Viongozi wa JKCI Hospital ya Dar Group wajengewa uwezo wa kudhibiti vihatarishi vya kiutendaji

.jpg)
Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospital ya Dar Group wakimsikiza CPA. Cosmas Mbogela wakati akitoa mafunzo ya jinsi ya kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi wa hospitali hiyo yanayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospital ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu na Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Ununuzi wa hospitali hiyo Iddi Lemmah wakimsikiza CPA. Cosmas Mbogela wakati akitoa mafunzo ya jinsi ya kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi wa hospitali hiyo yanayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.
**************************************************************************************************************************************************************************************
Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group wanahudhuria mafunzo ya kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi wa hospitali hiyo, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa mpango mkakati unaolenga kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza
kuhusu mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika jijini Dar es Salaam Mkurugenzi
wa JKCI Hospitali ya Dar Group Dkt.
Tulizo Shemu alisema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo
kuhakikisha maendeleo ya kiutendaji hayaathiriwi na changamoto zinazoweza
kuzuilika kupitia mipango thabiti.
Dkt. Shemu ambaye
pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya
damu ya moyo alisema mafunzo hayo
yataisaidia hospitali hiyo kuendelea kutoa huduma bora salama na endelevu kwa
wananchi.
“Leo tumejifunza
namna ya kubaini vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika mazingira yetu ya
kazi iwe ni katika utendaji wa kila siku au katika hatua za maendeleo ya
taasisi. Mafunzo haya yatasaidia kuhakikisha tunabaki kwenye mstari wa
mafanikio na kufikia malengo tuliyojiwekea”, alisema Dkt. Shemu.
Aliongeza kuwa
JKCI Hospitali ya Dar Group inahudumia wastani wa wagonjwa 500 kwa siku, na
katika kipindi cha miaka mitatu imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma
bora za moyo na magonjwa mengine kwa kuzingatia miongozo ya kisera na bajeti ya
mwaka ambayo inaelekeza utekelezaji wa shughuli.
“Azma yetu ni
kuhakikisha huduma za afya zinamfikia kila mtanzania kama alivyoelekeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumejipanga
kutoa huduma za kiwango cha juu hapa nchini na kuvuka mipaka ya nchi”, alisisitiza
Dkt. Shemu.
Kwa upande wake Mkuu
wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa hospitali hiyo CPA. Ashura Ally alisema uandaaji wa rejesta ya vihatarishi ni
takwa la Wizara ya Afya ambapo kila taasisi ya umma inapaswa kuandaa rejesta
hiyo ili kuimarisha utendaji wake.
“Tumepata mafunzo
ya jinsi ya kutambua viashiria vya vihatarishi, namna ya kuviainisha,
kuvipangia mikakati ya kudhibiti na kuviingiza kwenye mipango ya bajeti. Hii
itatusaidia kuhakikisha taasisi haikwami katika utendaji wa kila siku bali
inaendelea kufanikisha malengo iliyojiwekea”, alisema CPA. Ashura.
Naye Mkuu wa
Kitengo cha Ugavi na Ununuzi wa JKCI hospitali ya
Dar Group Iddi Lemmah alisema mafunzo
hayo ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano wa
taasisi hiyo kwani yamewasaidia kuelewa namna bora ya kuendesha taasisi kwa
ufanisi.
“Tumejifunza
namna ya kuainisha vihatarishi vinavyoweza kuchelewesha au kuzuia utekelezaji
wa malengo ya taasisi pamoja na kuweka mikakati ya kuvithibiti na kuandaa
bajeti ya kukabiliana navyo”, alisema Lemmah.
JKCI Hospitali ya Dar Group inatoa huduma za matibabu ya moyo, kinywa na meno, matibabu ya magonjwa ya kuambukiza kama malaria, huduma za dharura, kliniki ya wanawake na wajawazito, kliniki ya macho, pua, masikio na koo, kliniki ya mfumo wa mkojo, matibabu ya magonjwa ya tumbo na ini, figo, huduma za baba, mama na mtoto (RCH), upasuaji mkubwa na mdogo, upimaji wa VVU na ushauri, fiziotherapia (mazoezi tiba), huduma za maabara na gari la wagonjwa.

Comments
Post a Comment