JKCI kuokoa milioni 500 wagonjwa wa moyo 15 kutibiwa nchini
*************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeweza kuokoa kiasi
cha shilingi milioni 500 ambazo Serikali ingeweza kutumia kuwapeleka wagonjwa
wa moyo 15 nje ya nchi watakaotibiwa katika kambi maalumu ya upasuaji wa moyo
na mishipa ya damu inayofanywa na taasisi hiyo.
Kambi hiyo maalumu ya siku tano inafanywa na wataalamu wa
afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Cardiostart International
la nchini Marekani kwa wagonjwa wa moyo na mishipa ya damu wanaohitaji matibabu
ya upasuaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema Shirika la Cardiostart International limeanza kushirikiana na JKCI
tangu mwaka 2019 ambapo hadi sasa wameshafanya kambi maalumu za matibabu ya
moyo tano.
Aidha Dkt. Kisenge alisema sambamba na kutoa huduma za
matibabu shirika hilo pia limeweza kutoa vifaa tiba kwa wagonjwa wa upasuaji wa
moyo wanaotibiwa JKCI vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan ametengeneza mahusiano mazuri na nchi mbalimbali, mahusiano
ambayo yanatuwezesha kupata wataalamu kutoka nchi tofauti kufika JKCI kwaajili
ya kubadilishana ujuzi pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo
tunaowahudumia”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa
ya damu kwa watoto na watu wazima kutoka Shirika la Cardiostart International la
nchini Marekani Prof. Aubyn Marath alisema JKCI haijarudi nyuma hata baada ya
changamoto ya ugonjwa wa UVIKO 19 ulioiyumbisha dunia bado taasisi hiyo
imeendelea kukuwa upande wa wataalamu wabobezi, huduma za kibingwa na uwezo wa
kuokoa maisha ya wagonjwa.
Prof. Aubyn alisema shirika la Cardiostart International limekuwa
likiunganisha nguvu ya wataalamu wote wa afya wanaofanya kazi katika chumba cha
upasuaji wa moyo kuhakikisha kuwa ushirikiano katika kutoa huduma kwa wagonjwa
unafanyika kwa kiwango cha hali ya juu kuokoa maisha.
“Wataalamu wa JKCI mmendelea kuonyesha utalamu wenu, uadilifu
na kujitoa kwenu kuhakikisha kuwa huduma hizi za matibabu ya moyo zinaendelea
kukuwa hapa Tanzania, nawapongeza sana kwa hilo”, alisema Prof. Aubyn
Naye daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu
kwa watu wazima wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evarist Nyawawa
alisema Prof. Aubyn kutoka Shirika la Cardiostart International amekuwa akiwawezesha
wataalamu wa JKCI kutoa huduma za upasuaji mkubwa wa moyo na kupandikiza
mishipa ya damu tangu kuanzishwa kwa matibabu hayo.
Dkt. Nyawawa alisema mbali na kutoa mafunzo ya upasuaji kwa
wataalamu wa JKCI Prof. Aubyn aliweza kutafuta vyuo mbalimbali katika nchi
tofauti na pale nafasi ilipopatikana aliwaunganisha wataalamu wa afya wa JKCI
kupata mafunzo katika vyuo hivyo.
“Mimi ni mmoja wa wataalamu wa JKCI ambaye Prof. Aubyn
aliniunganisha na chuo kilichopo nchini Brazil kupata mafunzo kupitia program
zake za mafunzo ya upasuaji wa moyo na mishipa ya damu”, alisema Dkt. Nyawawa.
Dkt. Nyawawa alisema Cardiostart International imekuwa ikitoa
ushirikiano na JKCI kuwaunganisha wataalamu mbalimbali duniani kufanya kambi za
upasuaji wa moyo na JKCI.
Comments
Post a Comment