Wagonjwa 2760 wafanyiwa upasuaji wa moyo JKCI kwa mwaka wa fedha 2022/23
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari
wakati wa mkutano wa kuelezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo na kutoa mwelekeo wa utekelezaji kwa
mwaka wa fedha 2023/2024. Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa Idara ya
Habari - MAELEZO jijini Dar es Salaam.
************************************************************************************************************************************************************************************************
TAARIFA YA MKURUGENZI MTENDAJI WA TAASISI YA MOYO JAKAYA
KIKWETE (JKCI) DKT. PETER KISENGE KATIKA MKUTANO WA
WAANDISHI WA HABARI ULIOFANYIKA KWENYE UKUMBI WA IDARA YA HABARI - MAELEZO, DAR
ES SALAAM TAREHE 18 JULAI 2023.
Ndugu
Watumishi wa Umma,
Ndugu
Waandishi wa Habari,
Mabibi
na Mabwana,
NAWASALIMU KWA JINA LA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA……
Awali ya yote napenda kumshukuru
Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha kuifikia siku hii ya leo
tukiwa wazima wenye afya njema. Aidha, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mhe.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philipo Isdor Mpango,
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Ally
Mwalimu, Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel, Katibu Mkuu Wizara ya
Afya Dkt. Seif Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe
na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu kwa kuiwezesha Taasisi yetu kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Nawashukuru Wafanyakazi wote wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kujitoa kwao
kuwahudumia wananchi wenye matatizo ya moyo. Pia nipende kuwashukuru Waandishi
wa Habari kwa kufanya kazi na Taasisi yetu bega kwa bega ili kuhakikisha wananchi
wanapata taarifa sahihi za magonjwa ya moyo pamoja na huduma tunazozitoa.
Ndugu
Waandishi wa Habari, Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) ni hospitali maalumu inayotoa tiba ya magonjwa ya moyo,
mafunzo na utafiti. Katika kutekeleza majukumu yake Taasisi imeendelea
kuzingatia sera, mipango na mikakati yenye lengo la kuimarisha utoaji wa huduma
za kibingwa za matibabu ya magonjwa ya moyo hapa nchini.
Taasisi yetu inafanya yafuatayo:
a)
Wagonjwa
wanaotibiwa kwa siku ni 500.
b)
Wagonjwa
wanaolazwa kwa wiki ni 130.
c)
Wagonjwa
wanaofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua, upasuaji wa mishipa ya
damu na mapafu kwa siku ni sita.
d)
Kupitia mitambo
ya Cathlab (Catheterization Laboratory) wagonjwa
wanaochunguzwa, kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo na kuwekewa vifaa visaidizi
vya moyo kwa siku ni 14.
Ndugu
Waandishi wa Habari, kwa mwaka wa
fedha uliopita wa 2022/23 Taasisi yetu ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni 44.5
fedha ambazo zilitumika kufanya shughuli mbalimbali za utoaji wa huduma ya
matibabu ya moyo pamoja na shughuli za maendeleo. Katika mwaka huo wa fedha
Taasisi ilifanikiwa kufanya yafuatayo:
a) Tuliona wagonjwa 122,362 kati ya hawa watu wazima walikuwa 111,542
na watoto 10,820 wagonjwa waliolazwa walikuwa 4407 watu wazima 3286 na watoto
1121.
b)
Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa
kufungua kifua na kubadilishwa Valvu za moyo moja hadi tatu, upasuaji wa
kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery
–CABG), upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu walikuwa 714 kati ya hao watu
wazima walikuwa 412 na watoto 305. Watoto tuliowafanyia upasuaji walikuwa na
matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo
kutokukaa katika mpangilio wake na matatizo ya Valvu.
c)
Kupitia mitambo ya Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo
ni maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba ya magonjwa ya moyo inayotumia
mionzi maalumu wagonjwa 2046 kati yao
watu wazima 1762 na watoto 284 walipata
huduma za matibabu. Wagonjwa hawa walipata huduma za
uchunguzi, matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo, matibabu ya mishipa
ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba na kuwekewa vifaa visaidizi vya moyo.Uchunguzi
huu pamoja na tiba unafanyika kwa njia ya upasuaji wa bila kufungua kifua
kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja.
d)
Gharama ya matibabu ya wagonjwa hawa 2,760 tuliowafanyia
upasuaji mkubwa na mdogo wa moyo kama wangetibiwa nje ya nchi ni shilingi
62,340,000,000 lakini kwa kutibiwa kwao katika Taasisi yetu matibabu yao
yamegharimu kiasi cha shilingi 31,170,000,000 fedha ambazo
zimelipwa na bima za afya, ndugu wa wagonjwa, wafadhili na wengine kupata msamaha
wa matibabu. Kwa wagonjwa hawa kutibiwa
hapa nchini Serikali imeweza kuokoa kiasi cha shilingi
31,170,000,000 fedha ambazo zingelipwa kama wagonjwa hawa wangetibiwa
nje ya nchi.
e)
Kwa kipindi cha mwaka mmoja wagonjwa
waliotibiwa katika Taasisi yetu kutoka nje ya nchi walikuwa 301. Wagonjwa hawa
walitoka katika nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Uganda,Zambia,Visiwa
vya Comoro, Ethiopia, Burundi na wengine kutoka nje ya Afrika zikiwemo nchi za
Armenia, China, India, Norway, Marekani na Uingereza.
f)
Taasisi ilitumia shilingi bilioni 1,249,521,800 kwaajili ya kununua
mashine mbalimbali zikiwemo za utasishaji
wa vifaa vya Hospitali,
Digital X-Ray na mashine tatu za kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi
(Echocardiography).
g) Tarehe 20/4/2023 Taasisi yetu ilisaini makubaliano
ya miaka miwili na Hospitali za Taifa za nchini Rwanda na Zambia ya kutibu
wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hizo.
Pia tumesaini makubaliano ya kushirikiana katika
utoaji wa huduma za matibabu kwa
wagonjwa, kubadilishana ujuzi wa kazi, kufanya tafiti mbalimbali na kutoa mafunzo
kwa wafanyakazi wetu na chuo Kikuu cha Jagiellonian
cha nchini Poland, chuo cha madaktari wa upasuaji Afrika Mashariki, Kati na
Kusini mwa Afrika (COSESCA) nchi ya Malawi, Visiwa vya Comoro, Taasisi ya
Afya Ifakara (IHI), Taasisi
ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
h) Kupitia kozi ya miezi sita ya mafunzo
ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura inayotolewa kwa wauguzi kati ya wanafunzi 50 waliomaliza sita walitoka
katika nchi za Rwanda na Zambia.
i)
Katika
kutoa huduma za tiba mkoba
zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan Outreach Services tulifanya
upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi
kwa kuwafuata mahali walipo. Huduma hii imetolewa katika
mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Pwani,
Arusha, Geita, Iringa, Mtwara, Lindi, Unguja, Manyara na Pemba. Wananchi 6309 walifikiwa
na huduma hii kati ya hao 3239 walikutwa na matatizo ya moyo na waliopewa rufaa
ya kuja kutibiwa JKCI walikuwa 724.
j)
Mwezi
Mei mwaka huu wataalamu wetu walikwenda nchini Malawi katika Hospitali ya Queen Elizabeth kutoa huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo, huduma
hii ilitolewa kwa watu 724. Waliokutwa
na matatizo ya moyo walikuwa 537 kati yao 201 walipewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu.
k)
Serikali kupitia Sekretarieti ya
Ajira katika Utumishi wa Umma iliajiri wafanyakazi wapya 64 wa kada
mbalimbali na wafanyakazi 98 walipandishwa vyeo katika madaraja tofauti. Wafanyakazi 50 walilipiwa ada za masomo katika kozi mbalimbali
walizozifanya.
l)
Tarehe
14 Novemba mwaka jana Serikali ilitupatia Hospitali ya Dar Group iliyopo
wilayani Temeke kuwa sehemu ya JKCI. Kwa kutupatia hospitali hii kumetatua changamoto
ya nafasi ambayo tulikuwa tunakabiliana nayo kwa muda mrefu na kutatusaidia
kuboresha huduma za matibabu tunazozitoa kwa wananchi.
m) Tumechapisha matokeo ya tafiti za kisayansi
(Publication) 12 katika majarida ya kimataifa (International scientific
journals).
Ndugu Waandishi wa Habari, Kwa mwaka wa fedha 2023/24 Taasisi imetenga bajeti ya kiasi cha
Shilingi Bilioni 66.3 fedha hizi zitatumika kwaajili ya utekelezaji wa kazi
mbalimbali zilizoainishwa kwenye Mpango Kazi na Bajeti ya Mwaka 2023/24.
Taasisi itatumia fedha hizi kulipa
mishahara ya wafanyakazi, uendeshaji wa gharama za Taasisi, manunuzi ya vifaa
tiba na dawa, kusomesha wataalamu wetu kozi za muda mrefu na muda mfupi pia
zitatumika kwenye miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la vipimo vya
uchunguzi wa magonjwa pamoja na ofisi za utawala, ujenzi wa jengo la kutolea
huduma za matibabu kwa watoto katika Hospitali yetu ya Dar Group na ununuzi wa
vifaa kazi.
Mchanganuo
wa maeneo ambayo yamepewa kipaumbele katika bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2023/24
ni pamoja na yafuatayo:-
a)
Kuimarisha tiba za moyo kwa
kudhamini masomo ya muda mfupi na mrefu kwa wafanyakazi, kununua vifaa tiba vya
kisasa zaidi, kuendeleza ujenzi mbalimbali, kutoa huduma
za tiba mkoba kwa kuwafuata wananchi walipo.
b)
Kuendelea kutoa elimu ya
magonjwa ya moyo pamoja na lishe bora kwa wananchi kupitia luninga, magazeti na
mitandao ya kijamii.
Ndugu Waandishi wa Habari, manufaa ambayo wananchi watayapata kupitia vipaumbele vya Taasisi
kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni pamoja na:
a)
Kuzidi kuimarika
kwa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwani wataalamu wanazidi kuongeza
ujuzi walionao kupitia kozi za muda mrefu na mfupi wanazosoma pia kununuliwa
kwa vifaa tiba vya kisasa kutasaidia kutolewa kwa huduma bora kwa wananchi.
b)
Kukamilika kwa
jengo la utawala na vipimo ambalo limegharimu
kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kutasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata
huduma za vipimo vya moyo kwa wakati pia wafanyakazi watakuwa na ofisi za
kutosha na hivyo kupunguza msongamano katika ofisi walizopo.
c)
Taasisi
itaendelea kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchi kwa
kuwafuata mahali walipo (Mhe. Dkt.Samia Suluhu
Hassan Outreach Services) kwa kufanya hivyo wenye matatizo ya moyo
watapata huduma za matibabu mapema tofauti na ambavyo wangezifuata huduma hizo
Dar es Salaam. Tunafanya hivi kwa kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowatibu
mioyo yao huwa imechoka hii ni kutokana na kuchelewa kufika JKCI kwaajili ya
kupata matibabu ya kibingwa ya magonjwa haya.
d)
Kupitia vyombo
vya habari Taasisi itaendelea kutoa elimu ya jinsi ya kuyaepuka magonjwa ya
moyo kwa wananchi kwani magonjwa haya ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu
anaweza kuyaepuka akifuata mtindo bora wa maisha. Pia tutaendelea kutoa elimu
ya matumizi sahihi ya dawa za moyo pamoja na umuhimu wa kufuata ushauri wa
wataalamu wa afya kwa wagonjwa wa moyo.
Ndugu Waandishi wa Habari, ninaomba nimalizie taarifa yangu kwa kuwakumbusha wananchi mambo
yafuatayo:
a) Unaweza kuepuka kupata magonjwa ya moyo kwa kufanya mazoezi.
b) Kuzingatia lishe bora kwa kula matunda, mboga mboga, vyakula vyenye
madini ya potassium vile vile kupunguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta
na chumvi.
c) Kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri, kutambua kiwango cha sukari katika mwili wako,
kutambua msukumo wako wa damu na kiwango cha mafuta mwilini.
d) Kupima afya ya moyo japo mara moja kwa mwaka kunaweza kukakusaidia kujua
kama una tatizo hili au la na kama unatatizo utaweza kupata matibabu mapema.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
“Afya
ya Moyo Wako ni Jukumu Letu”.
Imetolewa na :
Dkt.
Peter Kisenge
Mkurugenzi Mtendaji
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
Comments
Post a Comment