Rais Samia apongezwa kwa kugusa mioyo ya wananchi wa Anjouan
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi zawadi kutoka taasisi hiyo Gavana wa Anjouan katika Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Dkt. Zaidou Youssouf mara baada ya kufanyika kwa sherehe ya ufunguzi wa kambi maalumu ya madaktari bingwa kutoka Tanzania wanaotoa huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa kisiwa hicho. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimweleza Gavana wa kisiwa cha Anjouan katika Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Dkt. Zaidou Youssouf Mhe. Dkt. Zaidou Youssouf huduma zinazotolewa na taasisi hiyo wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanywa na madaktari bingwa kutoka Tanzania kwa wananchi wa kisiwa hicho.
Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu akizungumza na viongozi wa kisiwani cha Anjouan wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanywa na madaktari bingwa kutoka Tanzania kwa wananchi wa kisiwa cha hicho.
Gavana wa Anjouan Mhe. Dkt. Zaidou Youssouf ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Comoro Mhe. Azali Assoumani kwa ushirikiano wao wa kipekee ulioiwezesha timu ya wataalamu wa afya kutoka Tanzania kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa kisiwa hicho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi maalumu ya matibabu ya kibingwa itakayofanyika
katika hospitali tatu kubwa za Anjouan Dkt. Youssouf alisema wananchi wa kisiwa
hicho wanamchukulia Rais Samia kama Mama
yao kutokana na mchango wake mkubwa
katika kuboresha afya za wananchi wa Comoro.
“Mama Samia ni mfano wa kuigwa. Siyo tu
anapambania maendeleo ya Watanzania, bali pia ya nchi nyingine za Afrika
ikiwemo Comoro. Leo tumeshuhudia kwa macho yetu jinsi alivyotuma madaktari wake
kuja kuokoa maisha ya wanacomoro wanaokabiliwa na magonjwa mbalimbali”, alisema
Dkt. Youssouf.
Aliongeza kuwa serikali yake itaweka utaratibu maalum wa ushirikiano wa kudumu
na hospitali za Tanzania, ili wagonjwa watakaohitaji rufaa waweze kupata
matibabu nchini humo kwa urahisi zaidi.
“Tutaanza pia kutuma madaktari wetu kwenda
Tanzania kwa mafunzo ya kitaalamu na wagonjwa wetu waanze kutumia mfumo wa miadi ya mtandaoni ili wagonjwa
kutoka Comoro waweze kuonana na madaktari wa Tanzania bila usumbufu”, aliongeza
Gavana huyo.
Aidha, Dkt. Youssouf aliitumia nafasi hiyo
kumtakia Mhe. Rais Samia mafanikio katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea
Tanzania, akisema wananchi wa Anjouan wanamuombea ashinde ili aendelee na kazi
yake nzuri ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu aliwapongeza
madaktari wa Tanzania kwa kutekeleza maelekezo
ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa wakati wa ziara yake nchini Comoro
alipokutana na wananchi, ambapo alisisitiza umuhimu wa kupeleka huduma
za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa kisiwa hicho kabla ya mwaka huu kuisha.
Naye Waziri wa Afya wa Comoro Mhe. Ahamadi Sidi
Nahouda alisema kambi hiyo ni ishara ya undugu wa kweli kati ya Tanzania
na Comoro, akibainisha kuwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 50 tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1975,
kwa kisiwa cha Anjouan kuwa na kambi kubwa ya aina hiyo.
“Tuna zaidi ya wataalamu 50 waliowasili hapa.
Hii ni historia mpya kwa taifa letu, tunawashukuru sana kwa moyo wa kujitolea,”
alisema Mhe. Nahouda.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Utalii Tiba Taifa
ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt.
Peter Kisenge, alisema mwaka jana katika kambi kama hiyo iliyofanyika
Ngazidja zaidi ya wagonjwa 2,700 walihudumiwa, baadhi yao walipelekwa Tanzania kufanyiwa
upasuaji na wengine wamepona kabisa.
Dkt. Kisenge aliongeza katika kambi hiyo
huduma zinatolewa bila malipo huku Bohari
ya Dawa Tanzania (MSD) ikiwa imechangia dawa zenye thamani ya Euro 20,000 zitakazotolewa kwa wagonjwa.
“Tumekuja na vifaa tiba vya kisasa zikiwemo
mashine za uchunguzi wa moyo na saratani. Mbali na matibabu, wananchi pia watapewa
elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza. Hadi sasa zaidi ya watu 2,500
wamejiandikisha kupata huduma”, alisema Dkt. Kisenge.
Ushirikiano huu kati ya Tanzania na Comoro ni ushahidi tosha kuwa Afrika inaweza kujitibu yenyewe kupitia ubunifu, umoja na dhamira ya pamoja ya kulinda uhai wa wananchi wake.


Comments
Post a Comment