JKCI yaombwa kutoa elimu ya lishe kwa wananchi
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Mlagwa Yango akimpima kipimo cha kuangalia
jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mwananchi aliyepatiwa
huduma katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo. Kambi hiyo maalumu ya siku
mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group Laetitia Kokutangaza akimpima shinikizo la damu mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
Mfamasia kutoka kampuni ya Microlabs Laborex Zawadi Mbasa akimpatia dawa mwananchi aliyefika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
************************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wameiomba Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kuendelea kutoa elimu ya lishe bora ambayo itawasaidia
kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo.
Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa kambi
maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo inayofanywa na wafanyakazi
wa Taasisi hiyo katika Hospitali ya JKCI Dar Group.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma
katika kambi hiyo walisema licha ya kupata huduma za matibabu pia wamefurahia
kupata elimu ya lishe ambayo imewasaidia kufahamu namna bora ya kuchagua
makundi ya vyakula.
Mzee Abdalah Yasini mkazi wa Temeke alisema inawezekana
kupatwa kwake kwa tatizo la mishipa ya damu kuziba kulisababishwa na kutokupata
elimu ya lishe bora kwani angejua toka zamani namna ya kula chakula chenye
mchanganyiko wa makundi yote ya vyakula kwa kiasi angeweza kuepuka tatizo la
mishipa yake ya damu kuziba.
“Ninawaomba wataalamu wa lishe watafute namna ya kufikisha
elimu ya lishe bora kwa jamii hata ikiwezekana katika vyombo vya habari kuwe na
kipindi cha lishe kitatusaidia sana”, alisema Mzee Abdalah
Mzee Abdalah alisema kama jamii itazingatia lishe bora kwa
kutumia makundi yote ya vyakula kwa kiasi kutasaidia kupunguza magonjwa
yasiyoambukiza na kuwa na jamii yenye afya bora.
Mama Yusta Joseph mkazi wa Kimbiji Dar es Salaam alisema elimu
ya lishe aliyoipata inaenda kumbadilisha kwa kiasi kikubwa kwani kuna vitu
amekuwa akivifanya ili kupunguza uzito kumbe alikuwa akifanya kimakosa.
“Elimu niliyoipata leo itaenda kunisaidia kwani nilikuwa
najitahidi kupambana kupunguza uzito kwa kutumia njia ambayo si sahihi,
nilikuwa sili milo ya asubuhi na mchana nakula usiku tu lakini nilivyofika hapa
mtaalamu amenipa maelekezo kuwa ninapokula jioni na kwenda kulala sehemu kubwa
ya chakula hutunzwa kama mafuta”, alisema Yusta
Yusta alisema mtaalamu wa lishe amemshauri kupunguza mlo wa
jioni na namna ya kupata chakula bora kuanzi mlo wa asubuhi hadi jioni huku
akimpa mbinu za kupunguza uzito wake bila ya kuleta athari nyingine za kiafya.
“Kwakweli elimu niliyoipata leo haitakuwa ya msaada kwangu tu
bali ninaenda kuisaidia familia yangu kwasababu mimi ndio mama yao na mimi ndio
mpishi hivyo ninaenda kuwasaidi pia katika kuboresha afya zao”, alisema Yusta
Mkuu wa Kitengo cha Lishe Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
Maria Samlongo alisema wamekuwa wakitoa elimu ya lishe bora kwa wagonjwa
wanaotibiwa katika taasisi hiyo pamoja na wananchi wanaohudumiwa katika kambi
ambazo wamekuwa wakizifanya.
Maria alisema wataendelea kushirikiana na vyombo vya habari
ili kuhakikisha elimu ya lishe bora inawafikia wananchi wengi zaidi.
“Bado elimu ya lishe haijaweza kuwafikia watu wote kutokana
na uchache wa wataalamu wa lishe, kama JKCI tumetengeneza vipeperushi
mbalimbali vinavyotoa elimu ya umuhimu wa lishe bora katika kupambana na
magonjwa yasiyoambukiza”, alisema Maria
Katika kambi hiyo jumla ya watu 364 walipatiwa huduma za
upimaji wa magonjwa ya moyo ambapo kati yao watoto walikuwa 41 na watu wazima
323.
Watoto 11 walikutwa na matundu kwenye moyo, shida za valvu na matatizo ya mishipa ya damu huku watu wazima 161 sawa na asilimia 50 walikutwa na matatizo
ya shinikizo la damu pamoja na magonjwa mengine ya moyo ikiwemo mishipa ya damu
na matatizo ya valvu za moyo.
Comments
Post a Comment