Kwa mara ya kwanza matibabu ya uzibuaji wa mishipa ya damu ya miguu yafanyika nchini
Wataalamu wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa
ya damu ya miguu (Peripheral Interventions) ambayo haipitishi damu vizuri
wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya matibabu hayo inayofanyika jijini Dar
es Salaam. Wagonjwa 100 wenye matatizo ya mishipa ya damu ya miguu iliyoziba
wanatarajia kupatiwa matibabu katika kambi hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika
hapa nchini
Wataalamu wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na mwenzao kutoka Hospitali ya BLK iliyopo nchini India Suhail Bukhari wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya miguu (Peripheral Interventions) ambayo haipitishi damu vizuri wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya matibabu hayo inayofanyika jijini Dar es Salaam. Wagonjwa 100 wenye matatizo ya mishipa ya damu ya miguu iliyoziba wanatarajia kupatiwa matibabu katika kambi hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika hapa nchini.
Na: JKCI
************************************************************************************************************
Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefanya
upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya miguu iliyoziba kwa wagonjwa 100 wenye
matatizo hayo kwa kutumia mtambo wa Cathlab kuzibua mishipa hiyo.
Matibabu hayo yamefanyika katika kambi maalumu ya matibabu ya
siku tano inafanywa na madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mwenzao kutoka Hospitali ya BLK iliyopo nchini
India.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema hadi leo tayari
wagonjwa 40 wameshapatiwa matibabu na hali zao kuendelea vizuri ambapo baadhi
ya wagonjwa tayari wameruhusiwa.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mishipa
ya damu alisema matatizo ya mishipa ya damu ya miguu kuziba yapo kwa wingi
katika jamii na mara nyingi huwapata wagonjwa wa kisukari, wagonjwa wa shinikizo
la juu la damu pamoja na watu wanaovuta sana sigara na kunywa sana pombe.
“Wagonjwa wengi wenye matatizo ya mishipa ya damu ya miguu
kuziba wamekuwa wakikatwa miguu kwa kuchelewa kupata matibabu ama wengine
kutokujua tatizo linalowasumbua hivyo kufikia hatua ya kukatwa miguu”, alisema
Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema JKCI imeona tatizo la mishipa ya damu ya
miguu kuziba linaongezeka kwa kasi hivyo kuamua kuanzisha huduma ya matibabu
hayo na kuifanya endelevu kusaidia wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo hayo.
“Baada ya kambi hii madaktari wetu wataendelea kutoa huduma
ya matibabu ya mishipa ya miguu baada ya kupata ujuzi kutoka kwa wenzetu wa
hospitali ya BLK iliyopo nchini India”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI inaenda kuanzisha huduma
nyingine mpya kwa kushirikiana na mabingwa wa Hospitali ya BLK iliyopo nchini
India ya kuzibua mishipa ya damu iliyoziba na kusababisha matatizo ya nguvu za
kiume kupungua ili kuwasaidia wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya nguvu za
kiume.
Kwa upande wake daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu
kutoka Hospitali ya BLK iliyopo nchini India Suhail Bukhari alisema hii ni mara
ya kwanza wataalamu kutoka Hospitali ya BLK kutoa huduma katika Taasisi hiyo
lengo likiwa ni kutoa ujuzi kwa wataalam wa JKCI pamoja na kuwasaidia wagonjwa
wenye matatizo ya mishipa ya damu ya miguuni kuziba.
Dkt. Suhail alisema upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya
miguu iliyoziba unafanyika kwa utaalamu wa kisasa hivyo kuwasaidia wagonjwa
kuondokana na maumivu na changamoto walizokuwa wakipita.
“Nimeongea na Mkurugenzi wa JKCI na kumshauri kuwa na idara
tofauti za upasuaji wa mishipa ya damu ili kusaidia wagonjwa wenye mishipa ya
damu ya miguu kuziba kupata huduma kwa haraka na kufanya matibabu haya
kujulikana Afrika yote”, alisema Dkt. Suhail.
Naye Daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. George Longopa alisema mwamko wa wagonjwa
kupata huduma katika kambi hiyo umekuwa mkubwa tofauti na ilivyotarajiwa hivyo
kuonyesha kuwa tatizo la mishipa ya damu ya miguuni kuziba kuwa kubwa.
“Tulipotoa tangazo kuhusu matibabu haya wagonjwa zaidi ya 200
walijitokeza hivyo kuwagawanya katika makundi na kuanza na wagonjwa 100 katika
kambi hii, wagonjwa wengine waliobaki tutaendelea kuwahudumia kwani tayari
tumeshapata ujuzi”, alisema Dkt. Longopa.
Dkt. Longopa alisema wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya
damu ya miguuni kuziba sasa watakuwa wanapatiwa matibabu JKCI na wale ambao
watakuwa na matatizo makubwa zaidi wataendelea kushirikiana na wataalam wa afya
kutoka Hospitali ya BLK iliyopo nchini India ili ujuzi uzidi kukuwa na
kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje ya nchi kwaajili ya matibabu.
Naye Betha Mkwawa aliyepata matibabu katika kambi hiyo
alisema amesumbuliwa na maumivu ya miguu kwa muda wa miaka zaidi ya kumi bila
kujua kama mishipa yake ya damu kwenye miguu imeziba.
Betha alisema baada ya kupata ajali na kuvunjika mguu
alipatiwa matibabu nchini India miaka 13 iliyopita na baada ya matibabu hayo
alianza kuumwa mguu lakini kila alipoenda hospitali kutibiwa aliambiwa maumivu
anayoyapata yanatokana na ajali aliyoipata.
“Nimehangaika sana na huu mguu hadi mwaka 2017
nilipogundulika kuwa mishipa yangu ya damu ya miguu imeziba haiwezi kupitisha
damu vizuri nikaanzishiwa dawa hadi mwaka huu nilipoona tangazo la matibabu ya
mishipa ya damu ya miguu kuziba nikaona ni wakati sasa wa kufika hapa JKCI na
kutibiwa”,
“Namshukuru Mungu nimepata matibabu na baada ya matibabu tu
nimeona mabadiliko kwani sasa mguu wangu umekuwa mwepesi, maumivu hakuna, hali
ya kuvimba imeondoka sasa mguu umenywea naamini na hii hali ya mguu kuwa mweusi
inaenda kuisha”, alisema Betha.
Comments
Post a Comment