Watu 447 wapimwa moyo Kagera
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari na mwenzake wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) Martin Rwabilimbo wakimsikiliza mwananchi aliyefika BBRH kwaajili ya kupata huduma ya matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu iliyomalizika hivi karibuni mkoani Kagera.
Wataalamu wa Taaasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizkia kwa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika mkoani Kagera. Jumla ya watu 447 wakiwemo watu wazima 405 na watoto 42 walifanyiwa uchunguzi wa moyo katika kambi hiyo.
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) Ernest Lengesela akimpima kipimo cha kuangalia shinikizo la damu mwilini mwananchi aliyefika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya upimaji iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa BRRH.
Mtafiti wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Saadi Kamtoi akimwelekeza Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) Jenny
Ndimuhela namna ya kujaza dodoso la kuwatambua wagonjwa wa moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi
na matibabu ya moyo iliyomalizika hivi karibuni mkoani Kagera.
**************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Jumla ya watu 447 wakiwemo watu wazima 405 na watoto 42 wamepata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika hivi karibuni mkoani Kagera.
Kambi hiyo ya siku tano ilifanywa na wataalamu
wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH).
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo daktari
bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Yona Gandye alisema kwa upande wa watu
wazima zaidi ya asilimia 95 ya watu waliowafanyiwa vipimo waliwakuta na tatizo
la shinikizo la juu la damu.
“Baadhi ya hawa tuliowakuta na tatizo
la shinikizo la damu walikuwa na
matatizo mengine ya moyo ikiwemo moyo kutanuka, uwezo wa moyo kusukuma damu
kuwa chini na wengine walikuwa na shida katika utengenezaji wa mapigo ya moyo
na hivyo mapigo yao ya moyo kuwa chini kuliko kawaida”,.
“Watoto tuliowapima baadhi yao
tumewakuta na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu kwenye moyo
na mishipa ya damu”, alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alisema wagonjwa 55
wakiwemo watu wazima 50 na watoto watano ambao wamekutwa na matatizo ya moyo
yaliyohitaji matibabu ya kibingwa wamepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika
Taasisi hiyo.
“Tunashukuru kambi hii imeenda vizuri
kwani uitikio kutoka kwa wananchi ulikuwa mkubwa na tumeweza kubadilishana
ujuzi wa kazi na wenzetu wa BRRH ambao wataendelea kutoa huduma za matibabu ya
moyo hata baada ya sisi kuondoka”, alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Bukoba Dkt. Museleta Nyakiroto aliishukuru JKCI
kwa kufanya kambi hiyo na kusema kuwa licha ya wananchi kupata huduma ya
kibingwa ya matibabu ya moyo lakini pia imewajengea uwezo wataalamu wa BRRH
katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo.
Dkt.
Nyakiroto alisema
wananchi wataendelea kupata huduma za matibabu ya moyo katika hospitali hiyo kwani
wataalamu wa BRRH wamejifunza kwa vitendo kutoka kwa wenzo wa JKCI na kama itatokea
kuna mgonjwa ambaye atakuwa na tatizo litakalohitaji matibabu ya kibingwa
watamtuma JKCI au Hospitali ya Kanda Bugando kwaajili ya kupata huduma zaidi.
“Tutaendeleza uhusiano uliopo baina
ya JKCI na BRRH na ninatarajia upimaji wa aina hii ufanyike zaidi ya mara moja
kwa mwaka kwani wagonjwa ni wengi wanaohitaji matibabu ya kibingwa ya moyo”
“Nimejifunza wenzetu wa JKCI kila
mgonjwa wanayemuona anapita kwa wataalamu wa lishe kupata ushauri nasi hapa
tunawataalamu wa lishe, tutaboresha
huduma na kuhakikisha wagonjwa wetu wanapita kwa wataalamu wa lishe ili kupata
huduma ya ushauri wa lishe bora ambayo itawasaidia kuepukana na magonjwa
yasiyoambukiza”, alisema Dkt. Nyakiroto.
Nao wataalamu wa afya kutoka BRRH ambao
walikuwa wanafanya kazi pamoja na wenzao wa JKCI walisema kambi hiyo
imewajengea uwezo wa jinsi ya kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo na
kufahamu mgonjwa ampe huduma ipi na kwa wakati gani.
“Nimejifunza mambo mengi ikiwemo jinsi
ya kuwatambua wagonjwa wa moyo kabla hawajafika katika hatua mbaya na jinsi ya
kuwatibu, kufanya vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na
mfumo wa umeme wa moyo na upimaji huu naweza kuufanya kwa mgonjwa yupi na kwa
wakati gani”, alisema Dkt. Milton
Kabiligi wa BRRH.
Wananchi waliopata huduma za
uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa
huduma hiyo na kusema kuwa imewapunguzia gharama ya kusafiri na kuifuata jijini
Dar es Salaam ambako ni mbali na mkoa wa Kagera.
“Huduma ni nzuri na nimeridhika nayo,
kwa muda mfupi niliofika hapa nimepata huduma zote zikiwemo za vipimo na
ushauri ninawasihi wenzangu zinapotokea nafasi kama hizi wazitumie vizuri kwa
kujitokeza kupima magonjwa mbalimbali”, alisema Erick Byabato mkazi wa Misenyi.
“Nimepima vipimo vyote vya moyo
nimekutwa sina tatizo, shida niliyonayo ni uzito mkubwa nimeonana na mtaalamu
wa lishe ambaye amenielekeza jinsi ya kula vyakula bora ambavyo vitanisaidia
kutokupata magonjwa ya moyo pia amenisisitiza umuhimu wa kufanya mazoezi ambayo
yatanisaidia kupunguza uzito”, alisema Restituta Barungi mkazi wa Bukoba.
Comments
Post a Comment