JKCI kushirikiana na UDSM kutoa mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ushirikiano wa JKCI na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kutoa mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof. Bonaventure Rutinwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu ushirikiano wa Chuo hicho na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kutoa mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Khuzeima Khanbhai akielezea aina
ya mafunzo yanayotolewa katika taasisi
hiyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu ushirikiano wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) na JKCI katika kutoa
mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo.
Mkufunzi wa mfunzo ya
kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Joshua Ogutu akitoa tathmini ya mafunzo yanayotolewa na JKCI wakati wa
mkutano na waandishi wa habari kuhusu ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) na Taasisi hiyo katika kutoa
mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo.
********************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika kutoa mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo katika
program za jinsi za kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura, upasuaji wa
moyo na udaktari bingwa wa masuala ya kufanya upasuaji wa kutibu kwa njia ya tundu
dogo la moyo.
Mafunzo mengine yanayotolewa ni pamoja na mfunzo endelevu
yaliyoanza kutolewa na JKCI tangu mwaka 2021 ya namna ya kuwahudumia wagonjwa
wa dharura, wagonjwa mahututi na wagonjwa wenye shida za figo wanaofanyiwa
dialysis.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika Hospitali za umma kuanzia
hospitali za wilaya hadi za taifa ikiwemo ujenzi wa vyumba vya kuhudumia
wagonjwa mahututi na wa dharura pamoja na vifaa tiba ambavyo vinahitaji
wataalamu wabobezi kuvitumia katika kuwatibu wagonjwa.
Dkt. Kisenge alisema JKCI iliona nguvu kubwa ambayo Serikali
imefanya hivyo kuamua kuwekeza katika kutoa mafunzo yatakayokidhi hadhi za
kimataifa za kutumia vifaa hivyo na kutoka huduma stahiki kwa wagonjwa wa moyo,
wagonjwa wa dharura, mahututi na
wagonjwa wanaofanyiwa usafishwaji damu kwenye figo (dialysis).
“Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni chuo cha kwanza kuanzisha
kozi za afya hapa nchini, tumeona tushirikiane nao katika kutoa mafunzo haya
ili wataalamu wanapomaliza mafunzo waweze kupata cheti kutoka chuo
kinachotambulika duniani kote”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema mafunzo yatakayotolewa yatawafikia
wataalamu wa afya waliopo nchi za Afrika mashariki na kati hivyo kuziomba hospitali
zote nchini kutosita kuwapeleka wataalamu wao kupata fursa hiyo.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) Prof. Bonaventure Rutinwa alisema UDSM imeanza ushirikiano na
JKCI katika kutoa mafunzo yanayohusiana na tiba na sayansi shirikishi upande wa
moyo kutokana na kuwepo na uhaba wa wataalamu katika fani hiyo.
Prof. Rutinwa alisema chuo hicho kimeamua kushirikiana na
JKCI na kuanza kupitia mitaala ili kiweze kutoa mafunzo bobezi na ujuzi wa hali
ya juu hivyo kuwalazimu kuwa na taasisi ambayo itatoa mafunzo kwa vitendo ya
kile kinachofundishwa darasani.
“Kozi zote ambazo tutakuwa tunazitoa zitaenda kujikita zaidi
katika kuwapatia wataalamu uwezo wa kutenda na sio nadharia”,
“Taasisi zote mbili zimepata ridhaa ya mamlaka zake na
kuruhusu mashirikiano haya kuwepo hivyo kwakuanzia tutakuwa na kozi za muda
mfupi lakini lengo letu ni kuifanya JKCI kuwa chuo kilichounganishwa na UDSM
ambacho kitakuwa kinatoa mafunzo ya shahada chini ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam”, alisema Prof. Rutinwa
Naye mkufunzi wa mafunzo ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura
na mahututi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Joshua Ogutu alisema JKCI
ilianza kutoa mafunzo kwa wauguzi wanaofanya kazi katika vyumba vya wagonjwa
mahututi na wa dharura tangu mwaka 2021.
Ogutu ambaye pia ni Afisa Uuguzi katika Taasisi hiyo alisema
mafunzo hayo yalianzishwa baada ya kuona uhitaji mkubwa uliopo katika kutoa
huduma za kina za uuguzi na kuwepo na uhitaji wa wauguzi wenye uwezo wa kutumia
vifaa vyote vinavyotoa huduma za dharura.
“Mafunzo yetu ya kwanza yalianza Decemba 2021 ambapo tulipata
wanafunzi 13 waliohitimu mafunzo yao Julai 2022, Agosti 2022 tulisajili mafunzo
ya awamu ya pili na kupata wanafunzI 22 ambao kati yao watatu walitoka nchini
Rwanda na kumaliza mafunzo yao mwezi Aprili 2023”.
“Mafunzo ya awamu ya tatu tulisajili wauguzi 28 kati yao
watatu walitoka nchini Zambia ambao walimaliza mwezi Februari mwaka huu na
mafunzo yetu ya awamu ya nne tutayafanya kwa kushirikiana na UDSM yataanza
tarehe 11 Machi mwaka huu ambapo hadi sasa tayari wanafunzi 12 wameshajisajili”,
alisema Ogutu.
Ogutu alisema kupitia mafunzo wanayoyatoa kumekuwa na mafanikio makubwa kwani wanafunzi wote waliofanya mafunzo hayo wamekuwa wakipata fursa za ajira kirahisi.
Comments
Post a Comment