Kambi ya upimaji na matibabu ya moyo yafanyika JKCI Dar Group

Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika foleni ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo zinazotolewa katika kambi maalumu ya siku mbili. Huduma hiyo inatolewa katika Hospitali ya JKCI Dar Group inayoenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Edwin Masue akimpima shinikizo la damu mwananchi wa Dar es Salaam wakati wa kambi maalumu ya siku mbili inayoenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Eva Wakuganda akimpima moyo mtoto wakati wa kambi maalumu inayofanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani. 


Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Maria Samlongo akimpa elimu ya lishe mwananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kambi maalumu ya siku mbili inayofanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani.

Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Noel Mingwe akimpima sukari kwenye damu mwananchi wa mkoa wa Dar es Salaam aliyefika katika kambi maalumu kwaajili ya kupima moyo. Kambi hiyo maalumu ya siku mbili inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

***************************************************************************************************************

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group inafanya
kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa
mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.


Huduma hiyo ya upimaji inatolewa kwa siku mbili za jumamosi na jumapili kwa

watoto na watu wazima.


Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa JKCI Hospitali

ya Dar Group Iddi Lemmah wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika
katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuona huduma zinazotolewa katika kambi hiyo.


Lemmah alisema upimaji huo una lengo la kusogeza huduma za matibabu ya

kibingwa ya moyo kwa wananchi na kuwahamasisha wananchi kujenga tabia ya
kupima afya za mioyo yao mara kwa mara.


“Upimaji huu unajulikana kwa jina la Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu

Hassan ambapo wataalamu wa Taasisi yetu wanawafuata wananchi mahali walipo
na kutoa huduma za ushauri,elimu, upimaji na matibabu ya moyo”.


“Huduma inayotolewa hapa ni ya kupima urefu na uzito, kiwango cha sukari

kwenye damu, shinikizo la damu mwilini, tunaangalia uwiano baina ya urefu na
uzito, tunatoa elimu ya lishe bora kwa wananchi na tunapima jinsi moyo
unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa moyo”, alisema Lemmah.


Lemmah alisema katika upimaji huo wanashirikiana na makampuni mbalimbali ya

uagizaji na usambazaji wa dawa za binadamu ambapo wananchi wanaokutwa na
matatizo ya moyo, kisukari na magonjwa mengine wanapewa dawa za kwenda
kutumia bila malipo yoyote yale.  


Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI

Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda alisema wananchi wengi waliowapa
hudumia katika kambi hiyo wamewakuta na matatizo mbalimbali ya moyo
ikiwemo shinikizo la juu la damu.

Dkt.Eva alisema baadhi ya wagonjwa waliowakuta na tatizo la shinikizo la juu la
damu wameacha kutumia dawa hiyo ni kutokana na kutokupata elimu ya kutosha
kuhusu ugonjwa huo kwani baada ya kupata naafuu waliacha kutumia dawa hizo. 


“Shinikizo la juu la damu lisipodhibitiwa linaleta madhara kwenye moyo ikiwa ni

pamoja na kutanuka kwa moyo na vifo vya ghafla hivyo basi tumewapa elimu
wananchi waweze kutumia dawa kwa usahihi na wasikatize dozi hata kama
watapata naafuu”, alisema Dkt. Eva.


Naye Maria Samlongo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Lishe wa Taasisi ya Moyo

Jakaya Kikwete (JKCI) alisema wananchi wengi aliowahudumia aliwakuta na tatizo
la kuwa na uzito mkubwa ambao unaweza kusababisha kupata magonjwa ya
moyo na kisukari na hivyo kuwapa elimu ya jinsi ya kuepukana na magonjwa hayo
kwa kufuata mtindo bora wa maisha.


“Nimewapa wananchi elimu ya kufuata mtindo bora wa maisha hii ikiwa ni

pamoja na kufanya mazoezi, kuepuka unywaji wa pombe uliopitiliza, kutotumia
bidhaa aina ya tumbaku na kula vyakula bora zikiwemo mboga za majani na
matunda”, alisema Maria.


Nao wananchi waliopata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo katika kambi

hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia vya
kutosha kuweza kutambua afya zao.


“Nimefika mahali hapa na kupata huduma ya vipimo, matibabu na elimu ya lishe

bora kwani sikuwa najua mengi kuhusu lishe lakini leo hii nimefahamu ni aina gani
ya vyakula ninavyotakiwa kuvila ili niwe na moyo wenye afya”. alisema Erick Urasa
mkazi wa Chanika Dar es Salaam.


“Nimepata huduma ya kupimwa vipimo mbalimbali vya moyo na nimepewa dawa

za presha na sukari bure bila kulipia chochote. Ninawaomba wananchi wenzangu
changamkieni fursa hii nanyi mje kupima moyo msiiache huduma hii ikawapita”,
alisema Mama Martha Kabelo mkazi wa Mbezi Dar es Salaam.
 

Comments

Popular posts from this blog

Wataalamu wa JKCI kufanya upasuaji wa moyo nchini Zambia

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024