JKCI yatoa elimu ya utalii tiba katika maonesho ya Sabasaba
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikweye (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimpima mapigo ya moyo kama yanadunda inavyotakiwa mkazi wa
Dar es Salaam aliyefika katika banda la Taasisi hiyo kwaajili ya kufanyiwa
uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa
ya Dar es Salaam (SABASABA).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikweye (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimpima kiwango cha oksijeni mwilini mtoto aliyefika katika
banda la Taasisi hiyo kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi wa agonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 47 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA).
Daktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Baraka Ndelwa akiwafundisha wanafunzi wa shule ya Sekondari Tusiime jinsi ya kujikinga na magonjwa ya moyo walipotembelea banda la hilo kwaajili ya kujifunza wakati wa maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA).
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inatoa elimu ya utalii
tiba kwa wageni wanaotembelea katika banda la Taasisi hiyo ili kuihamasisha
jamii kutumia huduma za tiba kama sehemu ya utalii.
Katika ketekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Taasisi hiyo imeona ni muhimu kuelimisha umma kuhusu utalii tiba kwani JKCI
inapokea wagonjwa kutoka nchi zaidi ya 20 wanaopata huduma za uchunguzi na
matibabu ya moyo katika Taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa
JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI imeona ni muhimu katika maonesho hayo
kutoa elimu ya utalii tiba kwani maonesho hayo yanahusisha wafanyabiashara
kutoka nchi zaidi ya 16 hivyo ni muhimu wakafahamu wakifika Tanzania kwa ajili ya shughuli za biashara pia
wanaweza kupata huduma bora JKCI lakini pia wakatumia fursa hiyo kutembelea
vivutio vilivyopo nchini.
“Watu wanaofika katika banda letu wanajionea huduma tunazozitoa
na kuhamasika kutufikia pale wanapopata changamoto za afya nasi tunawaahidi
kuwapa huduma bora na kwa wakati”,
“Banda letu lina madaktari bingwa wa moyo, wauguzi na
wataalamu wa afya waliobobea ambao kwa pamoja wamejipanga kuhakikisha huduma
bora zinatolewa kwa washiriki na watembeleaji wa maonesho haya ya 47 ya
Biashara”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema JKCI wakati wa maonesho ya Sabasaba imepata
wananchi wengi waliofika katika banda la Taasisi hiyo kwaajili ya kufanyiwa
uchunguzi na matibabu ya moyo, kupata elimu kuhusu magonjwa ya moyo, kupata
elimu ya lishe kutoka kwa mtaalamu wa lishe lakini pia watu kutoka nchi mbalimbali
wamefika katika banda hilo kuona huduma zinazotolewa.
Dkt. Kisenge alisema Serikali imewekeza katika Taasisi hiyo
ikiwemo uwekezaji wa vifaa vya kisasa vya upasuaji mdogo na upasuaji mkubwa wa moyo
hivyo kuifanya JKCI kufanana na Hospitali nyingine kubwa zinazotoa huduma ya
matibabu ya moyo katika nchi kubwa duniani.
“Kutokana na uwekezaji uliopo Taasisi yetu, sasa tunatoa
huduma ya premium au VIP kwa watu wanaohitaji kupata huduma binafsi na haraka
wanaweza wakapata huduma hiyo hivyo kupunguza muda mrefu wa kukaa hospitali kusubiri
kupata huduma”, alisema Dkt. Kisenge
Naye mkazi wa Dar es Salaam aliyefika katika banda hilo kwaajili
ya kupata huduma Mlele Mrisho amewataka wananchi kutumia fursa ya kuchunguza
afya zao wakati wa maonesho ya Sabasaba kwani watapata huduma kwa haraka na kwa
gharama nafuu.
“Huduma nilizopota katika banda la JKCI ni nzuri na za bei
nafuu tofauti na kama ningeenda hospitali, ni muhimu watu wakatumia fursa hii
kupima afya zoa wakati wa maonesho ya Sabasaba”,
“Nimefanyiwa vipimo vya moyo na shinikizo la damu, nimekutwa
na shinikizo la juu la damu na kupewa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya uchunguzi
zaidi, nisingepima leo nisingejijua kama nina shida ya shinikizo la juu la
damu”, alisema Mrisho.
Comments
Post a Comment