Watu 330 wafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani
******************************************************************************************************************
Jumla ya watu 330 kutoka Dar es
Salaam na mikoa jirani wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo
katika maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani.
Matibabu hayo, yaliyoendelea kwa
siku tatu, yamefanyika katika viwanja vya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group iliyopo Tazara, wilaya ya Temeke.
Akizungumza na waandishi wa
habari, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo yanayohusiana na kazi, kutoka JKCI,
Dkt. Elias Birago, alisema wananchi waliojitokeza walifanyiwa vipimo mbalimbali
ikiwemo kipimo cha sukari kwenye damu, ECG (Electrocardiogram) kuangalia mfumo
wa umeme wa moyo, ECHO (Echocardiogram) kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi,
kipimo cha shinikizo la damu, vipimo vya maabara, pamoja na ushauri wa lishe
bora.
“Wananchi wengi waliofanyiwa
uchunguzi walibainika kuwa na shinikizo la juu la damu. Sababu kuu ni mtindo wa
maisha na kutozingatia mlo bora. Tumetoa rufaa kwa watu 259 kuudhuria kliniki
zetu kwa vipimo zaidi. Pia, tumeona vijana wengi wamejitokeza kujichunguza,
tunawaomba waendelee kulinda afya zao”, alisema Dkt. Birago.
Aidha, watu 96 waliweza kuonana
na mtaalamu wa lishe kwa ajili ya ushauri, ambapo asilimia 77 walibainika kuwa
na uzito uliokithiri unaoweza kuathiri utendaji wa moyo.
JKCI imesisitiza kuendeleza
huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi, ili kuwapa fursa ya
kupima afya zao, kwani wengi hawana tabia ya kufanya hivyo mara kwa mara.
Comments
Post a Comment