20 watibiwa mfumo wa umeme wa moyo
Wagonjwa 20 wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo wamefanyiwa
upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab katika kambi maalum
iliyofanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani.
Kambi hiyo ya siku tano iliyomalizika leo ililenga
kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, kuwasaidia
wataalam wa afya ambao wapo masomoni kujifunza zaidi na kuongeza wigo wa
wataalam wa afya.
Akizungumzia kambi hiyo Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na
mfumo wa umeme wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye
alisema wagonjwa hao 20 waliofanyiwa upasuaji katika kambi hiyo
walipaswa kulipa sio chini ya shilingi milioni 500, lakini kupitia wenzao wa
Shirika la madaktari Afrika baadhi ya wagonjwa wamepata msamaha hivyo
kutogharamia matibabu yao.
Wagonjwa tuliowafanyia upasuaji wapo ambao mapigo yao ya moyo
yalikuwa yakienda chini sana (Heart block) na wengine mapigo yao ya moyo
yalikuwa yanaenda haraka sana”, alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alisema magonjwa yanayohusisha mfumo wa umeme wa
moyo mara nyingi huwa na sababu mbalimbali zinazopelekea hitilafu ya utengenezaji
wa mapigo ya moyo ikiwemo kuzaliwa na tatizo hilo ama kupata kutokana na kuwa
na magonjwa mengine kama shinikizo la juu la damu, moyo kutanuka na kuwa na
shambulio la moyo (heart attack).
“Mgonjwa anapopata tatizo la mapigo ya moyo kwenda juu au kuwa
chini anakuwa katika hali ya hatari hivyo anaweza kufariki ghafla ama
kuusababishia moyo kushindwa kufanya kazi”, alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande wake Daktari kutoka Shirika la Madaktari Afrika la
nchini Marekani Nitish Badhwar alisema JKCI ni moja ya Hospitali iliyowekezwa
vifaa vya kisasa vya kuhudumia wagonjwa wa moyo hivyo wagonjwa wa Tanzania
waitumie Hospitali hiyo vizuri kwani hakuna haja kufuata tena huduma za
matibabu ya moyo nje ya nchi.
Dkt. Nitish alisema kutokana na vifaa vya matibabu ya moyo
kuwa na gharama kubwa shirika la Madaktari Afrika liliamua kutuma vifaa ili
kuweza kuwasaidia wagonjwa ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu ikiwa ni
sehemu ya kutoa shukrani kwa jamii pamoja na kuokoa maisha.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Tanzania, nimefurahishwa
na huduma zinazotolewa katika Taasisi hii, katika kambi hii nimepata nafasi ya
kubadilishana ujuzi na madaktari wa JKCI na kuoana ni kwa kiasi gani
wameendelea kwani sasa wagonjwa wa moyo watanzania hawana haja ya kutafuta
matibabu nje ya nchi”, alisema Dkt. Nitish.
Naye mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo kutoka
Mkoani Dodoma Jafari Musa alisema gharama za matibabu yake zilifika kiasi cha
shilingi milioni 18 lakini kutokana na hali yake ya maisha kutokumudu kiasi
hicho cha fedha uongozi wa Taasisi uliruhusu apatiwe matibabu bila gharama.
“Naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Uongozi wa JKCI pamoja na madaktari kutoka Marekani kwa kunipatia msamaha wa
matibabu kwani sasa najisikia vizuri baada ya kukaa ndani ya chumba cha
upasuaji zaidi ya masaa manne madaktari wakitumia utaalam wao kuokoa maisha
yangu”, alisema Jafari.
Aidha Jafari amewataka watanzania kuwa na imani na Taasisi
hiyo kwani inatoa huduma bora kwa wagonjwa wa moyo, wataalamu wake huwa karibu
na wagonjwa wakati wote kufuatilia hali za wagonjwa mara kwa mara.
Comments
Post a Comment