Watu 484 wafanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo maonesho ya madini Geita
Baadhi ya wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifurahia baada ya kupokea tuzo ya mshindi wa pili kwa taasisi zinazotoa huduma ya afya wakati wa kufunga maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini yaliyomalizika hivi karibuni mkoani Geita.
Daktari wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Aisha Ally Said akimsikiliza mkazi wa Geita aliyefika
katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan kupatiwa huduma za
uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia
ya madini yaliyomalizika hivi karibuni mkoani Geita.
Wananchi wa mkoa wa Geita wakisubiri kupata huduma za
uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa na wataalamu wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia
ya madini yaliyomalizika hivi karibuni Mkoani Geita.
******************************************************************************************************
Watu 484 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa
ya moyo wakati wa maonesho ya nane ya kitaifa ya madini yaliyokuwa yanafanyika katika
viwanja vya maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
Hayo yamesemwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Henry Mayala wakati akizungumza na
waandishi wa Habari kuhusu huduma walizokuwa wanazitoa kwenye maonesho hayo.
Dkt. Mayala alisema kati ya watu 484 waliofanyiwa uchunguzi
na matibabu ya moyo 473 walikuwa watu wazima na 11 walikuwa watoto ambapo wengi
wao wamekutwa na shinikizo la juu la damu, kisukari na uzito uliopitiliza.
“Wengi walikuwa hawajui kama wana haya matatizo kwahiyo
kitendo cha kupima afya kimeweza kuwasaidia kupata matibabu mapema na elimu
itakayowasaidia kujikinga na magonjwa hayo”, alisema Dkt. Mayala.
Dkt. Mayala alitoa wito kwa wananchi waweze kujitokeza kwa
wingi pale wanaposikia taasisi hiyo ikitoa huduma za upimaji na matibabu
ya moyo kwa wananchi kwa kuwafuata mahali walipo ili kutibiwa mapema.
Nao wananchi waliopata huduma ya uchunguzi na matibabu ya
moyo katika maonesho hayo walishukuru kwa huduma walizozipata na kusema kuwa
zimwewasaidia kufahamu hali zao za afya na kupata matibabu.
“Huduma ipo vizuri ukifika unapimwa kwa dakika chache tu na
huchelewi na vipimo vyao ni bure na madaktari wanatupa ushauri mzuri wa kujua
afya zetu,” alisema Dayness Lucas mkazi wa Fadhili Bucha Geita.
“Nimepimwa presha na kisukari bure na nimepewa ushauri huu ni
msaada mkubwa kwa kuwa vipimo hivi ni vya gharama kubwa lakini hapa tumepata
bure,” alisema Neema Robin mkazi wa Geita.
“Kwa mfano huu upimaji wa moyo kikawaida ilikuwa kupata
huduma yao ni mpaka uende Dar es Salaam lakini sahivi tunapata hapa karibu,”
alisema Neema Robin mkazi wa Geita.
Katika maonesho hayo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
ilishika nafasi ya mshindi wa pili katika kundi la taasisi inayotoa huduma
ya afya.
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
Comments
Post a Comment