Dkt. Kisenge: Shinikizo la juu la damu linaua; Chukua tahadhari
Mkurugenzi wa Huduma ya Uuguzi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akimpima Salome Majaliwa shinikizo la damu (BP) wakati wa maadhimisho ya siku ya shinikizo la juu la damu duniani ambayo hufanyika kila
mwaka tarehe 17 mwezi wa tano.
*********************************************************************************************************************************************************************************************
Na Anna Nkinda - JKCI
Asilimia 25 ya vifo vya magonjwa ya moyo vinavyotokea duniani vinasababishwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu
mafanikio yaliyopatikana katika taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ya
uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema kwa kipindi cha miaka mitatu Taasisi hiyo imeona wagonjwa 361,894 wakiwemo watu wazima 331,557 na
watoto 30,337 kati ya
hao wagonjwa 238,850 ambao ni sawa na asilimia 66 walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.
Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema asilimia 90 ya wagonjwa wa
shinikizo la juu la damu hawana dalalili mpaka wapime wagonjwa wachache
wanakuwa na dalili za maumivu ya kichwa, macho kuona kiza, maumivu ya misuli ya
shingo, kutoka damu puani na wakati mwingine kupoteza fahamau, maumivu makali
kifuani, kuzunguzungu, mapigo ya moyo kwenda kasi na kutoka damu puani.
“Uonapo dalili hizi wahi hospitali mapema kwa ajili ya
kufanyiwa uchunguzi na kupata matibabu pia ninawasihi watu wajenge tabia ya
kupima shinikizo la damu na kiwango cha sukari kwenye damu mara kwa mara na kwa
wale watakaokutwa na tatizo na kuanzishiwa dawa wasiache kuzitumia hata kama
watapata naafuu”, alisema Dkt. Kisenge.
Mtaalamu huyo wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu alisema
unaweza kuepuka kupata shinikizo la juu la damu kwa kufanya mazoezi, kuzingatia
lishe bora kwa kula matunda, mbogamboga, vyakula vyenye madini ya potassion
vilevile kupunguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta na chumvi.
Kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri, kutambua kiwango cha
sukari mwilini, kutambua msukumo wa damu na kiwango cha mafuta mwilini.
Dkt. Kisenge aliyataja madhara yanayotokana na shinikizo la juu
la damu kuwa ni mwili kupooza, shambulio la moyo, moyo kushindwa kufanya kazi,
kutanuka kwa ukuta wa mishipa ya moyo, ugonjwa wa figo, kupunguza nguvu za
kiume, kifo cha ghafla na kupunguza muda wa kuishi.
Comments
Post a Comment