzania
imepeleka timu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kisiwani Anjouan
vilivyopo Comoro kwa lengo la kuendeleza
ushirikiano wa afya baina ya mataifa hayo mawili na kuhakikisha wananchi wa
visiwa hivyo wanapata huduma za kibingwa bobezi.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya madaktari hao ofisini kwake jana Gavana wa Anjouan katika Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Dkt. Zaidou Youssouf, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwatuma wataalamu wake kwenda kuwasaidia wananchi wanaosumbuliwa na magonjwa yanayohitaji matibabu ya ubingwa bobezi.
Alisema kisiwa cha Anjouan kina idadi kubwa ya
watu kuliko visiwa vingine vya Comoro na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi
kupima afya na kupata tiba stahiki.
“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
kwa kutuletea wataalamu hawa nchini kwetu. Hii ni ishara ya ushirikiano mzuri
wa kidiplomasia uliopo kati ya nchi hizi mbili”, alisema Mhe. Gavana Dkt. Youssouf.
Aliongeza kuwa ingawa wananchi wengi wa
Anjouan wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini, wamewapokea wataalamu
wa afya wa Tanzania kwa mikono miwili na wameahidi kuwapa ushirikiano wa
kutosha.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu alishukuru kwa
mapokezi mazuri waliyoyapata na kusema kuwa mwaka jana wataalamu kutoka
Tanzania walifanya kambi kubwa ya uchunguzi na matibabu katika kisiwa cha Ngazidja
kwa kutoa huduma
za matibabu ya kibingwa saba, ambapo jumla ya watu 2,770 walihudumiwa.
“Mwaka huu kambi ni kubwa zaidi. Huduma za
kibingwa 17 zitatolewa katika
hospitali kuu tatu zilizopo kisiwani Anjouan. Aidha, Bohari ya Dawa Tanzania
(MSD) imejumuishwa moja kwa moja na imekuja na dawa ambazo zitatolewa kwa
wagonjwa wote. Dawa zitakazobaki zitaachwa kwenye hospitali ili ziendelee
kutumika”, alisema Balozi Yakubu.
Aliongeza kuwa hadi sasa zaidi ya watu 1,000 wamejiandikisha kupokea huduma
hizo ambazo pia zitahusisha elimu kwa umma kuhusu magonjwa yasiyoambukiza,
katika maeneo matatu maalumu yaliyotengwa kwa wananchi.
Mhe. Balozi Yakubu alisema siku ya jana timu
ya wataalamu ilitembelea hospitali kubwa tatu zitakazotumika kutoa huduma
ambazo ni Hombo, Pomoni na Bambao,
kwaajili ya kuona vifaa vilivyopo na sehemu za kutolea huduma ya matibabu, huku
wataalamu wengine wakitarajiwa kuwasili leo jioni.
Akizungumza kwa niaba ya wataalamu wenzake wa
fya daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Salehe Mwinchete alisema
timu hiyo iko tayari kutoa huduma bora kwa wananchi wa Anjouan kwa kutumia
ujuzi waliobarikiwa na Mungu, huku akiahidi kutoa huduma zenye weledi na
upendo.
Wataalamu wanaoshiriki katika kambi hiyo wanatoka katika taasisi na hospitali kubwa sita za Tanzania ambazo ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Taasisi ya Saratani Ocean Road pamoja na Bohari ya Dawa Tanzania (MSD).
.jpg)

.jpg)
Comments
Post a Comment