Dkt. Peter Kisenge awasaidia madaktari wa Anjouan kuboresha uchunguzi na matibabu ya Moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwafundisha madaktari wa hospitali ya Hombo iliyopo Kisiwa cha Anjoan namna ya kupata mwonekano bora wa moyo wakati wa kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi ili kuboresha usahihi wa matokeo. Mfunzo hayo ameyatoa katika kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania inayofanyika kisiwani humo.
Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu akizungumza na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbi (MNH) Vincent Tarimo wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka Tanzania wanaotoa huduma za matibabu katika hospitali kubwa tatu zilizopo kisiwani Anjoan.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimwelekeza daktari wa Hospitali ya Hombo iliyopo kisiwani Anjouan Misdjal Ali dawa nzuri za kuwatibu wagonjwa wenye matatizo ya shambulio la moyo wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoa Tanzania inayofanyika katika Hospitali hiyo. Kulia ni Daktari kutoka JKCI Janeth Mmari.
Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu akizungumza na daktari
bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbi (MNH) Vincent Tarimo
wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali kutoka
Tanzania wanaotoa huduma za matibabu katika hospitali kubwa tatu zilizopo
kisiwani Anjoan.
Madaktari wa Hospitali ya Hombo iliyopo katika Kisiwa cha Anjouan nchini Comoro wamepatiwa mafunzo maalumu ya jinsi ya kufanya vipimo vya moyo kwa ufanisi na kutoa matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo makubwa ya moyo.
Mafunzo hayo yametolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba
pamoja na kupandikiza vifaa visaidizi vya moyo.
Dkt. Kisenge alisema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uwezo wa
madaktari wa ndani kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, kuyatambua
mapema na kuyatibu kwa ufanisi badala ya wagonjwa kusafiri hadi nchi nyingine
kufuata huduma hizo.
Alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha huduma za moyo
katika Hospitali ya Hombo kwa kuhakikisha madaktari wake wanafahamu matumizi ya
mashine za uchunguziwa moyo kama Echocardiogram
(Echo) na Electrocardiogram (ECG) pamoja na namna ya kusoma
majibu yake kwa usahihi.
“Tunataka madaktari wa Comoro waweze kutoa huduma bora za moyo
katika vituo vyao, bila kulazimika kutegemea wataalamu kutoka nje mara kwa
mara. Hii itapunguza gharama, kuokoa muda na kuboresha afya za wananchi wengi
zaidi”, alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wao, baadhi ya madaktari wa Hospitali ya Hombo walisema
wamefurahishwa kufanya kazi na Dkt. Kisenge kwani kupitia mafunzo hayo
wamejifunza mambo mapya mengi, ikiwemo njia sahihi za kufanya vipimo vya Echo,
kusoma matokeo yake na kutoa dawa zinazofaa kwa wagonjwa wa moyo kulingana na
hali zao.
“Tumefurahi sana kushirikiana na Dkt. Kisenge. Ameongeza uelewa
wetu wa jinsi ya kuchunguza wagonjwa wa moyo kwa undani na namna ya kuwasaidia wagonjwa
kwa kutumia dawa sahihi. Tunamshukuru yeye na timu ya JKCI kwa kutuletea
maarifa haya muhimu”, alisema Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Daniel
Oiridi.
Naye Dkt. Misdjal Ali mmoja wa madaktari waliopatiwa
mafunzo hayo, alisema amejifunza mambo mengi ya kitaalamu ikiwemo jinsi yakupata
mwonekano bora wa moyo wakati wa kufanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography)
ili kuboresha usahihi wa matokeo
“Kupitia
mafunzo ya Dkt. Kisenge nimeongeza uwezo wangu wa kufanya vipimo vya moyo kwa
ufanisi zaidi. Sasa naweza kubaini matatizo ya moyo mapema na kusaidia wagonjwa
kupata tiba sahihi kwa wakati”, alisema Dkt. Misdjal Ali.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa mafunzo kama hayo wakati wa kambi maalumu za matibabu ya magonjwa ya moyo inayozifanya ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuboresha huduma za afya na kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani katika kutibu magonjwa ya moyo.

Comments
Post a Comment