JKCI na SACH wafanya upasuaji wa moyo kwa watoto 29 wa nchini Zambia
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Rosemarry Mpella akimsikiliza mtoto aliyelazwa katika chumba cha uangalizi
maalumu (ICU) katika Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) baada ya kufanyiwa
upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya siku sita ya upasuaji wa moyo iliyokuwa
ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa NHH na Shirika la
Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel. Jumla ya watoto 29 wamefanyiwa upasuaji wa
moyo.
Wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) ya nchini Tanzania Dkt. Stella Mongella, Shirika la Okoa
Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel Dkt. Assa Sagi na Hospitali ya Taifa ya
Moyo Zambia (NHH) ya nchini Zambia Dkt. Evance Mulendele wakifanya upasuaji wa
bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab kuziba tundu lililopo kwenye
moyo wa mtoto wakati wa kambi maalumu ya siku sita iliyomalizika hivi karibuni
katika Hospitali ya NHH. Jumla ya watoto 29 wamefanyiwa upasuaji wa moyo.
Mama wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo Magreth Mwanza
akimjulia hali mtoto wake wakati wa kambi ya maalumu ya upasuaji wa moyo ya
siku sita iliyokuwa ikifanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa upasuaji wa
moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ya nchini Tanzania,
Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel na Hospitali ya Taifa ya
Moyo Zambia (NHH) ya nchini Zambia. Jumla ya watoto 29 wamefanyiwa upasuaji wa
moyo.
Na JKCI
*************************************************************************************************
Watoto 29 wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo wa nchini
Zambia wamefanyiwa upasuaji wa moyo na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa
watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ya nchini Tanzania na
Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (SACH) la nchini Israel.
Upasuaji huo uliomalizika hivi karibuni mjini Lusaka nchini
Zambia umefanyika wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto ya
siku sita katika Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) na kutoa mafunzo kwa
wataalamu wa hospitali hiyo.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo balozi wa
Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule aliwapongeza
wataalamu wa JKCI kwa kazi nzuri waliyoifaya na kuiheshimisha nchi ya Tanzania
kwa kuweza kUvuka mipaka na kutoa huduma za kibingwa bobezi za matibabu ya moyo
kwa watoto wa nchini Zambia.
Mhe. Balozi Mkingule alisema wakati wa harakati za uhuru katika
nchi za Afrika wahasisi walipambana kuhakikisha ukombozi wa bara la Afrika
unapatika, sasa Tanzania ipo kwenye harakati ya vita vya kiuchumi kuhakikisha
inazisaidia nchi za Afrika kupata ujuzi hivyo kuwa na Afrika yenye afya na
uwezo wa kutoa huduma bingwa bobezi kwa jamii zao.
“Nazidi kuwaomba muendelee kushirikiana na Hospitali ya Taifa
ya Moyo ya Zambia (NHH) kwa kuwapa mafunzo na msaada pale mnapoweza, ofisi ya
ubalozi itafuatilia utekelezaji wa mkabata mliosaini nao ili yale yaliyoeleza katika
mkataba muweze kuyafanyia kazi”, alisema Mhe. Balozi Mkingule
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongela alisema
watoto 10 wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na watoto 19 wamefanyiwa
upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo kwenye paja kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Dkt. Stella alisema wototo wote waliofanyiwa upasuaji katika
kambi hiyo wanaendelea vizuri na wengi wao baada ya upasuaji huo wamepona
kabisa magonjwa ya moyo.
“Jana baada ya kuhitimisha kambi watoto 9 waliofanyiwa
upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo kwenye paja tuliwaruhusu kurudi nyumbani
baada ya hali zao kuendelea vizuri”, alisema Dkt. Stella.
Dkt. Stella alisema kupitia kambi hiyo wataalamu kutoka NHH
wameweza kujifunza mambo mengi ikiwemo kufanya upasuaji mgumu wa moyo,
kuhudumia wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo waliopo katika chumba cha
uangalizi maalumu (ICU) na kuwatambua watoto wenye magonjwa ya moyo kwa wakati.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
kutoka Hospitali ya Taifa ya Moyo Zambia (NHH) Evance Mulendele alisema mafunzo
waliyoyapata kupitia kambi hiyo yanaenda kuwaongezea ujuzi wataalamu wa
Hospitali ya hiyo na kusaidia kupunguza idadi ya watoto wanaohitaji upasuaji wa
moyo.
Dkt. Mulendele alisema idadi ya watoto wenye magonjwa ya moyo
inazidi kuongezeka na uhitaji wa matibabu yakiwemo ya upasuaji wa moyo yameongezeka.
“Kupitia kambi hii tumeweza kujifunza mambo mengi, ninaamini
wataalamu wetu katika kipindi cha miaka mitano sita ijayo watakuwa kama hawa wa
JKCI walivyo, alisema Dkt. Mulendele.
Naye mama wa mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi
hiyo Margareth Mwanza aliwashukuru wataalamu wote walioshiriki kumfanyia
upasuaji wa moyo mtoto wake na kuokoa maisha yake.
Margareth alisema awali alipoteza tumaini kutokana na hali ya
mwanae ilivyokuwa ikibadilia kila kukicha ila baada ya mwanae kufanyiwa
upasuaji hali yake imekaa vizuri.
“Nina umri mdogo na nimekutana na changamoto kubwa za
magonjwa ya moyo kwa mwanangu, madaktari waliniambia alikuwa na tundu kwenye
moyo na mishipa yake ya damu ilikuwa imeziba, nawashukuru sana mmemfanyia
upasuaji mwanangu na sasa huyu hapa anaendelea vizuri”, alisema Margareth
Comments
Post a Comment