JKCI wapigwa msasa wa kutambua viatarishi maeneo ya kazi
Mkufunzi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) CPA. Gabriel Mwero
akitoa mafunzo ya namna ya kutambua viashiria mbalimbali vinavyoweza
kusababisha hatari katika eneo la kazi wakati wa mafunzo hayo ya siku mbili
yaliyotolewa kwa viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na
kumalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kutambua viashiria mbalimbali vinavyoweza kusababisha hatari katika eneo la kazi yaliyotolewa kwa viongozi wa Taasisi hiyo na kumalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wajumbe wa bodi ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kutambua viashiria mbalimbali vinavyoweza kusababisha hatari katika eneo la kazi yaliyotolewa kwa viongozi wa Taasisi hiyo na kumalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
**********************************************************************************************************
Taasisi za umma zimetakiwa kuzingatia miongozo inayotolewa na
Serikali ikiwa ni pamoja na miongozo ya kuweka mifumo ya kubainisha viatarishi
katika maeneo ya kazi.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na mkufunzi wa mafunzo ya
viashiria hatarishi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania CPA.Gabriel Mwero wakati wa mafunzo ya siku mbili ya kudhibiti
viashiria hatarishi vinavyoweza kuathiri shughuli zinazofanywa na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
CPA. Mwero alisema serikali kupitia wizara ya Fedha ilitoa muongozo wa
kuzitaka taasisi za umma kuweka taratibu za kuwawezesha kuainisha viatarishi na
kutafuta muafaka wa kuzuia viatarishi hivyo visiendelee.
“JKCI imeandaa mafunzo haya lengo likiwa kuongeza utaalamu wa
namna ya kukabiliana na viashiria hatarishi kuweza kufikia malengo ya taasisi
yao”, alisema CPA. Mwero.
CPA. Mwero alisema madhara ya viatarishi yanaweza kupelekea matumizi
mabaya ya fedha, kukiukwa kwa taratibu za manunuzi pamoja na kuharibu taratibu
za utendaji wa kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI ni moja ya Taasisi bora inayotoa
huduma za matibabu ya moyo barani Afrika hivyo ni muhimu kuweka mbinu za
kukabiliana na viashiria hatarishi ili kulinda rasilimali zilizowekezwa katika taasisi
hiyo.
“Sisi kama viongozi wa Taasisi tumetengeneza muongozo wetu
unaoangalia viashiria vinavyoweza kuleta kasoro katika kutoa maamuzi ya
kiutendaji”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema kupitia mafunzo hayo viongozi wameweza kupata
mbinu za kutambua viashiria hatarishi vinavyoweza kuharibu utendaji wa kazi na
wakati mwingine hata kuiangusha taasisi.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Ubora wa Huduma wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Naizihijwa Majani alisema mafunzo hayo yamelenga kuhakiksha
JKCI haiwezi kusimama katika kutoa huduma zake kwa kuweka mbinu za kudhibiti
viatarishi.
“Mafunzo haya ni muhimu kwani yanahakikisha huduma
hazisimami kwasababu kama tusipoweza kusimamia viatarishi tunaweza kusimamisha
huduma hivyo kuathiri maisha ya wagonjwa wetu”, alisema Dkt. Naizihijwa
Dkt. Naizihijwa alisema mafunzo hayo ni mwanzo wa mafunzo mengine
kwani mpango wa taasisi ni kuhakikisha kuwa kila mtumishi wa taasisi hiyo
anapatiwa mafunzo ya kuweza kutambua viatarishi katika eneo la kazi.
Comments
Post a Comment