Moyo Wangu, Afya Yangu: JKCI na HTAF wazindua shindano la insha kwa wanafunzi
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa uzinduzi wa shindano la uandishi wa insha Shule za Sekondari leo jijini Dar es Salaam. Shindano hilo linafanywa na JKCI kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) kufikisha elimu ya magonjwa ya moyo kwa wanafunzi.
Kamishina wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa akielezea umuhimu wa insha mashuleni wakati wa uzinduzi wa shindano la uandishi wa insha Shule za Sekondari leo jijini Dar es Salaam. Shindano hilo linafanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) kufikisha elimu ya magonjwa ya moyo kwa wanafunzi.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Heart Team
Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa shindano la uandishi wa
insha Shule za Sekondari
leo jijini Dar es Salaam. Shindano hilo linafanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na HTAF kufikisha elimu ya magonjwa ya moyo kwa
wanafunzi.
Na JKCI
******************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
Shirika lisilo la Kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) wameanzisha
shindano la insha kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini kuwaelimisha
kuhusu magonjwa ya moyo.
Shindano hilo yenye kauli mbiu isemayo “Moyo wangu afya
yangu” ni sehemu ya mradi wa miaka mitatu wa Taasisi hiyo unaolenga kuongeza
uelewa na kukuza kinga ya magonjwa yasiyoambukiza hususani magonjwa ya moyo na
mishipa ya damu kwa watoto wenye umri wa kwenda shule.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa shindano la uandishi wa
insha Shule za Sekondari kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Carolyne Nombo Kamishina wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
kutoka Wizara ya Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa alisema mradi huo unatarajia
kutoa elimu na kuwafikia watoto wa shule za sekondari kwa kutumia mbinu
mbalimbali kuhakikisha kuwa utoaji wa elimu unakuwa endelevu na kuwafikia
wanafunzi wengi nchini
“Kupitia mradi huo kutakuwa na vilabu vya afya mashuleni,
vipeperushi vinavyotoa elimu ya magonjwa ya moyo, vijarida, mabango, mashindano
ya uandishi wa insha, midahalo, kampeni za afya na usafi wa mazingira”, alisema
Dkt. Mtahabwa
Dkt. Mtahabwa alisema mbinu zote hizo zitatumika kama
majukwaa ya kuwaelimisha na kuwashirikisha wanafunzi kwa kuwajengea uwezo
waweze kufahamu umuhimu wa afya na namna ya kujikinga na magongwa ya moyo.
“Rasilimali watoto ni rasilimali yenye thamani kubwa kuliko
rasilimali nyingine yeyote na haina mbadala wake, juhudu za watanzania zielekezwe
katika kumlinda mtoto kuhakikisha yuko salama na katika mazingira rafiki ili
aweze kufikia ustawi tarajali”, alisema Dkt. Mutahabwa
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema jamii sasa imekuwa na mtindo wa
maisha ambao si mzuri kwa watoto kwa kuwapa vyakula ambavyo havizingatii mtindo
bora na ulaji wenye lishe bora hivyo JKCI na HTAF zikaona ili kuzuia magonjwa
ya moyo kwa watoto waanzishe mradi huo kuwapa elimu ya kutosha watoto waweze
kupenda afya zao.
“Kama mtoto wako hali lishe bora atakavyokuwa mkubwa atakuwa
katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo, JKCI tunasherehekea mafanikio ya
miaka 10 sio kwa kutoa huduma kwa wagonjwa wengi bali tunataka pia kuongeza
jitihada katika kuilinda jamii isipate magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema shindao la isha linabeba dhamana ya
kukuza uwezo wa wanafunzi katika kuelewa na kueleza masuala ya afya ya moyo kwa
maandishi ili waweze kuielimisha jamii, kugundua na kukuza vipaji vya uandishi
miongoni mwao na kuwafanya wanafunzi kuwa mabalozi wa afya katika taifa.
Naye Mtendaji Mkuu wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Heart
Team Africa Foundation (HTAF) Dkt. Naiz Majani alisema JKCI na HTAF wanataka
kupeleka elimu ya moyo mashuleni wakiwa na nia ya kusaidia watoto ili pale
wanapokuwa wasikumbane na changamoto ya magonjwa ya moyo.
“Tumegundua kuwa magonjwa mengi ya moyo ambayo watu wazima
wanapata chanzo chake uanzia utotoni, hivyo tukaona ni muhimu kupeleka elimu
hii ya afya ya moyo mashuleni kuwawezesha watoto wapate elimu ya afya ya moyo”,
alisema Dkt. Naiz
Washindi wa shindalo hilo linaloanza rasmi tarehe 8 Oktoba
hadi 1 Novemba 2025 watapewa zawadi ambapo mshindi wa kwanza atapata shilingi
milioni 3 na laptop, mshindi wa pili atapata shilingi milioni 2 na laptop,
mshindi wa tatu atapata shilingi milioni 1 na tablet, mshindi wa nne atapata
shilingi laki 5 na cheti na mshindi wa tano atapata shilingi laki 3 na cheti.
Sambamba na zawadi hizo washindi hao pia watapewa nafasi ya
kujengewa uwezo wa kushirikiana katika miradi ya elimu ya afya ya moyo ili
kupitia kwao ujumbe kuhusu kinga ya afya ya moyo uweze kwenda kwa kasi na
kuifikia jamii yote.
Comments
Post a Comment