China kutumia shilingi bilioni 112 kujenga Jengo jipya la JKCI Mloganzila

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpatia zawadi mhandisi kutoka Jamhuri ya Watu wa China Zhang Ziying wakati wa kikao na ujumbe wa wahandisi kutoka China kujadili mradi wa ujenzi wa jengo jipya la JKCI litakalojengwa katika eneo la mloganzila jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akielezea mafanikio ya Taasisi hiyo wakati wa kikao na ujumbe wa wahandisi kutoka Jamhuri ya Watu wa China kujadili mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) litakalojengwa katika eneo la mloganzila jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi kutoka Ubalozi wa China Nchini Tanzania Yang Zeyu akizungumza wakati wa kikao na Ujumbe wa wahandisi kutoka nchini China kujadili mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) litakalojengwa katika eneo la mloganzila jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoka Jamhuri ya Watu wa China Yang Ling akielezea mradi huo wakati wa kikao na viongozi wa JKCI leo kujadili mradi huo utakaojengwa katika eneo la mloganzila jijini Dar es Salaam.


Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na ujumbe wa wahandisi kutoka Jamhuri ya Watu wa China wakifuatilia mada zilizokuwa zinaendelea katika kikao cha kujadili mradi wa ujenzi wa jengo jipya la JKCI litakalojengwa katika eneo la mloganzila jijini Dar es Salaam.

Na JKCI

*************************************************************************************************

Serikali ya Watu wa China kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya kikwete (JKCI) kujenga jengo lenye thamani ya shilingi bilioni 112 katika eneo la Mloganzila kwaajili ya kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto.

Jengo hilo linalotarajiwa kuhudumia takribani watoto 900 ni sehemu ya malengo ya kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo kwa kuboresha upatikanaji wa huduma na kupunguza foleni ya watoto wanaohitaji huduma za upasuaji wa moyo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya wahandisi kutoka Jamhuri ya Watu wa China Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kwa sasa Taasisi hiyo ina uwezo wa kuhudumia watoto 400 wanaohitaji upasuaji wa moyo hivyo uhitaji wa nafasi kwaajili ya kutoa huduma bado unahitajika.

“Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alikutana na Rais wa China Xi Jiping wakakubaliana kujenga jengo jipya la JKCI ambalo litagharimu kiasi cha shilingi bilioni 112, hatua hii inatokana na ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa na Taasisi yetu”, alisema Dkt. Kisenge 

Dkt. Kisenge alisema jengo hilo litatoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za maabara, chumba maalumu cha upasuaji wa moyo (Theater), na Cathlab kwaajili ya upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo.

Aidha Dkt. Kisenge alibainisha kuwa kwa sasa JKCI inapokea watoto zaidi 16000 kwa mwaka ambao wanahitaji uchunguzi, matibabu na upasuaji wa moyo kwa haraka hivyo ni muhimu kupata jengo jingine litakaloweza kusaidia matibabu hayo na kupunguza msongamano uliopo.

“Tunatarajia jengo hilo linaloanza kujengwa kuanzia mwezi ujao litapunguza idadi ya vifo vya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaochelewa kupata huduma ya upasuaji hivyo kuokoa maisha yao”, aliasema Dkt. Kisenge

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Ubalozi wa China Nchini Tanzania Yang Zeyu alisema urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na China umewezesha ushirikiano katika kujenga jengo hilo la matibabu ya moyo kwa watoto ili kuwasaidia watoto wengi zaidi kupata matibabu kwa wakati. 

“Ushirikiano katika sekta ya afya kati ya China na Tanzania ni wa miaka mingi, tumekuwa tukileta watalamu wetu ili waweze kuongeza nguvu ya kuwahudumia wagonjwa hapa Tanzania, mradi huu utaanza haraka iwezekanavyo ili watoto wa Tanzania waweze kupata huduma za haraka na kupunguza muda wa kusubiria huduma”, alisema Zeyu.

Naye Mkuu wa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoka Jamhuri ya Watu wa China Yang Ling alisema Serikali ya China imedhamiria kushirikiana kimkakati na Tanzania katika sekta ya afya kwa kuleta wataalamu na kuimarisha miundombinu pamoja na vifaa tiba.

“Jengo tutakalolijenga litakuwa ni jengo la kisasa, na kuweka miundombinu ya kutoa huduma zote katika jengo hilo ili watoto watakapofikishwa hapo waweze kupata huduma zote”, alisema Yang.

 

Comments

Popular posts from this blog

Kutoka miaka 22 hadi kustaafu: Safari ya Lemmah yatoa somo kwa Watumishi wa Umma

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi